Papa Leo XIV Maadhimisho ya Siku ya Afrika Kwa Mwaka 2025: Mashuhuda wa Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Umoja wa Afrika tarehe 25 Mei 2025 umeadhimisha kumbukizi ya Miaka 62 tangu kuasisiwa kwake kama Umoja wa Nchi Huru za Afrika, OAU na ambayo baadaye iligeuzwa na kujulikana kama Umoja wa Afrika. Hili ndilo chimbuko la Siku ya Afrika, ishara ya umoja, maendeleo na juhudi za kuleta uhuru na ukombozi wa kweli Barani Afrika. Ilikuwa ni Mwezi Mei 1963, wakuu 32 wa nchi huru za Kiafrika walipokutana mjini Addis Ababa, Ethiopia kusaini mkataba wa kuanzisha kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika. Lengo likiwa ni kukoleza mapambano dhidi ya ukoloni, ili kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kuthamini amana na utajiri wa tamaduni za Kiafrika. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu Barani Afrika kuwa na ari na mwamko wa kutangaza na kushuhudia uzuri na ukarimu wa watu wa Bara la Afrika, katika huduma, ukweli na uwazi; kwa kuwa na ujasiri, msamaha pamoja na kuendeleza mapambano dhidi ya ukosefu wa haki kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; bila kusahau kuwa na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, tayari kujenga na kudumisha urafiki na mafungamano ya kijamii.
Tarehe 9 Septemba, 1999 Wakuu wa Nchi na Serikali wa OAU walipitisha Azimio la Sirte huko Sirte nchini Libya. Umoja wa Afrika ukazinduliwa rasmi Julai 2002 huko Durban, Afrika Kusini. Maadhimisho ya miaka 62 ya Umoja wa Afrika kwa Mwaka 2025 yamenogeshwa na kauli mbiu “Wacha Tuwe Wabunifu wa Afrika Tunayoitaka.” Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii kwa lugha ya Kiswahili anasema, “Bara la Afrika linatoa ushuhuda mkubwa kwa ulimwengu mzima. Asante kwa kuishi imani yenu katika Yesu Kristo. Ni jinsi gani ilivyo muhimu kwamba kila mbatizwa ajisikie kuitwa na Mungu kuwa ishara ya matumaini katika Ulimwengu mamboleo.” Huu ni ujumbe ambao kwa mara ya kwanza unatolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV kwa lugha ya Kiswahili, wakati huu, Umoja wa Afrika unapoadhimisha Kumbukizi ya miaka 62 tangu kuanzishwa kwake.
Jumatatu tarehe 26 Mei 2025 Kardinali Francis Arinze akishirikiana na Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson pamoja na Askofu mkuu Fortunatus Nwachukwu, ameongoza Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya Mabalozi wanaowakilisha nchi zao mjini Vaticana na Italia katika ujumla wake. Ibada hii ya Misa Takatifu imeongozwa na kauli mbiu: “L’Esperance de la paix en Afrique” Yaani “Tumaini la Amani Barani Afrika.” Hii ni siku ambayo pia Mabalozi hawa wameitumia kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 62 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika sanjari na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo inanogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Ni katika muktadha wa maadhimisho ya kumbukizi ya Miaka 62 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika sanjari na Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Baba Mtakatifu Leo XIV mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu huku akiwa ameandamana na Kardinali Francis Arinze anayeadhimisha kumbukumbu ya Miaka 40 tangu alipoteuliwa kuwa Kardinali, hapo tarehe 25 Mei 1985 aliwasalimia Mabalozi na waamini waliohudhuria Ibada hii ya Misa Takatifu, huku akitumia fursa hii, kuwakaribisha mjini Roma na Vatican katika ujumla wake, huku akiwataka waendelee kuwa ni mashuhuda na vyombo vya matumaini na kwamba, kila Mkristo anapaswa kujisikia kuitwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni alama ya matumaini katika Ulimwengu mamboleo.
Imani ni chemchemi ya nguvu inayowawezesha kuuona mwanga wa Kristo Yesu katika maisha yao na hivyo kugundua umuhimu kwa waamini kuiishi kikamilifu imani yao, si tu wakati wa Dominika na Hija za maisha ya kiroho, lakini imani inapaswa kumwilishwa katika kila siku ya maisha na hivyo kujazwa na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu; matumaini yanayowawezesha kutembea kama ndugu wamoja, huku wakiendelea kumtukuza Mwenyezi Mungu na kwamba, yale yote waliyo nayo ni zawadi kutoka kwa Mungu na kwamba, zawadi hizi zinapaswa kutumiwa kwa ajili ya huduma, ustawi na maendeleo ya jirani zao. Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru Mabalozi kwa kuendelea kuiishi imani yao kwa Kristo Yesu. Aliwataja Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Kardinali Francis Arinze pamoja na Askofu mkuu Fortunatus Nwachukwu, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, wote hawa ni mashuhuda wa imani kutoka Barani Afrika. Kwa hakika, huu ni wakati wa kumshukuru na kumtukuza Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha mkutano wake na Mabalozi kutoka Afrika kwa kuwapatia baraka zake za kitume.
Wakati huo huo, Kardinali Fridolin Ambongo Besungu, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, kama sehemu ya Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 62 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika, AU, amegusia changamoto na dharura zinazoendelea kulikabili Bara la Afrika ikiwa ni pamoja: Ukosefu wa haki, vitendo vya kigaidi, kinzani na migogoro ambayo imewalazimu mamilioni ya watu kuyakimbia makazi na nchi za ona hivyo kujikuta wakiwa ni wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum hata katika nchi zao. Kuna umaskini mkubwa wa hali na kipato; changamoto za elimu, afya, ustawi, maendeleo; majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali; changamoto za ikolojia, biashara haramu ya binadamu pamoja na mifumo ya utumwa mamboleo.
Kardinali Fridolin Ambongo Besungu, ana matumaini makubwa kwamba, viongozi Barani Afrika watasikiliza wito na ushauri kutoka kwa Baba Mtakatifu Leo XIV, huku wakifuata nyayo za Mtangulizi wake, Papa Francisko kwa kuimarisha dhamira ya Kanisa kuendelea kujikita katika haki, amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu; huku upendeleo wa pekee ukitolewa kwa ajili ya maskini. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu Barani Afrika kuwa ni wasanifu na wajenzi wa Afrika wanayoitaka; Afrika bora yenye furaha na matumaini. Kumbe, ni jukumu la dini na madhehebu mbalimbali kukuza na kudumisha haki, amani na maridhiano, kwa kuendelea kupambana na ukosefu wa haki msingi za binadamu; Ubaguzi, Unyonyaji na Ukwapuaji wa madini na raslimali kutoka Barani Afrika; mifumo mbalimbali ya unyanyasaji. SECAM inawaalika watu wa Mungu Barani Afrika kuwa ni mahujaji wa matumaini na hivyo wajikite katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Watu wa Mungu Barani Afrika wajenge madaraja ya amani na matumaini ndani na nje ya Bara la Afrika.