ĐÓMAPµĽş˝

Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuweka wakfu Krisma ya Wokovu, ni ufunuo wa Kanisa, Fumbo la Mwili wa Kristo unaofumbatwa katika huduma, karama na neema mbalimbali za Roho Mtakatifu. Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuweka wakfu Krisma ya Wokovu, ni ufunuo wa Kanisa, Fumbo la Mwili wa Kristo unaofumbatwa katika huduma, karama na neema mbalimbali za Roho Mtakatifu.  (Vatican Media)

Umuhimu wa Mafuta Matakatifu Katika Maisha na Utume wa Kanisa

Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuweka wakfu Krisma ya Wokovu, ni ufunuo wa Kanisa, Fumbo la Mwili wa Kristo unaofumbatwa katika huduma, karama na neema mbalimbali za Roho Mtakatifu katika hija ya maisha yake kumwendea Kristo Yesu. Ni mafuta yanayowaweka wakfu Wakristo, ili kushiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu. Ibada hii ya Misa Takatifu inalionesha Kanisa kuwa ni Sakramenti ya Wokovu, inayotakasa. Umuhimu wa Mafuta Matakatifu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mafuta ni alama ya ushirika, furaha, upendo na mshikamano. Ni alama ya imani inayoimarisha vifungo vya upendo kwa njia ya Roho Mtakatifu ili kutangaza na kushuhudia: Ukuu, uzuri na utakatifu wa familia ya Mungu. Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, kamwe hawatindikiwi na mafuta ya neema ya imani, matumaini na mapendo. Huu ni mwaliko wa kuboresha maisha ya kiroho kwa kujikita katika: Sala, Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Matendo adili na matakatifu na kwamba, Msalaba uwe ni kimbilio na ngao ya maisha ya mwamini. Kardinali Domenico Calcagno, Rais mstaafu wa Utawala wa Amana ya Kiti cha Kitume kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa Alhamisi kuu tarehe 17 Aprili 2025 kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuweka wakfu Mafuta ya Krisma ya Wokovu, “Sacrum Chrisma.” Ibada hii itaadhimshwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 3:30 Asubuhi kwa saa za Ulaya, sawa na Saa 4:30 kwa Saa za Afrika Mashariki. Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuweka wakfu Krisma ya Wokovu, ni ufunuo wa Kanisa, Fumbo la Mwili wa Kristo unaofumbatwa katika huduma, karama na neema mbalimbali za Roho Mtakatifu katika hija ya maisha yake kumwendea Kristo Yesu. Ni mafuta yanayowaweka wakfu Wakristo, ili hatimaye, kushiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu. Ibada hii ya Misa Takatifu inalionesha Kanisa kuwa ni Sakramenti ya Wokovu, inayotakasa. Baba Mtakatifu atabariki Mafuta ya Wakatekumeni na Mafuta ya Wagonjwa pamoja kuweka wakfu Mafuta ya Krisma ya Wokovu; mafuta yanayotumika kwa ajili ya kuwapaka waamini wakati wanapopokea Sakramenti ya Ubatizo, Sakramenti ya Kipaimara na wanapowekwa wakfu kuwa Mapadre na Maaskofu.

Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma
Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma   (Vatican Media)

