ĐÓMAP”Œșœ

Kazi ya hadhi kwa wote:jumbe za mapapa watatu wa mwisho

Iliwakilishwa video yenye nia za maombi ya Papa wa kwa mwezi Mei:Kwa njia ya kazi kila mtu ajikamilishe,familia iweze kuhifadhi hadhi na jamii iweze kuwa ya kibinadamu zaidi.Katika Mafundisho ya Papa Yohane Paulo II,Benedikito wa XVI na Papa Francisko inaonesha kuwa watu lazima wawe kitovu na kipaumbele cha kazi ulimwenguni.Mtandao wa Maombi ya Kimataifa unaomba Bwana kupata Papa mpya aweze kukabiliana na changamoto za ubinadamu na utume wa Kanisa.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika uchapishaji wa kila mwaka wa nia za maombi kwa 2025, Papa Francisko alitualika kusali kwa Mei "Kwa hali ya kazi." Kutokana na kifo chake, video inayoambatana na nia hii ya maombi inabadilishwa muundo wake ili kuhimiza tafakari inayokumbuka baadhi ya maneno ya Mapapa watatu wa mwisho kuanzia na Yohane Paulo II, Benedikto XVI na Francisko, kuhusu mada hii. Katika Video ya Papa kwa mwezi Mei, iliyotayarishwa kwa msaada wa Chama cha Wafanyabiashara cha Roma na Mtandao wa Maombi ya Ulimwengu wa Mfuko wa Papa na kusambazwa na Mtandao nia za Maombi ya Papa Ulimwenguni, ambaye anatualika kusali ili kwa njia ya  kazi, kila mtu aweze kujitimizwa, familia ziweze kusaidiwa kwa hadhi  na jamii ipate kuwa ya kibinadamu zaidi.

Picha zinazoambatana na maneno ya Mapapa zinaleta pamoja mang’amuzi mbalimbali ya maisha yanayozunguka ulimwengu wa kazi. Kwanza kabisa, kuna duka la useremala, lenye sanamu ya Mtakatifu Yoseph seremala iliyochongwa kwa mkono katika karne ya kumi na tisa, katika mbao za chokaa, na wachongaji mahiri wa Val Gardena; kuna hali halisi mbalimbali za mji wa Kimataifa wa Loppiano wa Wafocolari, ikiwa na maabara ya kutengeneza vitu vya udogo wa mfinyanzi, ushirika wa kilimo, kampuni inayohusika na ufungaji na kumaliza makala nyingi - ambayo kazi ni uzoefu katika mtazamo wa ushirika. Kuna baadhi ya picha zenye kusisimua za unyonyaji ambazo mamilioni ya wafanyakazi wanateseka katika sehemu mbalimbali za dunia.

Watoto milioni 160 wanaolazimishwa kufanya kazi.

Ulimwengu wa kazi umekuwepo sana katika mafundisho ya Kanisa tangu mwisho wa karne ya 19: matokeo ya mtazamo wa makini wa Mapapa juu ya ukweli na wasiwasi wao kwa ajili ya ustawi wa kiroho na kimwili wa watu. Kwa sasa, kulingana na takwimu kutoka UN na ILO, watu milioni 402.4 duniani kote hawawezi kupata kazi; watoto milioni 160 wanalazimishwa kufanya kazi; Wafanyakazi milioni 240 wanapata chini ya dola 3.65 kwa siku; na zaidi ya 60% ya watu hai duniani wanafanya kazi katika uchumi usio rasmi, ambayo ina maana kwamba takriban watu bilioni 2 wanakosa haki za kazi na ulinzi wa kijamii.

Mapapa na ulimwengu wa kazi

Maneno ya Papa Fransisko yanasisitiza kwamba kazi huleta "upako wa hadhi": hupata mkate na humpatia heshima mtu. Yesu mwenyewe alifanya kazi ya useremala, “kazi ngumu sana” ambayo “haikuhakikisha mapato makubwa,” na ambayo alishiriki pamoja na wafanyakazi wote katika historia. Baadhi ya maneno ya Papa Benedikto XVI yanasisitiza umuhimu mkuu wa kazi “kwa ajili ya utimilifu wa mwanadamu na kwa maendeleo ya jamii.” Kama tokeo hili, kazi lazima iandaliwe na ifanywe kwa heshima kamili kwa ajili ya utu na kwa ajili ya manufaa ya wote.” Wakati huo huo, mwanadamu lazima asijiruhusu kufanywa mtumwa wa kazi (...) akidai kupata ndani yake maana ya mwisho na ya uhakika ya maisha ambayo yanaweza kupatikana kwa Mungu tu. Hatimaye, maneno ya Mtakatifu Yohane Paulo II yanatuhimiza kushughulikia kukosekana kwa usawa wa kiuchumi na kijamii na hali ya ukosefu wa haki iliyopo katika ulimwengu wa kazi, tukiweka “hadhi ya wanaume na wanawake wanaofanya kazi, uhuru wao, wajibu na ushiriki wao.” Haya yote, bila kusahau wale ambao wanakabiliwa na ukosefu wa ajira, ujira wa kutosha, na ukosefu wa nyenzo. Kwa hakika kukosekana kwa usawa huku na hali hizi za dhulma zinatufanya tuombe kwamba kitovu cha kazi na maisha ya kiuchumi na kijamii ni mwanadamu, na sio faida.”

