Siku ya Afrika:Nishati,ushirikishwaji na mustakabali thabiti barani Afrika!
Na Paul Samasumo – Vatican.
Mkutano wa Siku ya Afrika ulitoa zaidi ya nafasi ya kutafakari kuhusu Afrika na mambo ya Afrika. Ulifanyika kama jukwaa madhubuti la kuakisi kile ambacho Afrika tayari inawakilisha leo hii kwenye jukwaa la kimataifa kama vile: bara mahiri lenye utajiri wa maliasili, mtaji wa watu na vijana wake wenye shauku ya kuunda bara lenye nguvu ambalo mara nyingi halieleweki. Sehemu kubwa na hasa vijana ilikaribisha jopo la wazungumzaji na wataalamu kutoka sekta mbalimbali—ikiwa ni pamoja na uchumi, mazingira, ushirikiano na udhibiti wa nishati, kwa mjadala mpana kuhusu mojawapo ya mada za dharura na za kimkakati za wakati wetu: Jukumu la Afrika katika mpito wa nishati duniani na mchango muhimu wa kizazi kipya katika kujenga mustakabali endelevu katika bara hili.
Siku ya Afrika na changamoto za nishati
Mkutano huo katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Santa Croce(Msalaba Mtakatifu) ulifunguliwa na kijana raia wa Togo anayeishi Roma, Bwana Isaac Kodjo Atchikiti, mtaalam wa fedha za tabianchi kutoka Chuo Kikuu cha Frankfurt cha Fedha na Usimamizi na mgombea wa udaktari wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Sapienza cha Roma. Bwana Atchikiti alisema bara la Afrika linahitaji kuunda Afrika yenye ustawi inayosukumwa na ushirikishwaji wa watu wote. "Ujumuishi wa vijana kwa bahati mbaya wakati mwingine hutumiwa tu kama kauli mbiu," alisema. Hata hivyo aliongeza kuwa, "Kuunda Afrika endelevu kunahitaji uchumi ulio wazi na dhabiti. Hii isiwe tu mikakati bali misingi ya msingi ya kujenga mustakabali ambapo tunaweza kusherehekea mafanikio yanayoonekana kwa watu wa Afrika." Bwana Atchikiti alidokeza umuhimu wa kuunganisha Ajenda ya Maendeleo ya Oslo kama njia inayowezekana. Hii ni kwa sababu inatetea maendeleo fungamani na endelevu kupitia mashauriano na ushirikiano wa wadau mbalimbali.
Mipango ya huduma ya nishati iliyofanywa katika vyumba vya bodi
Aliyefuata kuzungumza alikuwa Bi Musamamba Mubanga, kijana raia wa Zambia anayefanya kazi na Caritas Internationalis na pia yuko Roma. Bi Mubanga alitoa ushuhuda wa kuvutia, akitoa kutokana na uzoefu wake binafsi na kazi yake na Caritas Internationalis kuhusu uhusiano wa kina kati ya nishati, haki ya hali ya tabianchi, haki za binadamu, na usalama wa chakula. "Suala la kutengwa na huduma muhimu za nishati linasalia kuwa moja ya changamoto zetu za dharura," alisema. "Mipango ya nishati barani Afrika mara nyingi hubuniwa katika vyumba vya mikutano na miji mikuu mbali na jamii zilizoathirika." Alisisitiza kuwa nishati sio tu suala la mazungumzo ya kisera kwa Waafrika wengi bali ni mapambano ya kila siku ya kuishi. Bi Mubanga alisisitiza kuwa bado kuna hali katika baadhi ya nchi za Afrika ambapo 80% ya watu wanapata umeme mdogo. Nyumba nyingi, hasa katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, zinategemea sana mkaa katika kupikia—tabia inayochangia ukataji wa miti, kwani inahusisha kukata miti mingi. Ikiwa mabadiliko ya maana yanapaswa kuwa katika utoaji wa huduma za nishati, maoni ya watu wa kawaida na uzoefu wao wa maisha unahitaji kusikilizwa.
Maji na Nishati: Nguzo za maendeleo
Akizungumzia mitazamo ya udhibiti, raia wa Italia Bwana Fabio Tambone, Mkurugenzi wa Udhibiti katika ARER (Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati, Mitandao na Mazingira), alisisitiza kwamba "maji na nishati ni nguzo mbili ambazo maendeleo endelevu ya Afrika lazima yazingatie." Alibainisha kuwa Afrika ina rasilimali nyingi sana, inayotoa fursa kubwa na changamoto tata. "Ni muhimu kukuza mfumo wa usambazaji wa nishati," alishauri. "Bila kutumia mbinu hii, bado tutakuwa tukipambana na matatizo ambayo haitatatuliwa miaka ijayo," alisema. Bibi Isabela Stoll, Mkuu wa Mahusiano ya Kimataifa katika kampuni ya Usambazaji wa Nishashi( GSE ya Italia (Gestore dei Servizi Energetici), alitoa mtazamo wa kiutendaji kuhusu ushiriki wa Italia na kueleza uwezekano wa ushirikiano wa nishati kati ya Italia na nchi za Afrika. Mwanajopo mwingine, Bi Angela Cestari, Mtendaji wa Kundi la Cestari la Italia—shirika linalofanya kazi katika sekta ya nishati katika mataifa kadhaa ya Afrika—alifunga mjadala huo kwa mifano halisi ya kampuni ambayo imechagua kuwekeza kimaadili na kwa maono ya muda mrefu barani Afrika.
Harambee!
Tukio la Siku ya Afrika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Santa Croce lilitokana na ripoti ya ‘Harambee Africa International’ "Mapinduzi ya Kimya," ambayo inachunguza nafasi ya Afrika katika mpito wa nishati duniani. Harambee Kimataifa inataka kukuza maelewano kati ya Magharibi na Afrika. Neno ‘Harambee’ linatokana na neno la KiSwahili linalomaanisha “tuvutane, tufanye kazi pamoja” au “tuungane.” Inajumuisha ari ya jumuiya ya kujisaidia na juhudi za pamoja, zilizokita mizizi katika tamaduni na mila za Kiafrika. Dhana hiyo ilienezwa na Jomo Kenyatta, Rais wa kwanza wa Kenya. Harambe inasalia kuwa kichocheo kikuu cha maendeleo na ushiriki unaoongozwa na jamii nchini Kenya.
Siku ya Afrika
Tukio la Siku ya Afrika, ambalo zamani lilijulikana kama 'Siku ya Uhuru wa Afrika' na kisha 'Siku ya Ukombozi wa Afrika', lina asili yake katika upinzani wa pamoja wa Waafrika dhidi ya ukoloni na unyonyaji wa kiuchumi. Katika bara na kwa wale walioko ughaibuni, Siku ya Afrika inaadhimishwa kama wakati wa kusherehekea na kuaakisi msisimko wa tamaduni, mavazi, vyakula na tamaduni mbalimbali za watu wa Afrika.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kusasisha kwa kujiandikisha kwenye jarida letu la kila siku: Just click here