MAP

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Waamini Wakatoliki kutoka katika Makanisa ya Mashariki kuanzia tarehe 12 hadi 14 Mei 2025. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Waamini Wakatoliki kutoka katika Makanisa ya Mashariki kuanzia tarehe 12 hadi 14 Mei 2025.  (ANSA)

Hotuba ya Papa Leo XIV Kwa Wanajubilei wa Makanisa ya Mashariki: Ushuhuda

Mahujaji wa Makanisa ya Mashariki wamekuwa wa kwanza kukutana na Papa Leo XIV mjini Vatican, katika kipindi hiki cha Pasaka, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo. Katika hotuba yake amekazia kuhusu amana na utajiri wa Makanisa ya Mashariki; Kiliturujia na Kinidhamu na kwamba, Makanisa ya Mashariki ni shuhuda wa imani, matumaini na mapendo na kwamba, viongozi wa Makanisa ya Mashariki waendelee kuwa ni wajenzi wa Kanisa la Kisinodi na udugu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hayati Baba Mtakatifu Francisko, katika mkesha wa Noeli tarehe 24 Desemba 2024 alifungua Lango Kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, mwanzo wa Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo. Hili ni Lango la matumaini, chemchemi ya watu wote wa Mungu. Maadhimisho ya Jubilei ni kwa ajili ya watu wote, ili kuwaonjesha tena matumaini ya Injili, matumaini ya mapendo na matumaini ya msamaha wa kweli. Alisema, Pango la Noeli ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; chemchemi ya matumaini; upendo wa Mungu unaovunjilia mbali ukaidi wa mwanadamu pamoja na hofu yake, tayari kutafakari ukuu wa matumaini yaliyo mbele ya mwanadamu. Mwelekeo huu, uwe ni mwangaza wa mapito ya kila siku ya mwanadamu. Ni katika muktadha wa usiku huu ambapo “Lango Takatifu” la Moyo wa Mungu lilifunguliwa. Kristo Yesu, Mungu pamoja nasi, alizaliwa kwa ajili ya binadamu wote. Kumbe, pamoja naye, furaha ya dunia inachanua kama “maua ya kondeni.” Pamoja na Kristo Yesu, maisha yanabadilika na pamoja na Kristo Yesu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5. Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa matumaini.” Matumaini ya waamini yako katika Msalaba, yaani katika Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa Katoliki huheshimu sana taasisi, madhehebu ya Kiliturujia, Mapokeo ya Kikanisa pamoja na Nidhamu ya maisha ya Kikristo ya Makanisa ya Mashariki “Orientalium ecclesiarum.” Maana ndani yake, maadamu ni maarufu kwa ukale wake mstahiki, hung’ara mapokeo yatokanayo na Mitume kwa njia ya Mababa; na Mapokeo hayo ni sehemu ya hazina iliyofunuliwa na Mwenyezi Mungu na isiyogawanyika ya Kanisa lote zima. Makanisa ya Mashariki ni shuhuda hai wa Mapokeo haya ya Kanisa. Orientalium ecclesiarum, 1.

Wana Jubilei wa Makanisa ya Mashariki wakihudhuria Mkutano na Papa Leo XIV
Wana Jubilei wa Makanisa ya Mashariki wakihudhuria Mkutano na Papa Leo XIV   (ANSA)

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Waamini Wakatoliki kutoka katika Makanisa ya Mashariki, kuanzia tarehe 12 Mei hadi tarehe 14 Mei 2025 wamekuwa wakishiriki katika maadhimisho ya Jubilei kwa Makanisa ya Mashariki na hatimaye, Jumatano tarehe 14 Mei 2025 wamekuwa ni mahujaji wa kwanza kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Leo XIV mjini Vatican, katika kipindi hiki cha Pasaka, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo. Katika hotuba yake amekazia kuhusu amana na utajiri wa Makanisa ya Mashariki; Kiliturujia na Kinidhamu na kwamba, Makanisa ya Mashariki ni shuhuda wa imani, matumaini na mapendo na kwamba, viongozi wa Makanisa ya Mashariki waendelee kuwa ni wajenzi wa Kanisa la Kisinodi, Udugu wa kibinadamu na uwajibikaji wa pamoja; ukweli na uwazi katika matumizi ya mali ya Kanisa. Makanisa ya Mashariki ni amana na utajiri mkubwa kwa Mama Kanisa kutokana na utofauti, mateso, madhulumu na nyanyaso ambazo waamini wengi wa Makanisa ya Mashariki wamepitia. Haya ni Makanisa yenye amana na utajiri mkubwa wa hekima na maisha ya kiroho, Mapokeo na kwamba, yamekuwa mstari wa mbele katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Ni Kanisa lenye utajiri mkubwa wa Mababa wa Kanisa pamoja na Monasteri na kwamba, wanayo nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa kama ambavyo Papa Leo XIII alivyobainisha na kukazia umuhimu wa kuheshimu na kuthamini Liturujia pamoja na nidhamu ya maisha ya Kikristo kwa ajili ya sifa na utukufu wa Kanisa.

