Baba Mtakatifu Leo XIV:Vipaumbele:Umoja wa Kanisa na Upendo wa Mungu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema kwamba Yesu Kristo, aliye Mchungaji wa milele, alijenga Kanisa takatifu, akawatuma Mitume kama Yeye mwenyewe alivyotumwa na Baba (Rej. Yn 20:21), tena akataka waandamizi wao, yaani Maaskofu, wawe wachungaji wa Kanisa lake hata ukamilifu wa nyakati. Kusudi Uaskofu wenyewe uwe mmoja na usiogawanyika, akamweka Mt. Petro juu ya Mitume wengine, na katika yeye akatia chanzo na msingi udumuo na uonekanao wa umoja wa imani na wa ushirika. Mtaguso Mtakatifu huwatolea tena waamini wote fundisho hilo la uanzishaji, udumifu, nguvu na tabia ya mamlaka tukufu ya Papa na ya Mamlaka fundishi ya Kanisa yasiyoweza kukosa, ili liaminike kwa uthabiti. Tena, katika kuendelea kwa njia hiyohiyo, linaamua kukiri na kutangaza mbele ya wote fundisho juu ya Maaskofu walio waandamizi wa Mitume, ambao pamoja na mwandamizi wa Petro, aliye Wakili wa Kristo na kichwa kionekanacho cha Kanisa zima, waiongoza nyumba ya Mungu aliye hai. Kama vile Mtakatifu Petro na wale Mitume wengine wameunganika, kwa agizo la Bwana, katika urika mmoja tu wa kitume, kwa jinsi iliyo sawa (pari ratione), Baba Mtakatifu aliye mwandamizi wa Petro, na Maaskofu walio waandamizi wa Mitume, wanaungana pamoja. Kuna mambo mawili yaoneshayo tabia na maumbile ya kiurika ya Daraja ya uaskofu: yaani nidhamu ya kale, ambayo kufuatana nayo Maaskofu wa ulimwengu mzima walishirikiana wao kwa wao na pamoja na Askofu wa Roma, katika kifungo cha umoja, upendo na amani.
Urika wa Maaskofu hauwezi kuwa na mamlaka usipounganika na Baba Mtakatifu, aliye mwandamizi wa Petro, naye ndiye kichwa chake, ambaye mamlaka ya ukuu wake hudumu kabisa juu ya wote, wachungaji kwa waamini. Kwa maana Baba Mtakatifu, kwa nguvu ya wadhifa wake kama Wakili wa Kristo na Mchungaji wa Kanisa lote, ana mamlaka katika Kanisa, iliyo kamili, ya juu kabisa na iwahusuyo wote (plenam, supremam et universalem potestatem), ambayo anaweza kuyatimiza kwa uhuru. Urika wa Maaskofu (Ordo Episcoporum) ni urithi wa urika wa Mitume katika kufundisha na katika uongozi wa kichungaji; na ndani yake umoja wa Mitume huendelezwa katika nyakati. [Urika huo wa Maaskofu] pamoja na Kichwa chake aliye Baba Mtakatifu, na kamwe pasipo yeye, una mamlaka ya juu kabisa na kamili juu ya Kanisa lote. [Mamlaka hiyo] yaweza kutekelezwa tu kwa idhini ya Baba Mtakatifu. Bwana alimweka Simoni Petro tu kuwa mwamba na mshika ufunguo wa Kanisa (Rej Mt 16:18-19), akamweka kuwa Mchungaji wa kundi lake zima (Rej Yn 21:15nk); lakini wadhifa wa kufunga na kufungua aliopewa Petro (Rej. Mt 16:19), ulikabidhiwa pia kwa Urika wa Mitume uliounganika na mkuu wake (taz. Mt 18:18; 28:16-20.) Urika huo maadamu umeundwa na wengi, huonyesha hali ya Taifa la Mungu ya kuwa la namna nyingi na la ulimwengu mzima; maadamu ulikusanyika chini ya kiongozi mmoja tu, huonyesha umoja wa kundi la Kristo. Rej. LG 18-22.
