MAP

Papa Leo wa XIV ni kiongozi anayelifahamu Bara la Afrika kama Mkuu wa Shirika la OSA, Kama Askofu na Kama Kardinali mwenye dhamana ya kuongoza Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu. Papa Leo wa XIV ni kiongozi anayelifahamu Bara la Afrika kama Mkuu wa Shirika la OSA, Kama Askofu na Kama Kardinali mwenye dhamana ya kuongoza Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu.  (Ordine di Sant'Agostino )

Askofu Musomba, OSA: Papa Leo XIV Analifahamu Sana Bara la Afrika

Baba Mtakatifu Leo wa XIV ni kiongozi mwenye ufahamu mpana sana wa maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika, kwanza kama Mkuu wa Shirika la Waagustianini Duniani, Kama Askofu alipata nafasi ya kutembelea nchi kadhaa Barani Afrika zikiwemo: Kenya, DRC na Kusini mwa Tanzania. Alitoa hamasa kwa Shirika kuwekeza katika rasilimali watu na matokeo yake ni Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA wa Jimbo Katoliki Bagamoyo nchini Tanzania

Na Sarah Pelaji – Vatican.

Wakati Kanisa Katoliki Ulimwenguni likiwa linasherehekea kupata Baba Mtakatifu Mpya ambaye amechaguliwa Mnamo tarehe 8 Mei 2025 Habemus Papam Robertum Franciscum Prevost qui sibi nomen imposuit Leonem XIV ambaye kwa jina lake kamili ni Kardinali Robert Francis Prevost wa Shirikila la Mtakatifu Augustino ambaye ni raia wa Marekani na kuchagua jina la Upapa wake kuwa LEO XIV, imeelezwa kuwa ni Papa ambaye ana uhusiano wa karibu na Afrika kwani ametembelea nchi ya Tanzania na Kenya wakati alipokuwa Mkuu wa Shirika hilo Duniani. Pia inaelezwa kuwa anazo karama za uongozi kutokana na kuwa Mkuu wa Shirika la Waagustinian kwa takribani miaka 12, ikiwemo pia hekima, unyenyekevu, mpenda amani na umoja kama ilivyo kauli mbiu yake ya ‘Sisi ni wakristo wengi, katika Kristo mmoja sisi ni wamoja.’

Papa Leo XIV analifahamu sana Bara la Afrika
Papa Leo XIV analifahamu sana Bara la Afrika   (Ordine di Sant'Agostino)

Askofu Stephano Lameck Musomba OSA wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo ameeleza kuwa amefurahia uchaguzi wa Papa mpya ambaye ni mwanafamilia wa Shirikila la Kimataifa la Mtakatifu Agustino. Anasema kuwa, anamfahamu Papa Mpya kwasababu alikuwa Mkuu wa Shirika tangu mwaka 2001 mpaka 2013. Hivyo kama wanashirika waliishi kama wanafamilia wakitekeleza na kuziishi karama za Mtakatifu Augustino kwa pamoja. “Binafsi ninamfahamu kwani alifika Tanzania mwaka 2003 kipindi ambacho nilipata Daraja Takatifu la Upadri. Yeye alifika Agosti 2003 na mimi nilipata Daraja Takatifu ya Upadri Julai mwaka 2003. Badaye mwaka 2004 nilienda Roma masomoni katika Chuo cha Kipapa cha Mtakatifu Augustino wakati yeye alikuwa Mkuu wa Shirika Duniani. Nimekaa naye katika nyumba moja katika Makao Mkauu ya Shirika Roma jengo lililopo karibu na Vatican hivyo ninamfahamu vizuri si kwa kusikia kwa watu bali kwa kuishi naye,” amesema Askofu Musomba.

Papa Leo XIV akiwa na wanashirika wa OSA Barani Afrika
Papa Leo XIV akiwa na wanashirika wa OSA Barani Afrika   (Ordine di Sant'Agostino)

Badaye alipomaliza masomo yake Mkuu wa Shirika Padri Robert Francis Prevost alimteua Askofu Msomba wakati huo Padri Musomba kuwa mjumbe wa Kamati ya Waagustiniani Kimataifa mpaka alipomaliza muda wake wa uongozi wa Shirika mwaka 2013 alipochaguliwa kuwa Askofu. Pia amekutana naye kwenye vikao mbalimbali hasa walipofanya mkutano huko Kinshasa DRC wa Familia ya Waagustiniani wanaoishi Barani Afrika, AFA. Hivyo walikuwa pamoja naye. “Alinipigania sana kwenda kusoma na ni yeye alimwomba Mkuu wa Shirika huku Tanzania kuwa ninafaa kwenda kujiendeleza kitaaluma. Katika hili ninamkumbuka sana,” amesistiza Askofu Musomba. Akielezea kuhusu karama za Papa Mpya Leo XIV kuwa ni mtu anayesoma alama za nyakati kama ambavyo Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unavyoelekeza ili kuzitafsiri kadiri ya tunu na mwanga wa Injili. Ameliongoza Shirika la Waagustiniani Ulimwenguni kwa miaka 12 kwa hekima, busara na maarifa makubwa. Anao uwezo mkubwa wa uongozi hivyo sina mashaka naye.