Kwa vile Mapadre ni waadhimishaji na wagawaji wa Mafumbo ya Kanisa, wanapaswa kujitakatifuza katika maisha yao, kwa kuambatana na Mungu kwa njia ya Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti. Haya ni mafuta yanayotumika pia kutabaruku Kanisa kwa kupaka Altare na kuta za Kanisa kuonesha kwamba, Jengo hili, yaani Kanisa limetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya mambo matakatifu ya Mungu. Mafuta haya ni ishara ya uwepo wa Roho Mtakatifu. Haya ni mafuta yaliyotiwa manukato na kuwekwa wakfu na Askofu mahalia, huashiria paji la Roho Mtakatifu kwa mbatizwa mpya. Amekuwa Mkristo, yaani “Mpakwa” na Roho Mtakatifu, ameingizwa katika Kristo Yesu, ambaye amepakwa mafuta kama: Kuhani, Nabii na Mfalme. Hii ni siku ambayo Mama Kanisa anabariki pia Mafuta ya Wagonjwa: “Oleum infirmorum.” Yanayotumika katika Sakramenti ya Mpako wa wagonjwa: Mafuta haya hutolewa kwa wagonjwa walio katika hatari kubwa, kwa kuwapaka mafuta usoni na mikononi; mafuta yaliyobarikiwa itakiwavyo, yaliyokamuliwa kutoka katika matunda ya Mizeituni kwa kusema mara moja tu: “Kwa Mpako huu Mtakatifu na kwa pendo lake kuu, Bwana akujaze kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Akuondoe katika enzi ya dhambi, akuweke huru. Kwa wema wake akupe nafuu katika mateso yako na kukujalia neema.” Ni mafuta yanayoweza kuleta: faraja, msamaha wa dhambi na uponyaji kadiri ya mapenzi ya Mungu pamoja na kumwondolea dhambi mgonjwa ambaye hawezi kuungama. Mafuta ya Wakatekumeni: “Oleum Catechumenorum” ni ishara ya nguvu ya Kristo Yesu kwa waamini wanaojiandaa kupokea Sakramenti ya Ubatizo, ili waweze kupata uwezo wa kupambana na vishawishi pamoja na dhambi. Ni mafuta yanayowaandaa Wakatekumeni kupambana dhhidi ya uovu na hivyo kuwakirimia waamini neema ya awali kabla ya kupokea Sakramenti ya Ubatizo.

Mafuta Matakatifu ni Muhimu Sana katika maisha na utume wa Kanisa
Mafuta Matakatifu ni Muhimu Sana katika maisha na utume wa Kanisa   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mama Kanisa anafundisha kwamba, Kristo Yesu aliwapenda watu wake upeo na alipokuwa anakaribia “Saa yake” ili kutoka hapa ulimwenguni na kurudi kwa Baba yake wa mbinguni, Siku ile ya Alhamisi kuu, walipokuwa wakila, aliwaosha Mitume wake miguu yao na kuwapatia Amri ya upendo inayomwilishwa katika huduma ya upendo, hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Akataka pia kuwapatia amana ya upendo huu na kuendelea kubaki kati yao na kuendelea kuwashirikisha Fumbo la Pasaka, aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, kielelezo cha sadaka, shukrani, kumbukumbu endelevu na uwepo wake kati yao katika alama ya Mkate na Divai! Alhamisi kuu ni Siku ambayo Mama Kanisa anakumbuka siku ile Kristo Yesu alipoweka Sakramenti ya Daraja Takatifu ya Upadre inayopata utimilifu wake katika Daraja ya Uaskofu. Hii ni siku ambayo Kristo Yesu aliwaweka Mitume wake, wawe wafuasi wake wa karibu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kumbe, hii ni siku ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Daraja Takatifu ya Upadre na kuwashukuru Mapadre kwa sadaka na majitoleo yao licha ya dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu. Huu ni mwaliko kwa Mapadre kuishi mintarafu Daraja Takatifu ya Upadre, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume wa Kipadre, wakitambua kwamba, kwa njia ya Daraja Takatifu ya Upadre wanashirikishwa maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Mapadre wanapaswa kusimama kidete ili kuweza kuishi fadhila za maisha na utume wa Kipadre, kwa kujitahidi kuishi kama Kristo mwingine “Alter Christus” ili kwamba, waamini waweze kumtambua Kristo Yesu ndani mwao. Hii pia ni Siku ambayo Mapadre wanarudia tena ahadi pamoja na viapo vyao, jambo wanalopaswa kulifanya kutoka katika sakafu ya nyoyo zao, ili kuendelea kuimarisha urika wao pamoja na Maaskofu wao.

