MAP

Ijumaa Kuu: Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu yaani: Mateso, kifo na ufufuko wake ni kilele cha ufunuo wa: huruma, upendo, ukuu, utukufu na utakatifu wake. Ijumaa Kuu: Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu yaani: Mateso, kifo na ufufuko wake ni kilele cha ufunuo wa: huruma, upendo, ukuu, utukufu na utakatifu wake. 

Ijumaa Kuu: Msalaba Ni Ufunuo wa Huruma, Upendo, Msamaha na Upatanisho!

Fumbo la Msalaba yaani: Mateso, kifo na ufufuko wake ni kilele cha ufunuo wa: huruma, upendo, ukuu, utukufu na utakatifu wake, changamoto kwa Wakristo ni kushikamana pamoja na Kristo katika mapambano, ili siku moja waweze kushinda pamoja naye! Huu ndio ujumbe wa matumaini unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba, mwaliko kwa waamini kumtafakari Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kuwa ni kiini cha imani ya Kikristo.

Na Padre Pascha Ighondo, - Vatican.

Msalaba wa Kristo ni chombo cha wokovu na utukufu wa Mungu. Badala ya kashfa na utupu, Msalaba unakua ni chombo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Ni ishara ya mapendo, neema, sala, msamaha, upatanisho na matumaini. Ni kutokana na maana hii mpya, Mama Kanisa anaona fahari kuu kuutangaza utukufu na kuimba sifa kuu za Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Msalaba unaendelea kumfunza mwamini kwamba, hakuna mapendo kamili yasiyokuwa na mateso na matumaini ya uzima wa milele. Changamoto kwa waamini katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo ni kuuangalia, kuutafakari, kuushangaaa, kuusikiliza, kuuheshimu, kuutukuza na kuuabudu kwa imani, matumaini na mapendo, kwani ni kielelezo ambacho wokovu wa dunia umetundikwa juu yake! Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu yaani: Mateso, kifo na ufufuko wake ni kilele cha ufunuo wa: huruma, upendo, ukuu, utukufu na utakatifu wake, changamoto kwa Wakristo ni kushikamana pamoja na Kristo katika mapambano, ili siku moja waweze kushinda pamoja naye! Huu ndio ujumbe wa matumaini unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba, mwaliko kwa waamini kumtafakari Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kuwa ni kiini cha imani ya Kikristo. Fumbo la Msalaba ni alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu; kielelezo cha sadaka ya hali ya juu kabisa ya Kristo Yesu dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu; ubinafsi, dhuluma na nyanyaso. Msalaba ni alama ya ushindi dhidi ya dhambi na kifo. Msalaba ni kielelezo cha mateso, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo wanaouwawa kikatili kwa kuchomwa moto wangali hai; na wakati mwingine nyanyaso na dhuluma hizi zinatendwa katika hali ya ukimya mkubwa.

Ijumaa kuu: Mateso na Kifo cha Kristo Msalabani
Ijumaa kuu: Mateso na Kifo cha Kristo Msalabani   (ANSA)

Tafakari ya Neno la Mungu, Siku ya Ijumaa Kuu. Awali ya yote ikumbukwe kuwa hii ni siku ambayo Kanisa haliadhimishi Sakramenti zo zote ikiwa ni pamoja na Sadaka ya Misa Takatifu kwa kufuata mapokeo ya tangu zamani za kale kabisa. Altare inapaswa kuwa tupu kabisa, haina msalaba, wala mishumaa, wala vitambaa. Hii ni kwa sababu ni siku ambapo Kristo Yesu alikufa msalabani, ni siku ambayo alijitoa Yeye mwenyewe Sadaka, kafara ya mwanakondo wa Agano Jipya na la milele. Kumbe ni siku ambayo mama Kanisa anaadhimisha mateso na kifo cha Bwana wake Yesu Kristo. Hali kadhalika, siku ya Jumamosi Kuu Kanisa haliadhimishi Sadaka ya Misa Takatifu, liko kimya likiyawaza-waza mateso na kifo cha Yesu, Meza Takatifu, Altare iko tupu, mpaka zitakapoanza sherehe za Pasaka baada ya Vijilia Takatifu katika Kesha la ufufuko. Ibada anayoadhimisha Mama Kanisa Siku ya Ijumaa Kuu imegawanyika katika sehemu kuu tatu. Ibada hii inaanza kwa Padre na watumishi kuingia kanisani na kwenda moja kwa moja mbele ya altare wakiwa wamevaa mavazi mekundu kama kwa Misa. Nao wakifika mbele ya altare, wanatoa heshima mbele yake kwa kujilaza kifudifudi, au kupiga magoti kama hawawezi kujilaza kifudifudi, kisha wanasali kimya kimya kwa kitambo kidogo, wakiyatafakari mateso ya Kristo Yesu. Kisha wanakwenda kwenye viti, na Padre anasali sala ya mwanzo akiwa amefumba mikono, bila kusema tuombe kama ilivyo wakati wa misa za kawaida. Sala hii inaweka wazi dhamira kuu ya siku hii ikisema; “Ee Mungu, kwa mateso ya Kristu Mwanao Bwana wetu, umetuondolea mauti tuliyorithi sisi binadamu wote kwa dhambi ya kale. Utujalie sisi tuliozaliwa na hali ya kibinadamu kwa maumbile, vivyo hivyo tuzaliwe na hali ya kimungu kwa kutakaswa na neema yake.”