Papa Leo XIV wakati wa uongozi wake alikazia elimu kwa wanashirika wake
Papa Leo XIV wakati wa uongozi wake alikazia elimu kwa wanashirika wake   (Ordine di Sant'Agostino)

Askofu Musomba ameeleza kuwa, alipoitembelea Tanzania alikwenda maeneo ya kusini mwa Tanzania yaani Songea katika eneo la Mahanje na alizunguka karibu jimbo kuu la Songea. Kisha akaenda Jimboni Morogoro kwa ajili ya kupokea nadhiri za daima za maburuda wa Shirika lake la Waagustiniani. “Katika safari hiyo nilikuwa na yeye ndiye aliendesha gari kuonesha ushujaa na unyenyekevu wake kwa watu wake,” ameeleza. Amelitaka Kanisa la Kiulimwengu kuwa na imani na Papa Leo XIV kwani anao uwezo na mang’amuzi mapana ya uongozi. Pia kila mmoja ampe zawadi ya sala ili apate nguvu, afya na hekima ya kuliendeleza Kanisa la kiulimwengu kwani kwa sasa ni Baba wa Katika Katoliki la kiulimwengu. Ameelezea kauli mbiu ya Papa Leo wa XIV ya Sisi ni wakristo wengi, katika Kristo mmoja sisi ni wamoja ’ akisema anahamasisha umoja baina ya Wakristo kwani mwili wa Kristo ni mmoja haujagawanyika. Watu wakiwa wamoja wataishi kwa amani na upendo ambalo ni zawadi ya kwanza ya Yesu alipofufuka. Anamwombea Papa Leo XIV: afya njema na ufanisi katika kuliongoza Kanisa la Mungu. Kutokana na Mtandao wa “Aciafrika”, Papa Leo XIV, akiwa Robert Francis Kardinali Prevost, alitembelea Kenya mnamo Desemba 2024, alitafakari juu ya haja ya kulipa kipaumbele Neno la Mungu kama "roho na uzima" na nafsi ya Yesu Kristo kama chanzo cha "uzima wa kweli" na msingi wa Kanisa. Akiwa Kenya Kardinali Prevost, aliongoza Ibada ya kutabaruku Kanisa jipya la “Augustinian International House of Theology” huko Karen, Nairobi Kenya. Papa Leo wa XIV amefanya huduma mbalimbali za baada ya kupewa Daraja Takatifu ya Upadre mwaka 1982, Padri Prevost alitumwa Peru mwaka 1985 kama mmisionari.  Alitumikia katika maeneo mbalimbali ya Peru, ikiwa ni pamoja na Chulucanas na Trujillo, ambako alihudumu kama: Paroko, Mkurugenzi wa malezi, mwalimu wa sheria za kanisa, na Jaji wa Mahakama ya Kanisa. Mnamo mwaka 1999, alichaguliwa kuwa Mkuu wa  Shirika la Augustino Kanda ya Chicago, na mwaka 2001 alichaguliwa kuwa mkuu wa Shirika hilo duniani, nafasi aliyoitumikia hadi mwaka 2013.

Watu wa Mungu nchini Uganda wameadhimisha Misa kwa ajili ya Papa Leo XIV
Watu wa Mungu nchini Uganda wameadhimisha Misa kwa ajili ya Papa Leo XIV

Kwa ufupi kabisa: Baba Mtakatifu Robert Francis Prevost, wa Shirika la Mtakatifu Augustino, O.S.A., Leo wa XIV, alizaliwa tarehe 14 Septemba 1955, Jimbo kuu la Chicago, Illinois, nchini Marekani. Tarehe 29 Agosti 1981 akaweka nadhiri za daima kwenye Shirika la Mtakatifu Augustino, O.S.A. Tarehe 19 Juni 1982 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 14 Septemba 2001 akachaguliwa kuwa ni Mkuu wa Shirika la Mtakatifu Augustino hadi tarehe 4 Septemba 2013. Tarehe 26 Septemba 2015, Hayati Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Chiclayo, nchini Perù. Tarehe 30 Januari 2023 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Rais wa Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Maaskofu na Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini na kumpandisha cheo na hivyo kuwa ni Askofu mkuu. Tarehe 12 Aprili 2023 akasimikwa rasmi kuwa Rais wa Baraza la Kipapa kwa Ajili ya Maaskofu na Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini na hivyo kuchukua nafasi ya Kardinali Marc Armand Ouellet, aliyekuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu. Tarehe 30 Septemba 2023 akasimikwa kuwa Kardinali. Mwadhama Kardinali Robert Francis Prevost, wa Shirika la Mtakatifu Augustino, O.S.A., ndiye Baba Mtakatifu, wa 267 aliyechaguliwa na Baraza la Makardinali katika mkutano wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Askofu mkuu wa Roma, kama alivyotangazwa na Kardinali Shemasi Dominique Mamberti, Alhamisi tarehe 8 Mei 2025 na amechagua jina la Leo wa XIV.

Papa Leo XIV na Afrika
10 Mei 2025, 15:39