Baba Mtakatifu Leo XIV: Kipaumbele Cha Kwanza Mafundisho Jamii
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha adili ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo, zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.
Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Papa Leo XIII; Mambo Mapya; “Rerum novarum.” Alisema, kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, ina thamani na heshima yake ya asili. Aligusia haki msingi za wafanyakazi, mshahara wa haki na wajibu wa wafanyakazi; Umiliki wa binafsi wa mali; wajibu wa Serikali ni pamoja na kuhakikisha haki, sanjari na kuwalinda wanyonge ndani ya jamii; Ustawi na maendeleo ni kwa ajili ya wote, lakini maskini wapewe kipaumbele cha kwanza. Kanuni ya auni inapaswa kuzingatiwa! Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, katika Waraka wake kuhusu Masuala ya Kijamii “Centesimus Annus,” alifafanua kwa kina kuhusu asili ya haki msingi za binadamu; umuhimu wa kukuza na kudumisha upendo na mshikamano miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa, kama inavyojidhihirisha katika Waraka wake wa “Sollicitudo Rei Socialis” cheche ya uanzishaji wa vyama vya kitume kijamii vilivyokuwa vinapania kulinda na kutetea uhuru, utu na haki msingi za binadamu. Itakumbukwa kwamba, uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu ni muhtasari wa haki zote za binadamu. Dini zisaidie kujenga amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na kamwe zisiwe ni chanzo cha vurugu, kinzani na vita. Kanuni maadili na utu wema ni sehemu muhimu sana katika maisha ya mwanadamu zinazopaswa kulindwa ili amani na utulivu viweze kushika kasi, bila kusahau nafasi na dhamana ya uwepo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Waamini wanapaswa kufahamu vyema kweli za imani yao ili wasiyumbishwe, bali wasimame kidete kuilinda, kuitetea na kuishuhudia kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi.
Baba Mtakatifu Leo XIV (69) ambaye anaongozwa na kauli mbiu yake ya Kiaskofu “In Illo unum uno” Yaani “Ingawa sisi Wakristo ni wengi, katika Kristo mmoja sisi ni wamoja.” Huu ni ufafanuzi uliotolewa na Mtakatifu Agostino mintarafu Zaburi ya 127. Papa Leo XIV ni Mtawa wa kwanza wa Shirika la Waagostiniani kuchaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na Mmarekani wa pili kuwahi kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro baada ya Hayati Papa Francisko. Katika salam zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, “Urbi et Orbi”, Alhamisi tarehe 8 Mei 2025 alikazia pamoja na mambo mengine: Umuhimu wa ujenzi wa amani inayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka; Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na upendo kwa waja wake wote na kwamba, kamwe ubaya hauwezi kushinda. Kuna haja ya kuwa vyombo na wajenzi wa haki na amani; waaminifu kwa Kristo Yesu, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo, huku wakijitahidi kuwa ni wamisionari. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kati ya waamini yeye ni Mkristo na kwao yeye ni Askofu. Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajenga Kanisa la: Kisinodi na kimisionari, kwa kujikita katika Injili ya upendo hasa kwa maskini na wahitaji sanjari na majadiliano, ili kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu.
Baba Mtakatifu Leo XIV, katika mahubiri yake, Ijumaa tarehe 9 Mei 2025, kwenye Ibada ya Misa Takatifu na Makardinali walioshiriki katika uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro amekazia umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa; Ukulu wa Mtakatifu Petro katika kumkiri na kumtangaza Kristo Yesu na kamwe wasimezwe na: maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia; uchu wa mali, madaraka na raha za dunia hii, bali waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili; faraja kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu; tayari kuganga na kutibu changamoto na kinzani za maisha ya ndoa na familia pamoja na ukanimungu na kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu na chombo cha umoja. Baba Mtakatifu Leo XIV anauanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kielelezo cha upendo, sadaka na majitoleo kwa wale wote waliopewa dhamana ya kuliongoza Kanisa la Kristo Yesu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Inyasi wa Antiokia, ili watu wengi zaidi wapate fursa ya kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Mungu.