Fumbo la Mateso na mahangaiko ya binadamu halina majibu ya mkato.
Fumbo la Mateso na mahangaiko ya binadamu halina majibu ya mkato.   (AFP or licensors)

Kisha madhehebu hayo ya mwanzo, ndipo inaanza sehemu ya kwanza, liturujia ya Neno ambayo kiini chake ni simulizi la mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo. Sehemu hii ya Liturujia ya Neno inahitimishwa kwa maombezi kwa watu wote ikiwa ni sala; Kwa ajili ya Kanisa, kwa ajili ya Baba Mtakatifu na wenye daraja katika Kanisa – Maaskofu, Mapadre na Mashamesi, kwa ajili ya Wanafunzi wa Dini, kwa ajili ya umoja wa Wakristu, kwa ajili ya Wayahudi, na wale wasiomwamini Kristo, na wasiomwamini Mungu, kwa ajili ya Viongozi wa Serikali, na kwa ajili ya wenye taabu. Hivyo ni vyema katika sehemu hii kila mmoja ndani ya moyo wake kujiombea na kuwaombea wengine kila inapofika sehemu ya kutafakari, Padre anapotualika kusali akisema tuombe, tupige magoti, simameni. Haya maelekezo anayoyatoa Padre tusiyafanye tu kwa mazoea, bali tusali na kuomba kweli kweli tunapopiga magoti na tukisimama Padri anaposali kwa niaba ya watu wote, sisi tutafakari moyoni. Somo la kwanza ni la Kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 52:13-53:12). Somo hili ni tafakari ya Wasifu wa Mtumishi wa Mungu. Waamini wa Kanisa la mwanzo waliona uwakilishi wa Yesu Kristo katika sura ya mtumishi huyu wa Mungu aliyetukomboa kutoka utumwa wa dhambi kwa njia ya mateso; uso wake uliharibiwa sana, hakuwa na umbo wala uzuri wa kumtamani, alidharauliwa na kukataliwa na watu wake, mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko, na hakuhesabiwa kuwa kitu. Lakini ndiye aliyeyachukua masikitiko yetu, akajitwika huzuni zetu, alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu, adhabu yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Bwana aliweka juu yake maovu yetu sisi sote. Alionewa, lakini alinyenyekea, hakufunua kinywa chake mbele ya watesi wake. Alihukumiwa kwa kuonewa, akapigwa mijeledi kwa sababu ya makosa yetu, na akafanyiwa kaburi pamoja na wabaya. Ingawa hakutenda jeuri, wala hapakuwa na hila kinywani mwake, Bwana aliridhia kumchukua amehuzunisha, akaifanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi zetu. Kwa haki yake akawafanya wengi kuwa wenye haki, akamwaga nafsi yake hata kufa ili sisi wakosaji tukombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mauti.