Makanisa ya Mashariki: Amana na Utajiri wa Liturujia na Sala
Makanisa ya Mashariki: Amana na Utajiri wa Liturujia na Sala   (@Vatican Media)

Waamini wa Makanisa ya Mashariki wanateseka sana kwani kuna baadhi yao wanalazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita, nyanyaso na madhulumu; ukosefu wa amani na utulivu pamoja na umaskini; mambo yanayohatarisha utambulisho wao wa maisha ya kiroho pamoja na kupoteza ardhi, hali inayotishia kutoweka kwa amana na utajiri wa Makanisa ya Mashariki. Wakristo wa Makanisa ya Mashariki walioko ugenini “Diaspora” wanapaswa kuheshimu na kutunza madhehebu ya Mashariki. Baba Mtakatifu Leo XIV analitaka Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki kumsaidia katika kuweka kwa usahihi: Kanuni, Sheria na Miongozo, ili Maaskofu wa Madhehebu ya Kilatini, waweze kuwasaidia waamini wa Makanisa ya Mashariki, huku wakishuhudia Mapokeo ya Makanisa ya Mashariki na hivyo kutajirisha Makanisa ya Kilatini.Papa Leo XIV anakaza kusema, Mama Kanisa anawahitaji waamini wa Makanisa ya Mashariki ili kuendelea kuvumbua mafumbo ya imani yanayoendelea kujikita katika Liturujia inayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili na hivyo kumwezesha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani na kwamba, kuna haja pia ya kutambua na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu katika maisha; kukuza na kudumisha tasaufi ya Makanaisa ya Mashariki inayofumbatwa katika: Kufunga na kusali; toba na wongofu wa ndani pamoja na majuto ya kweli kwa dhambi zao binafsi na zile zinazotendwa na walimwengu na kamwe wasithubutu kuyumba kutoka kwenye Mapokeo yao kwa kuelemewa na tabia ya ulaji wa kupindukia. Mapokeo yao ya tasaufi ni dawa, chemchemi ya huruma ya Mungu na matumaini yanayobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba kama ambavyo Mtakatifu Efremu wa Siria anavyokiri na kwamba, dhambi kubwa kwa waamini ni kutoamini juu ya nguvu ya Fumbo la Ufufuko.

Papa Leo XIV akipewa zawadi na viongozi wa Makanisa ya Mashariki
Papa Leo XIV akipewa zawadi na viongozi wa Makanisa ya Mashariki   (ANSA)

Makanisa ya Mashariki ni shuhuda wa imani. Hawa ni wale waamini wanaotoka katika Nchi Takatifu, Ukraine, Lebanon, Siria pamoja na Mashariki ya Kati; Ethiopia bila kusahau Mashariki mwa Asia. Katika mateso, dhuluma na nyanyaso hizi, Kristo Yesu mwenyewe anasema: “Amani iwe nanyi: anaendelea kusema: “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.” Yn 14:27. Amani ya Kristo ni zawadi inayopyaisha maisha, changamoto na mwaliko kwa waamini anasema, Baba Mtakatifu Leo XVI ni kumwomba Kristo Yesu ili aweze kuwakirimia amani ya kudumu inayofumbatwa katika upatanisho na msamaha pamoja na ujasiri wa kuanza upya. Papa Leo XIV anasema, diplomasia ya Vatican inapania kuwaunganisha na kuwakutanisha maadui uso kwa uso; kuwajengea matumaini wale watu waliovunjika na kupondeka moyo; kulinda na kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu pamoja na amani. Kwa hakika walimwengu wanatamani sana kuona kwamba, amani inatawala.

Makanisa ya Mashariki yana amana na utajiri mkuwa: Tasaufi na Sala
Makanisa ya Mashariki yana amana na utajiri mkuwa: Tasaufi na Sala   (@Vatican Media)

Huu ni muda wa kukutana, kuzungumza na kujadiliana kwani amani ya kweli inawezekana na kwamba, umefika wakati kwa silaha kukaa kimya, kwani silaha hazileti suluhu ya matatizo ya watu wa Mungu, bali zinaongeza matatizo na magumu ya maisha. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kuimarisha udugu wa kibinadamu kwa kukataa dhana ya kudhaniana vibaya kama maadui au wahalifu wanaopaswa kuchukiwa, bali ni watu ambao wanaweza kuzungumza. Huu ni mwaliko wa walimwengu kukataa kugawanywa kwenye makundi ya watu wema na wabaya! Baba Mtakatifu Leo XIV anawashukuru na kuwapongeza wale wote katika hali yao ya ukimya, sala na sadaka wanapandikiza mbegu ya amani. Wakristo wa Mashariki wana haki ya kupewa fursa ya kubaki katika nchi zao wenyewe! Baba Mtakatifu Leo XIV anawashukuru na kuwapongeza Wakristo wa Makanisa ya Mashariki kwa kuendelea kuwa ni mwanga angavu katika: katika imani, matumaini na mapendo. Makanisa ya Mashariki yaendelee kuwa ni mfano bora wa kuigwa na viongozi wao wawe ni waragibishaji wa ushirika na uadilifu hususan katika maadhimisho ya Sinodi. Makanisa yawe ni mahali pa ujenzi wa udugu wa kibinadamu na uwajibikaji wa pamoja; ukweli na uwazi katika usimamizi na matumizi ya mali za Kanisa; wawe ni kielelezo cha unyenyekevu, sadaka na majitoleo kwa watu wa Mungu, pamoja na kuondokana na uchu wa madaraka, ukuu na kutaka kujionesha. Hii ni changamoto ya kujimanua kutoka katika malimwengu na yale yote yanayokwenda kinyume cha ushirika, ili kuendelea kuwa waaminifu katika utii na ushuhuda wa Kiinjili. Baba Mtakatifu Leo XIV amewapatia baraka zake za kitume na kuwasihi kuendelea kusali kwa ajili ya Kanisa pamoja na ufanisi katika utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Jubilei Makanisa ya Mashariki

 

14 Mei 2025, 16:38