Alama za huduma kama Khalifa wa Mtakatifu Petro: Pallio Takatifu na Pete ya Mvuvi: Pallio Takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachovaliwa na Baba Mtakatifu, Maaskofu wakuu wa majimbo ya Kanisa Katoliki pamoja na Mapatriaki. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, Mchungaji mwema, hata kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Maaskofu wakuu na Mapatriaki wanahamasishwa kuwabeba kondoo wao kama kielelezo cha wachungaji wema; wakumbuke kwamba, wameteuliwa si kwa ajili ya mafao yao binafsi, bali kwa ajili ya kondoo wa Kristo Yesu. Papa mpya na Maaskofu wakuu wanapaswa pia kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Pallio takatifu ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, Maaskofu wakuu na Mapatriaki, mshikamano unaopata chimbuko lake katika Fumbo la Umwilisho, linalofikia utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka. Pallio Takatifu imebarikiwa na Kardinali Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Siria. Baba Mtakatifu Leo XIV amevishwa pia “Pete ya Mvuvi”: “Anuli Piscatoris” Pete ambayo inamwakilisha Mtakatifu Petro aliyekuwa ni Mvuvi kutoka Galilaya. Pete hii inatumika kama muhuri binafsi wa Baba Mtakatifu; kielelezo cha imani ya Mtakatifu Petro kwa Kristo Yesu na hivyo kuthibitisha uhalisia wake. Pete ya Mvuvi imebarikiwa na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Sala kutolewa na Kardinali Fridolin Ambongo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri, yake Dominika tarehe 18 Mei 2025 anapouanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 267 na Askofu wa Roma, amegusia kifo cha Papa Francisko; Umoja na Mshikamano wa Baraza la Makardinali pamoja na sala za waamini; Ujenzi wa Kanisa linalosimikwa katika upendo wa Mungu; Kwa kukuza na kudumisha: Umoja na mshikamano wa Kanisa, chachu ya upatanisho, tayari kujikita katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari. Baba Mtakatifu Leo XIV ametambua uwepo wa umati mkubwa wa watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia waliofika kushuhudia anapouanza utume wake rasmi kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa kifo cha Papa Francisko, waamini waligubikwa na huzuni na majonzi makubwa, wakawa kama kondoo wasio na mchungaji. Rej. Mt 9:36. Waamini wakajikita zaidi katika imani kwa Kristo Mfufuka kwa kutambua kwamba, kamwe Kristo hawezi kuwaacha kondoo wake wapotee, atawakusanya, na kuwalinda, kama mchungaji alindavyo kundi lake.Rej. Yer 31:10. Ni katika roho ya Pasaka, Baraza la Makardinali lilikutanika kufanya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu, Askofu wa Roma, Mchungaji mwenye uwezo wa kulinda na kudumisha amana na utajiri wa imani ya Kikristo, akiwa na mwelekeo mpana zaidi, ili kuweza kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa mbalimbali katika ulimwengu mamboleo. Makardinali wakasindikizwa na Sala za waamini, wakashirikiana na kushikamana na matokeo yake wamempata Papa Leo XIV anayekuja mbele ya Kanisa kama ndugu anayetaka kujisadaka katika huduma ya imani, ili aweze kuwa kweli ni chemchemi ya furaha, huku wakitembea kwa pamoja katika njia ya upendo wa Mungu, anayetaka watu wote wawe wamoja kama familia moja.
