Baraza la Makardinali Limesoma Alama Za Nyakati: Papa Leo XIV
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Takwimu zinaonesha kwamba, Vatican ina uhusiano wa kidiplomasia na nchi 184 duniani. Mabalozi wakazi wanaoishi mjini Roma kwa sasa ni 89, wengine, ni mabalozi wanaowakilisha nchi zao wakiwa wanatoka nje ya Roma. Kuna Mashirika ya Kimataifa kama vile, Shirikisho la Nchi za Kiarabu pamoja na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR. Tarehe 26 Juni 2018, Vatican na nchi ya San Marino wameridhia kwa pamoja mkataba wa ushirikiano na Kanisa ili kutoa fursa ya kufundisha dini shuleni. Tarehe 23 Agosti 2018 Vatican na Benin zimeridhia mkataba wa ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa na kwamba, kwa sasa Serikali ya Benin inalitambua Kanisa kisheria! Mkutano wa Baraza la Makardinali umewachagulia waamini wa Kanisa Katoliki kiongozi wa maisha ya kiroho, mkomavu katika shughuli za kichungaji, ambaye katika maisha na utume wake amepambana uso kwa uso na umaskini, utafutaji wa utu, heshima na haki msingi za binadamu; upendo pamoja na shauku ya kupata majibu muafaka ya maisha. Mtazamo wa Baba Mtakatifu Leo XIV unawaambata na kuwakumbatia watu wote wa Mungu, ili kuwakirimia amani inayopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Mfufuka. Hii ni amani inayowaambata na kuwakumbatia watu kutoka katika Mataifa na tamaduni mbalimbali kwa kutambua kwamba, Kanisa daima linapenda kujenga ujirani mwema na watu wote wa Mungu.
Baba Mtakatifu Leo XIV anaanza maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kati kati ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” Jubilei ni kipindi cha toba, wongofu wa ndani pamoja na upyaisho wa maisha ya kiroho; ni mwaliko wa kujenga, kudumisha na kutangaza Injili ya amani; umoja na mshikamano, ili kuwawezesha watu wote wa Mungu kuishi katika ukweli, haki na amani. Hii ni sehemu ya utangulizi iliyotolewa na Balozi George Poulides kutoka Cyprus, ambaye ni Dekano wa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican, Ijumaa tarehe 16 Mei 2025 wakati Baba Mtakatifu Leo XIV alipokutana na kuzungumza na Mabalozi hawa kwa mara ya kwanza. Amesema, Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kumkumbuka na kumwombea Hayati Baba Mtakatifu Francisko ambaye ni kiongozi aliyesimama kidete kupambania amani pamoja na changamoto mbalimbali za Jumuiya ya Kimataifa.
Baba Mtakatifu Leo XIV anabeba ndani mwake tasaufi ya Mtakatifu Agostino anayetoa ufunguo wa jinsi ya kutafuta amani, mintarafu diplomasia kwa kujikita katika amani “Ukipenda amani, katika hali yoyote uliyo nayo; wahurumie wale ambao hawapendi kile unachopenda; wahurumie kwa kukosa kile ambacho unacho wewe.” Ni maneno kuntu kutoka kwa Mtakatifu Agostino, mwaliko na changamoto ya watu kuvuka tofauti zao msingi, ili hatimaye kujenga msingi wa majadiliano kati ya watu wa Mataifa, Majadiliano ya kidini na majadiliano kati ya watu wenyewe. Watu wa Mungu wanapaswa kushukuru kwa sayansi ya ugunduzi ambayo inaonesha matunda mengi, lakini pia dunia imeendelea kushuhudia kinzani, migogoro, mipasuko na vita; ukosefu wa usawa unaendelea kupanuka kila kukicha, hali inayoongesha choyo na ubinafsi, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa. Katika hali na mazingira kama haya, uzoefu na mang’amuzi ya Mama Kanisa ni msaada mkubwa sana kwa Jumuiya ya Kimataifa.
Papa Leo XIII aliliongoza Kanisa katika kipindi cha Mapinduzi ya Viwanda yaliyoleta changamoto mbalimbali na kwamba, leo hii, binadamu anakabiliana na changamoto mamboleo za maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano pamoja na ukuaji wa teknolojia ya akili unde. Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanapenda kujizatiti katika ujenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu, ili kupambana na mateso pamoja na mahangaiko yanayoendelea kuwasibu binadamu; tayari kukabiliana na changamoto mamboleo, ili hatimaye, kuweza kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi; kupambana na ukosefu wa usawa kati ya watu; hali mbayo inaendelea kupanuka kila kukicha, tayari kujikita kuwasaidia maskini na wanyonge; watu wasiokuwa na ulinzi pamoja na wale wanaosukumizwa pembeni mwa vipa umbele vya jamii. Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, wanamtakia heri na baraka Baba Mtakatifu Leo XIV katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii iwe ni fursa ya kukuza na kudumisha matumaini pamoja na kujenga umoja na mshikamano wa watu wote wa Mungu.