MAP

2025.04.21 PAPA FRANCESCO AMETUTOKA 2025.04.21 PAPA FRANCESCO AMETUTOKA  Tahariri

Papa wa huruma

Papa ametutoka ghafla asubuhi ya leo,baada ya kutoa baraka zake za mwisho za Urbi et Obi Siku ya Pasaka kutokea 'Loggia'ya kati ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro,baada ya kufanya mzunguko wake wa mwisho kati ya umati,kubariki na kusalimiana.

Andrea Tornielli

"Huruma ya Mungu ni ukombozi wetu na furaha yetu. Tunaishi kwa huruma na hatuwezi kuruhusu kuishi bila huruma: ni hewa tunayopumua. Sisi ni maskini sana kuweza kuweka masharti, tunahitaji kusamehe, kwa sababu tunahitaji kusamehewa." Ikiwa kuna ujumbe mmoja ambao zaidi ya mwingine wowote umeonesha upapa wa Fransisko na ambao umekusudiwa kubaki, ni ule wa huruma. Papa ametutoka ghafla asubuhi ya leo, baada ya kutoa baraka zake za mwisho za Urbi et Obi (Roma na Ulimwenguni) katika Siku ya Pasaka kwa kutokea katikati ya balkoni ya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na baada ya kufanya mzunguko wake  mwisho kati ya umati, kubariki na kusalimiana. Papa wa kwanza wa Argentina katika historia ya Kanisa alishughulikia maswala mengi, hasa umakini kwa maskini, udugu, utunzaji wa nyumba yetu ya kawaida ya pamoja, na kukataa kabisa masharti ya vita. Lakini moyo wa ujumbe wake, ambao kwa hakika umefanya matokeo makubwa zaidi, ni wito wa kiinjili wa huruma. Kwa ule ukaribu na huruma ya Mungu kwa wale wanaojitambua kuwa wanahitaji msaada wake. Huruma  kama "hewa tunayopumua", yaani, kile tunachohitaji zaidi, bila ambayo haiwezekani kuishi. Upapa mzima wa Jorge Mario Bergoglio uliishi chini ya bendera ya ujumbe huu, ambao ni moyo wa Ukristo.

Tangu Sala ya Malaika ya kwanza ya mnamo tarehe 17 Machi  2013 kutoka katika dirisha la nyumba ya Kipapa ambayo hangeweza kukaa kamwe, na ambapo Papa Francisko amezungumza juu ya ukuu wa huruma, akikumbuka maneno ambayo aliambiwa na bibi mmoja mzee ambaye alikuja kuungama wakati alikuwa askofu msaidizi wa Buenos Aires kwamba: "Kama Bwana angekuwapo angesamehe kila kitu ... " Papa ambaye alikuja “kutoka mwisho wa dunia” hakuleta mabadiliko kwa mafundisho ya mapokeo ya Kikristo ya miaka elfu mbili, lakini kwa kurudisha huruma katikati ya mafundisho yake kwa njia mpya, alibadili mtazamo ambao wengi walikuwa nao kuhusu Kanisa. Alitoa ushuhuda kwa uso wa kina mama wa Kanisa ambalo linainama juu ya wale waliojeruhiwa, hasa wale waliojeruhiwa na dhambi. Kanisa linalochukua hatua ya kwanza kuelekea mwenye dhambi, kama Yesu alivyofanya huko Yeriko, ajikaribisha kwenye nyumba ya mtu asiyeonekana na anayechukiwa Zakayo, bila kumwomba chochote, bila masharti. Na ni kwa sababu alihisi kutazamwa na kupendwa namna hiyo kwa mara ya kwanza ndipo Zakayo alijitambua kuwa ni mwenye dhambi, akipata kwenye  mtazamo huo wa Mnazareti msukumo wa kuongoka. Watu wengi, miaka elfu mbili iliyopita, walishikwa na kashfa walipomwona Mwalimu akiingia katika nyumba ya mtoza ushuru wa Yeriko. Watu wengi wamekashifiwa katika miaka ya hivi karibuni kwa ishara za kukaribishwa na ukaribu wa Papa wa Argentina kwa kila aina ya watu, hasa "wasioonekana" na wenye dhambi.

Katika mahubiri yake ya kwanza katika misa na watu, katika kanisa la Mtakatifu  Anna mjini  Vatican Papa Francisko alisema: “Ni wangapi kati yetu labda tunastahili hukumu! Lakini Yeye husamehe! Kwa namna gani? Kwa huruma ambayo haifuti dhambi: msamaha wa Mungu pekee ndio unaoifuta, wakati huruma inapita zaidi. Ni kama anga: tunatazama anga, nyota nyingi sana, lakini jua linapokuja asubuhi na mwanga mwingi, nyota haziwezi kuonekana. Hivi ndivyo huruma ya Mungu ilivyo: nuru kuu ya upendo, ya huruma, kwa sababu Mungu hasamehi kwa amri, bali kwa kubembeleza." Kwa muda wote wa miaka ya upapa wake, mrithi wa 266 wa Petro ameonyesha uso wa Kanisa la karibu, lenye uwezo wa kushuhudia huruma na upole, kuwakaribisha na kukumbatia kila mtu, hata kwa gharama ya kuwa hatari na bila wasiwasi juu ya athari za mawazo sahihi.

"Ninapendelea Kanisa ambalo limejeruhiwa, kujeruhiwa na uchafu kwa sababu limekuwa nje mitaani," Papa Francisko aliandika katika Waraka wa "Evangelii Gaudium," ambao ulikuwa ramani ya njia ya upapa wake, "badala ya Kanisa ambalo ni mgonjwa kwa kufungwa na faraja ya kushikamana na uhakika wake." Kanisa lisilotumainia uwezo wa kibinadamu, katika ushawishi wa washawishi wanaojirejea wao wenyewe tu na katika mikakati ya uuzaji wa kidini, lakini linajiweka wazi ili kujulisha uso wa huruma wa Yeye aliyelianzisha na kulifanya kuwa hai, licha ya yote, kwa miaka elfu mbili. Ni uso huo na mkumbatio huo ambao wengi wameutambua ndani ya Askofu mzee wa Roma aliyetoka Argentina, aliyeanza kazi yake ya Upapa kwa kwenda kuwaombea wahamiaji waliokufa baharini huko Lampedusa, na kuhitimisha kwa kukaa katika kiti cha magurudumu, akitumia hadi dakika ya mwisho kushuhudia kwa ulimwengu kumbatio la huruma la Mungu aliye karibu na waaminifu kwa upendo.

Tahariri ya Kifo cha Papa
21 Aprili 2025, 12:02