Kristo Yesu baada ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, alimkabidhi Mtakatifu Petro dhamana ya kuendeleza utume wa upendo na umoja, baada ya kumchagua na kumwimarisha kama mvuvi wa watu, sasa anaitwa na kutumwa kushusha nyavu za matumaini ya Injili, huku akiendelea kuogelea katika bahari ya maisha ya watu wa Mungu, ili wote, hatimaye, waweze kukumbatiwa na Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Petro angeweza kutekeleza dhamana na utume huu kwa kuonja na kuguswa na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka mintarafu nguvu na udhaifu wake wa kibinadamu. Huu ni upendo wa Kimungu, yaani “Agape” unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tofauti kabisa na ule upendo aliouonesha kwanza Mtakatifu Petro alipokuwa akimjibu Kristo Yesu, kwani kwake upendo huo ulikuwa ni kielelezo cha urafiki kati yao. Lakini Kristo Yesu alikita swali lake katika upendo wa Kimungu “Agape”, tayari kujikita katika kuwachunga kondoo wa Kristo Yesu. Upendo wa Kimungu unamsukuma Mtakatifu Petro kuwapenda zaidi ndugu zake, tayari hata kusadaka maisha yake. Kumbe, Mtakatifu Petro amepewa dhamana ya kupenda zaidi kuliko Mitume wengine wote. Amepewa dhamana ya kuwaongoza watu wa Mungu katika imani, kwa kutembea pamoja, kwani kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo hata waamini wamekuwa ni mawe hai, hivyo wanaitwa na kutumwa kujenga Nyumba ya Mungu katika udugu wa kibinadamu, amani na utulivu katika Roho Mtakatifu, huku wakizingatia tofauti zao msingi zinazojenga umoja na upendo kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, ana kiu ya ujenzi wa Kanisa moja, alama ya umoja na ushirika, unaogeuka na kuwa ni chachu ya upatanisho ulimwenguni. Inasikitisha kuona kwamba, Ulimwengu mamboleo umegubikwa na mipasuko ya kijamii, madonda makubwa kutokana na chuki na uhasama, ghasia, maamuzi mbele na woga wa jirani; uchumi tenge unaonyona rasilimali za dunia kwa kuwaacha maskini wakiendelea kutumbukia katika umaskini.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, anataka kuwa ni chachu itakayochachua umoja, ushirika na udugu wa kibinadamu, kwa kumwangalia na kumkaribia Kristo Yesu. Kwa hakika Neno la Mungu linaangaza na kufajiri, mwaliko kwa waamini kufuata na kumwilisha ushauri wake wa upendo, ili kujenga familia kubwa ya binadamu na kuendelea kuragibisha majadiliano ya kiekumene na waamini wa Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo; Majadiliano ya kidini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema ili kwa pamoja wote waweze kujikita katika ujenzi wa Ulimwengu mpya ambamo amani inatawala. Hii ndiyo roho ya kimisionari inayokita mizizi yake katika upendo wa Mungu, ili kweli umoja wa watu wa Mungu kutoka katika jamii na dini mbalimbali uweze kufikiwa. Huu ni wakati wa kumwilisha Injili ya upendo kutoka kwa Mungu unaowafanya wote kuwa ni ndugu wamoja na hivyo kuishi katika amani. Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha mahubiri yake kwa kuwaalika watu wote wa Mungu kwa mwanga na nguvu ya Roho Mtakatifu, kujikita katika ujenzi wa Kanisa linalosimikwa katika upendo wa Mungu, kama alama ya umoja, Kanisa la Kimisionari, linalofungua malango yake na kuukumbatia ulimwengu; Kanisa linalotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na hivyo kugeuka kuwa ni chachu ya amani kwa ajili ya binadamu; watu wote wa Mungu kama ndugu wamoja, watembee kumwendea Mwenyezi Mungu huku wakipendana wao kwa wao.
Kabla ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Leo XIV alizungukia viunga vyote vya mji wa Vatican, ili kusalimiana na umati mkubwa wa watu waliofika kushuhudia tukio hili la kihistoria. Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na wawakilishi wa Jumuiya ya Wayahudi, Waislam, Wahindu, Wabuddha, Wazoroastriani pamoja na Wagianisti. Kumekuwepo na uwakilishi mkubwa wa Makanisa ya Kiorthodox pamoja na Jumuiya za Kikristo; Viongozi wa Serikali, Falme mbalimbali pamoja na Mabalozi.