Utukufu wa Kristo Umetundikwa juu ya Mlasaba
Utukufu wa Kristo Umetundikwa juu ya Mlasaba   (ANSA)

Katika mateso yake Yeye, Kristo Yesu Bwana wetu aliyaweka matumaini yake yote kwa Mungu Baba. Ni katika tumaini hili sisi nasi katika zaburi ya wimbo wa katikati tunasali na mzaburi tukisema; “Nimekukimbilia Wewe Bwana, nisiaibike milele, kwa haki yako uniponye. Mikononi mwako naiweka roho yangu; umenikomboa, Ee Bwana Mungu wa kweli. Kwa sababu ya watesi wangu, nimekuwa laumu, naam, hasa kwa jirani zangu, na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu, nao walioniona njiani walinikimbia. Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa, nimekuwa kama chombo kilichovunjika. Maana nisikiapo masingizio ya wengi, hofu ziko pande zote. Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana, nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu. Nyakati zangu zimo mikononi mwako, uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. Umwangaze mtumishi wako, kwa nuru ya uso wako, uniokoe kwa ajili ya fadhili zako. Iweni hodari, mpige moyo konde, ninyi nyote mnaomngoja Bwana (Zab. 31 :1, 5, 11-13a, 14-16, 24). Na hili ndilo tumaini letu sisi kwa Mungu Baba yetu wa Mbinguni. Somo la pili ni la Waraka kwa Waebrania (Ebr 4:14-16; 5: 7-9). Somo hili linatuasa tumwamini Yesu Kristo kuhani wetu mkuu aliyeonja na kuvumilia taabu na mateso mengi kwa ajili ya wokovu wetu. Maana Yeye anafahamu taabu na matatizo yetu, daima Yupo tayari kutuombea kwa Baba. Sharti ni hili; kuyashika maangano yetu tuliyofanya naye kwa njia ya ubatizo. Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 18:1-19, 42). Sehemu hii ya Injili inasimulia mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo, mtu mwenye haki asiye na hila ndani yake, kwa upendo wake, upole wake, unyenyekevu wake, uvumilivu wake na utii wake anakubali kutoa maisha yake kwa ajili yetu sisi wadhambi. Katika simulizi hili, Yuda alimsaliti Yesu kwa busu, ishara na alama ya upendo, maaskari wakamkamata wakiwa na taa mienge na silaha (Yn. 18:3), mitume wengine kwa hofu wakamkiambia na kumwacha peke yake.

Fumbo la kifo katika maisha ya binadamu
Fumbo la kifo katika maisha ya binadamu   (Vatican Media)

Baada ya kukamatwa, Yesu alipelekwa kwa kuhani mkuu Kayafa, mkuu wa Baraza la Wayahudi, “Sanhedri”, chombo chenye mamlaka ya juu ya kidini (Yn. 18:12-14); Baraza likaamuru apelekwe kwa gavana wa Kirumi, Pontio Pilato naye akaamuru apelekwe kwa mkuu wa mkoa wa Galilaya, Herode Antipas kwa vile Yesu alikuwa mwenyeji wa Nazareti katika Galilaya (Yn.18:28ff). Mahangaiko haya yote ni kwa sababu kila mamlaka haikuona hatia yoyote juu yake. Lakini alihukumiwa pasipo haki ili sisi tusio na haki tuwe na haki. Baada ya hukumu isiyokuwa ya haki Yesu alipigwa mijeledi, akavikwa taji ya miiba, akavuliwa nguo, akapigwa kwa mwanzi, akatemewa mate, akabebeshwa Msalaba mzito, akaanza safari kuelekea Golgota, alipofika alisulubiwa msalabani, akafa, nchi ikatetemeka, jua likafifia, kukawa na giza juu ya nchi, pazia la hekalu likapasuka mara mbili, alipotobolewa ubavu kwa mkuki, ilitoka damu na maji, chemchemi za Sakramenti za Kanisa.Ni katika mukatadha huu Msalaba umekuwa ni alama ya umoja wa kweli na Yesu Kristo. Kuuchukua Msalaba maana yake ni kuacha mambo ya dunia na fahari zake zinazokinzana na mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristo. Msalaba umekuwa ni chombo cha Ukombozi wa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi. Msalaba ni Sadaka ya Yesu, zao la upendo wake kwetu sisi. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, “Msalaba siyo ishara ya kifo, bali uzima; siyo ishara ya jambo la kuvunja moyo, bali matumaini; siyo ishara ya kushindwa, bali ya ushindi”. Msalaba sasa si tena alama ya adhabu bali ya wokovu ndiyo maana katika sala zetu na ibada zetu tunatumia ishara ya msalaba. Kila mkrito kwa kweli kama mtume Paulo hatuna budi kusema; “Lakini mimi hasha, nisione fahari ya kitu chochote ila msalaba wa Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu ulisulubishwa kwangu na mimi na ulimwengu” Gal.6:14. Msalaba ni muhuri na kitambulisho cha mkristo.

