Baba Mtakatifu Leo XIV: Umuhimu wa Michezo Katika Maisha
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa anatambua na kuthamini michezo kuwa ni nyenzo muhimu sana katika kusimamia haki msingi za binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Michezo ni muhimu sana katika ujenzi wa jamii na ushiriki mkamilifu katika kudumisha: haki, amani na utulivu bila vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya kwa njia ya michezo, umuhimu wa kujikita katika urafiki, udugu na haki, mambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo. Hayati Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni katika uzinduzi wa Waraka wa “Dare il meglio di se”, yaani “Kujitoa Kikamilifu”: Mtazamo wa Kikristo kuhusu michezo na binadamu” uliochapishwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, michezo ni mahali pa kuwakutanisha watu katika ngazi mbalimbali, ili kufikia lengo maalum. Michezo ni kiungo maalum cha majiundo na tunu msingi za maisha ya kiutu. Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha: ukarimu, unyenyekevu, sadaka, udumifu, furaha, kila mtu akijitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake, kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na mshikamano unaobomolea mbali tabia ya ubinafsi na uchoyo.
Hayati Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Michezo katika nafasi mbalimbali ni jukwaa la kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa walimwengu. Ni wakati wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Yesu Mfufuka wanapokuwa uwanjani. Hata wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao kila kukicha!
Michezo inapania kujenga na kuimarisha urafiki na udugu kati ya watu; maelewano na amani; kuheshimiana, maridhiano na utulivu kwa kuthamini tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Tunu msingi za michezo zinapaswa kusisitizwa miongoni mwa vijana na watoto, ili kuwasaidia kutambua kwamba, kila fursa iliyopo inaweza kutumika kwa ajili ya maboresho ya maisha ya mtu: kiroho na kimwili. Kufaulu na kushindwa katika masuala ya michezo ni ukweli usioweza kupingika. Hii iwe ni fursa ya kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu; kwa kuzingatia na kuheshimu sheria, kanuni, maadili na utu wema; mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya michezo.
Ni katika muktadha wa umuhimu wa michezo, katika maisha ya watu, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumanne, tarehe 27 Mei 2025 amekutana na kuzungumza na Klabu ya Soka ya Napoli “Società Sportiva Calcio Napoli” iliyoibuka kidedea katika mashindano ya Soka nchini Italia kwa mwaka 2025. Ushindi huu ni matokeo ya safari ndefu ya umoja, ushirikiano na mshikamano kama timu inayoundwa na wachezaji, kocha pamoja na klabu nzima. Mshikamano huu ni muhimu kwa timu na jamii katika ujumla wake na kwamba, mchezo wa soka una umaarufu sana nchini Italia na Ulimwengu katika ujumla wake. Kumbe, kuna umuhimu wa kuhakikisha kwamba, wanasoka wanaweka karama na mapaji yao kwa ajili ya huduma ya pamoja. Michezo haina budi pia kutumika kama nyenzo ya kurithisha elimu na tunu msingi za maisha ya kijamii! Lakini pale soka inapogeuzwa kufanywa kuwa biashara, kuna hatari ya kupoteza tunu zake. Kumbe, kuna haja kwa wadau wa michezo kuhakikisha kwamba, wanajizatiti katika kulinda na kudumisha: kanuni maadili, utu wema pamoja tunu msingi za michezo, changamoto hii inapaswa kuvaliwa njuga na wazazi pamoja na walezi. Vijana wapewe malezi na majiundo makini ya kimaadili na utu wema.