Hotuba ya Papa Leo XIV Kwa Vyombo Vya Mawasiliano ya Jamii
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa tarehe 4 Desemba 2023 aliadhimisha kumbukizi ya Miaka 60 tangu Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha “Tamko la Inter Mirifica” yaani “Kati ya Mambo ya Ajabu: Kuhusu Vyombo Vya Upashanaji Habari.” Hili ni tamko ambalo limeleta mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki mintarafu vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Hii ni hati ambayo ilifungua malango kwa tafakari ya kisasa, taratibu, kanuni maadili na utu wema juu ya mawasiliano yanayotekelezwa na Mama Kanisa na kwamba, amana na mchango wake unaendelea kung’ara hata katika ulimwengu mamboleo unaoendelea kushuhudia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Vatican wanasema, vyombo hivi kama vikitumiwa vyema vyaweza kuleta faida kubwa kwa binadamu. Vinatoa mchango mkubwa katika ukuzaji na ustawishaji wa nafsi za watu na pia katika uenezaji na uimarishaji wa Ufalme wa Mungu.
Vyombo hivi vinapotumika kinyume cha maongozi ya Mwenyezi Mungu vinaweza kusababisha madhara na hivyo kusababisha huharibifu kwa Jumuiya ya watu. Kimsingi Inter Mirifica iligusia mwongozo kwa matumizi manyofu ya vyombo vya upashanaji habari; kwa kuangalia wajibu wa Kanisa, Kanuni maadili, Haki ya upashanaji habari, sanaa na maadili; Onesho la ubaya wa kimaadili, maoni ya umma, wajibu wa wapokeaji, wajibu wa vijana na wazazi, wajibu wa watunzi sanjari na wajibu wa Serikali. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipembua kwa kina na mapana kuhusu vyombo vya upashanaji habari na kazi ya kitume, inayotekelezwa na Mama Kanisa, kwa kuangalia kazi ya wachungaji na waamini; utendaji wa waamini; mafunzo ya watunzi, malezi na majiundo ya wapokeaji, vifaa na misaada. Mtaguso Mkuu wa Vatican ndio uliopitisha azimio la maadhimisho ya Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni, ili kuwakumbusha waamini kuhusu wajibu wao katika mchakato mzima wa mawasiliano ya jamii, ili kuchangia katika maboresho na ustawi wa miradi inayoendeshwa na kusimamiwa na Mama Kanisa katika sekta ya mawasiliano ya jamii na kuendelea kusoma alama za nyakati.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 12 Mei 2025 amezungumza na wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii Kimataifa waliofika mjini Vatican kushuhudia uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na wafanyakazi wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano. Papa Leo XIV ametumia fursa hii kuwashukuru wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kwa mchango wao mkubwa ambao ni neema kwa Mama Kanisa katika maisha na utume wake. Amekazia umuhimu wa kulinda na kudumisha amani; mshikamano wa Mama Kanisa na waandishi wa habari waliofungwa au kupotea katika mazingira tatanishi; waandishi wa habari ni wahudumu wa ukweli; umuhimu wa kutumia vyema rasilimali muda; umuhimu wa mawasiliano kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya watu wa Mataifa; Matumizi ya teknolojia ya akili unde “Artificial Intelligence” na kwamba, Vyombo vya mawasiliano ya jamii visaidie kukuza na kudumisha kiu ya haki na upendo, ili kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, mawasiliano yasaidie kujenga amani. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, “Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu.” Mt 5:9. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kujikita katika mchakato wa kutafuta, kujenga na kudumisha Injili ya amani inayopata chimbuko lake katika moyo wa kila mtu, jinsi watu wanavyoangaliana, wanavyosikilizana na kuzungumza na wengine, mwaliko wa kukataa vita ya maneno na matendo.
Mama Kanisa anapenda kuonesha mshikamano wake na wadau wa mawasiliano waliofungwa kutokana na kazi yao ya kutafuta na kutangaza ukweli, wanapaswa waachiliwe mara moja. Kuna waandishi wa habari wanaohatarisha maisha yao kwa kuwa mstari wa mbele, ili kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu; haki ya kuhabarishwa, ili kufanya maamuzi ya kina. Waandishi wa habari waliofungwa wanaleta changamoto kwa dhamiri hai kwa Mataifa na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake; huu ni wito na mwaliko wa kulinda na kuheshimu uhuru wa habari sanjari na uhuru wa vyombo vya mawasiliano. Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru wadau wa mawasiliano ambao wamekuwepo hapa mjini Roma ili kutoa habari kuhusu maisha na utume wa Kanisa; katika utofauti na umoja wake. Wanahabari wamekuwepo wakati wa maadhimisho ya Juma kuu, alipofariki Baba Mtakatifu Francisko katika mwanga wa Pasaka ambao uliwaingiza Makardinali katika mkutano wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kiasi kwamba, wakafanikiwa kutangaza uzuri wa upendo wa Kristo Yesu, unao waunganisha watu na hivyo kuwawezesha kuwa wamoja, huku wakiongozwa na Mchungaji mwema ili waweze kuwa wamoja. Wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii katika huduma zao tofauti, wanapaswa kuzingatia rasilimali muda, kwa kuutumia vyema na kwamba, mambo yatakwenda vyema pia.
Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru wadau wa mawasiliano ya jamii kwa kutoa tafsiri sahihi ya maisha na utume wa Kanisa; kwa kuzingatia na hatimaye kuhabarisha mambo msingi, changamoto na mwaliko kwa vyombo vya mawasiliano ya jamii kujikita katika mchakato wa kuwaunganisha watu kutoka katika tamaduni mbalimbali. Dhamana na jukumu la mawasiliano si tu kuwahabarisha watu, bali kutengeneza tamaduni za kiutu na mazingira ya kidigitali, ili kujenga mazingira ya majadiliano katika ukweli na uwazi na kwamba, jambo hili linapaswa kupewa uzito wa pekee kutokana na maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili unde, AI., kwa kuwajibika barabara na hivyo kufanya mang’amuzi, ili maendeleo haya makubwa yaweze kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni wajibu wa wadau mbalimbali ndani ya jamii. Kipindi hiki cha maadhimisho ya Juma kuu, Kifo cha Baba Mtakatifu Francisko na hatimaye, Uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kimekuwa ni kipindi cha watu kushirikishana mambo mengi, kiasi cha kufunua lile Fumbo na kiu ya upendo na amani, changamoto na mwaliko kwa vyombo vya mawasiliano ya jamii kuondokana na mawasiliano yasiyokuwa na tija; maamuzi mbele, ushabiki na hata na chuki. Jamii haitaji mawasiliano ya sauti na nguvu, bali mawasiliano yenye uwezo wa kusikiliza na kukusanya sauti za wanyonge ambao hawana sauti. Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka waandishi wa habari wajitahidi kuupokonya ulimwengu silaha, kwa kuzingatia mitazamo tofauti ya ulimwengu na hivyo kutenda mintarafu njia inayolingana na utu na heshima ya binadamu. Waandishi wa habari wako mstari wa mbele kuripoti kuhusu vita, kinzani, migogoro na matarajio ya amani; juu ya ukosefu wa haki, mapambano dhidi ya umaskini unaodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na kazi zinazotekelezwa katika kimya kikuu na watu wengi wanaojizatiti kuunda ulimwengu bora zaidi. Ni kutokana na mantiki hii, Papa Leo XIV anawaalika wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kuchagua kwa uangalifu na kwa ujasiri mawasiliano yatakayojenga na kudumisha Injili ya amani duniani.