Njia ya Msalaba ni mwanzo wa maisha mapya
Njia ya Msalaba ni mwanzo wa maisha mapya   (Vatican Media)

Sehemu ya pili ya Ibada ya siku ya Ijumaa Kuu ni Kuuabudu Msalaba, Wokovu wa dunia uliotundikwa juu yake, ndiye Yesu Kristo. Msalaba umekuwa kwetu ishara ya ushindi dhidi ya dhambi na mauti kwa sababu Kristo mwana wa Mungu aliyechukua makosa yetu na adhabu tuliyostahili mwilini mwake, badala ya kuteswa sisi akateswa yeye, badala ya kusulibiwa sisi akasulibiwa yeye na badala ya kufa sisi kwa dhambi zetu akafa yeye kifo cha Msalabani. Hivyo tunafanya tendo la nje la kuuheshimu mti wa msalaba ambao kwao Kristo alikufa juu yake ili atukomboe na utumwa wa dhambi, na kumwabudu wokovu wetu ndiye Kristo Yesu juu ya msalaba ambao ni alama ya ukombozi. Hivyo tunapaswa kuliadhimisha tendo hilo kwa ibada na unyenyekevu kwa maana mbele ya Wokovu, Kristo Yesu, Nafsi ya Pili ya Utatu Mtakatifu, aliye Mungu kweli. Hivyo asiyeamini kuwa Wokovu wetu, Yesu Kristo yupo Msalabani, ni aheri asijongee mbele kuuabudu Msalaba, kwani hatafaidika na chochote, hatajipatia neema wala baraka zozote. Na mwenye imani na aukaribie msalaba, kwa moyo wa unyenyekevu, majuto, toba, ibada na sala shukrani, na maombi mbele za Mungu wetu katika nafsi ya pili, Yesu Kristo Mkombozi wetu. Sehemu ya tatu na ya mwisho inayohitimisha maadhimisho ya siku ya Ijumaa Kuu ni ibada ya Komunio Takatifu, tunda la mateso, kifo na ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo kama sala kabla ya Komunio inavyosema; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, wewe umetukomboa kwa kufa na kufufuka kwake Kristu Mwanao. Dumisha ndani yetu hiyo kazi ya huruma yako, ili tunaposhiriki fumbo hili tuishi katika uchaji sikuzote”. Mara baada ya kumaliza kuabudu Msalaba, kitambaa kinatandazwa juu ya altare na juu yake korporale na Misale ya Altare inawekwa karibu yake. Kisha shemasi au Padre mwenyewe akisindikizwa na watumishi wenye mishumaa inayowaka anakwenda kuleta Sakramenti Takatifu kutoka mahali ilipowekwa siku ya Alhamisi Kuu. Baada ya Ekaristi Takatifu kuweka Altareni, mara inafuata sala ya Baba Yetu na sala za kuwaalika waamini kupokea Ekaristi Takatifu.

Msalaba wa Kristo Yesu ni chemchemi ya uadilifu na utakatifu wa maisha
Msalaba wa Kristo Yesu ni chemchemi ya uadilifu na utakatifu wa maisha   (AFP or licensors)

Mama Kanisa anahitimisha maadhimisho haya kwa sala mbili. Sala ya kwanza ni baada ya Komunio akisali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, wewe umetukomboa kwa kufa na kufufuka kwake Kristu Mwanao. Dumisha ndani yetu hiyo kazi ya huruma yako, ili tunaposhiriki fumbo hili tuishi katika uchaji siku zote”. Na ya pili ni kuwaombea watu akisali hivi; “Tunakuomba, ee Bwana, baraka zako nyingi ziwashukie watu wako, ambao wamekumbuka kufa kwake Mwanao na kutazamia kufufuka kwao. Wapate rehena, wajaliwe kitulizo, waongezewe imani takatifu, wathibitishwe ukombozi wa milele”. Baada ya sala hizi waamini wote wanaondoka kimya kimya wakiyatafakari na kuyawaza-waza Mateso na kifo chake Yesu Kristo, mpaka siku ya Jumamosi Kuu, zitakapoanza sherehe za Mkesha wa Sherehe ya Pasaka. Hapo tena sherehe za kipasaka zitaendelea muda wa siku hamsini, mpaka Sherehe ya Pentekoste. Tumsifu Yesu Kristo!

Ijumaa Kuu 2025
17 Aprili 2025, 18:01