Kardinali Farrell alithibitisha rasmi kifo cha Papa Francisko
Vatican News
Ilikuwa ni saa 2:00 usiku masaa ya Ulaya, Jumatatu tarehe 21 Aprili 2025 ambapo Kardinali Kevin Farrell, Camerlengo wa Kanisa Takatifu katoliki la Roma alipoongoza ibada ya kuhakikisha kifo na kuwekwa kwa mwili wa marehemu Papa Francisko katika jeneza. Tukio hilo ilifanyika katika Kanisa dogo la nyumba ya Mtakatifu Marta mjini Vatican, mahali ambapo Papa Francisko alikuwa anaishi.
Waliohudhuria ni pamoja na Dekano wa Makardinali, Kardinali Giovanni Battista Re, na wanafamilia wa hayati Papa Francisko, pamoja na Dk Andrea Arcangeli na Dk. Luigi Carbone, Mkurugenzi na Naibu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Afya na Usafi jijini Vatican.
Kufuatia ibada hiyo, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Afya na Usafi wa Jimbo la Vatican, Dk Andrea Arcangeli alithibitisha kuwa Papa alifariki dunia baada ya kuugua kiharusi, hali iliyosababisha kukosa fahamu na kuporomoka kwa mfumo wa moyo usioweza kurekebishwa.
Kulingana na ripoti ya matibabu, ikumbukwe Papa alikuwa na historia ya kushindwa kupumua kwa papo hapo kulikosababishwa na nimonia ya pande mbili za virusi vya mkamba, shinikizo la damu,na kisukari cha Aina ya II.