Ustawi wa pamoja

Lorenzo Tagliavanti, rais wa Chama cha Wafanyabiashara cha Roma, alisema “kazi ni kama hewa: unatambua thamani yake inapokosekana.” Kulingana na Mafundisho ya Kijamii ya Kanisa, kazi ni haki ya msingi ya binadamu na jambo la kuamua kwa ajili ya utimilifu wa kibinafsi wa kila mtu na kwa ajili ya maendeleo ya jamii yenye usawa zaidi na inayounga mkono: nyanja zote ambazo kila siku, kama taasisi ya marejeo ya jumuiya ya kiuchumi ya Roma na eneo lake, tunajaribu kufanya tuwezavyo, pamoja na wafanyabiashara na wafanyakazi. Nia hii ya maombi, ambayo huambatana na Jubilei ya wafanyakazi na ile ya wajasiriamali, kwa hivyo inatupatia fursa ya kusisitiza ahadi iliyotolewa mnamo 1831, Tagliavanti alisema: "Niruhusu, kukumbuka maneno ya Papa Francisko katika 2023 kwa kikundi cha wajasiriamali wa Kifaransa: 'ikiwa ni kweli kwamba kazi humpa mwanadamu heshima, ni kweli zaidi kwamba ni mwanadamu ambaye hutukuza kazi.” Na kwa hakika umakini huu kwa mwanadamu ndio unaotutia motisha katika kazi yetu ya kila siku, katika kutafuta kielelezo cha maendeleo chenye mwelekeo wa ustawi unaoshirikishwa na wote.”

Kazi na heshima

Dhana nyingine inayosisitizwa na Mapapa ni kwamba thamani ya kazi inakwenda vizuri zaidi ya nyanja yake ya kiuchumi. “Tukiwauliza watoto kumi kile wanachotaka kufanya watakapokuwa wakubwa,” alisema Stefano Simontacchi, mshiriki mwanzilishi na mshiriki wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Mtandao wa Maombi ya Papa Ulimwenguni “huenda tutapata majibu kumi tofauti, kwa sababu matarajio ya kila mtu ni tofauti: kama vile katika mfano wa talanta, kiukweli, kila mmoja amepewa yake mwenyewe, na kazi ni uwezekano wa kuifanya kuzaa matunda, kutambua utu wa mtu. Katika kazi, kiukweli, kuna mengi zaidi ya uhuru wa kiuchumi, ambayo pia ni muhimu: kuna mchango ambao mtu hutoa kwa jamii, na kwa sisi waamini pia kushiriki katika kazi ya Mungu ya uumbaji. Papa Francisko alitumia usemi mzuri sana kufafanua haya yote: aliita kazi kama ‘upako wa hadhi’, na upako huu wa hadhi ndiyo hasa unaoleta tofauti katika maisha yetu.” Hata zaidi katika enzi hii ya mabadiliko makubwa, kama vile Akili Mnemba(AI), ambayo lazima itusukume kukuza mifumo ya mshikamano kama aina ya mshikamano wa kijamii. Shukrani, heshima na mshikamano lazima viwe dira yetu”.

Kazi yenye heshima na kipaumbele

Mkurugenzi wa Kimataifa wa Mtandao wa Nia za Maombi ya Papa Ulimwenguni Pote, Padre  Cristóbal Fones, S.J., alieleza kwamba, kwa Mtakatifu Yohane Paulo II, mwanadamu anaitwa kufanya kazi kwa usahihi “kwa sababu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu:”ni Bwana hasa anayempa uwezekano wa kushiriki katika kazi yake ya uumbaji kupitia kazi. Katika Waraka wa Kitume wa  Laborem exercens, Papa Paulo  II anatuambia kwamba kupitia kazi yetu, hadhi yetu ya  binadamu, umoja wa kidugu na uhuru lazima kuongezeka duniani. Kazi ya Mkristo, pamoja na maombi yake, hufanya ulimwengu uendelee na, lililo muhimu zaidi, huchangia maendeleo ya Ufalme wa Mungu.”

 Padre  Fones, aliendela "Kwa msingi huu, mrithi wake, Benedikto XVI, alisema katika waraka wa Caritas kwa uthibitisho kwamba hadhi ya mtu inahitaji kwamba uchaguzi wa kiuchumi usiongeze ukosefu wa usawa, na kwamba kazi yenye heshima kwa wote ni lengo la kipaumbele. Papa Benedikto alihakikishia kwamba umaskini, mara nyingi, ni matokeo ya ukiukwaji wa heshima ya kazi ya binadamu: wakati mwingine uwezekano wa mtu ni mdogo, kama katika kesi ya ukosefu wa ajira au ukosefu wa ajira; na nyakati nyingine haki ya kupata mshahara wa haki au usalama wa mfanyakazi na familia yake haiheshimiwi." Kwa maana hiyo, Fr. Fones alisisitiza mwendelezo wa hukumu ya Baba Mtakatifu Francisko na ile ya watangulizi wake: "Papa Francisko anatuambia kwamba kazi ni takatifu. Ndiyo njia tunayopaswa kujenga jamii zaidi ya wanadamu."

Ikiwa tunataka jamii yenye uadilifu zaidi, ni lazima tukuze ajira yenye heshima, imara, inayofanywa katika mazingira yenye afya na kwa hatua za kutosha za usalama, ambazo zinahusisha kuheshimu haki za kimsingi na ulinzi wa kijamii, pamoja na mshahara unaoruhusu familia kudumisha hali nzuri ya maisha. Hili litawezekana ikiwa tutapata thamani ya kweli ya kazi, ikiwa tutaacha mantiki ya faida kwa gharama yoyote na kuweka watu katikati, hasa wale ambao leo hawawezi kuishi kwa njia ya kibinadamu. Hatimaye, katika muktadha wa Mwaka Mtakatifu wa 2025, Video ya Papa inapata umuhimu fulani, kwa sababu inatujulisha nia za maombi ya papa. Ili kupata neema ya raha ya Yubile, lazima tuombe nia hizi.

Nia za Papa
06 Mei 2025, 09:46