Krisma ya Wokovu inawekwa wakfu
Krisma ya Wokovu inawekwa wakfu   (Vatican Media)

Naye Angela Kibwana, kutoka Jimbo Katoliki la Morogoro anasema, Askofu Lazarus Vitalis Msimbe SDS, katika Ibada ya Misa Takatifu ya kuweka wakfu Krisma ya Wokovu na Kubariki Mafuta Matakatifu, amewataka Mapadre kuyaheshimu Mafuta haya matakatifu na yatumike kadiri ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa na kamwe yasitumike kuwa ni kichocheo cha biashara. Watangaze na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; wawafundishe watu wa Mungu kwa ari na moyo mkuu, huku wakiendelea kuwatakatifuza na kuwaweka huru. Waamini waadhimishe mafumbo ya Kanisa kwa uchaji, ibada na utii. Amewapongeza Mapadre kwa kuendelea kuwahudumia watu wa Mungu licha ya changamoto wanazokabiliana nazo. Amewashukuru na kuwapongeza waamini kwa kulitegemeza Jimbo pamoja na kuwahudumia vyema Mapadre wao. Wakristo wanapaswa kuwa macho na watu wanaogawa au kupaka watu mafuta, kwani wanawadanganya na kutaka kuwanyonya. Hii ni changamoto kwa Mapadre kuzingatia Ukuhani walioshirikishwa na Kristo Yesu. Wajipange kufundisha mafundisho sahihi ya imani, katekesi makini na kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika maisha na wito wao wa Kipadre, ili kweli waweze kuwa ni mfano bora wa kuigwa na waamini wao, ili hatimaye, waamini hao waweze kumfahamu, kumpenda na kumfuasa Kristo Yesu, tayari kumshuhudia kwa dhati kabisa. Baraka itolewe kwa msingi na uelewa wa mafundisho ya Kanisa Katoliki. Sakramenti za Kanisa ziadhimishwe kwa ibada na uchaji, ili kuzuia kufuru dhidi ya Sakramenti hasa ya Ekaristi Takatifu. Mapadre wasimame kidete kutoa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu pale inapostahili na kutumika kama inavyopaswa kadiri ya mafundisho ya Kanisa Katoliki. Mapadre washikamane na Kristo Yesu, kiasi kwamba, waamini waweze kumtambua Kristo Yesu ndani mwao.

Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma
Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma   (Vatican Media)

Alhamisi kuu ni siku ambayo pia Mapadre wanarudia ahadi, maagano na viapo vyao vya Kikuhani, changamoto ni kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuishi kadiri ya maagano haya, ili kweli waweze kuwa ni baraka katika Kanisa la Mungu.Mapadre wanapaswa kufanya mabadiliko chanya katika maadhimisho ya mafumbo ya Kanisa, kwa kuhakikisha kwamba, Ibada ya Misa Takatifu inaadhimishwa kwa Ibada, uchaji na imani zaidi ili kupyaisha imani, kujenga na kudumisha moyo wa sala na ibada. Mapadre wajitahidi kuhubiri kwa viwango, waelimishane, waalikane na watambue kwamba, wanaunganishwa na kushikamanishwa na Sakramenti ya Daraja Takatifu ya Upadre. Kumbe, Mapadre wanapaswa kupendana, kushikamana na kutembeleana. Mapadre waoneshe mabadiliko chanya katika kuchapa kazi kwa kuhakikisha kwamba, wanatoa huduma makini kwa watu wa Mungu. Mapadre wayafahamu maeneo yao ya utume na wayahudumie kwa ari, moyo mkuu na upendo. Wawe ni waaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, huku wakijitahhidi kuipyaisha ile kauli mbiu ya Mwaka wa Mapadre: Uaminifu wa Kristo, Uaminifu wa Padre. Hii iwe ni dira na mwongozo wa maisha na utume wao kama Mapadre. Wajitahidi kuinjilisha kwa njia ya ujenzi wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo.

Mafuta Matakatifu
15 Aprili 2025, 15:06