MAP

Kitengo kinachotoa huduma ya Kimataifa kwa Chama cha Kitume cha Wakarismatiki Wakatoliki, CHARIS kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Kitengo kinachotoa huduma ya Kimataifa kwa Chama cha Kitume cha Wakarismatiki Wakatoliki, CHARIS kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Jubilei ya Chama Cha Huduma ya Upyaisho Ya Wakarismatiki Wakatoliki Kimataifa!

Kitengo kinachotoa Huduma ya Kimataifa kwa Chama cha Kitume cha Wakarismatiki Wakatoliki, CHARIS kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo na Baba Mtakatifu Francisko anawatia shime, kuadhimisha Jubilei hii katikati ya moyo wa Kanisa, huku wakiinua sala zao kwa Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya watu wa Mungu, ustawi, maendeleo na mafanikio ya walimwengu. Kitengo hiki kinataka kujisadaka kwa ajili ya Kanisa pamoja na kutekeleza kwa dhati kabisa nia za Papa

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha limeanzisha kitengo maalum kijulikanacho kama “CHARIS” katika asili yake, neno hili maana yake ni “neema au zawadi maalum kutoka kwa Roho Mtakatifu”. Kwa sasa hiki ni kitengo kinachotoa huduma ya kimataifa kwa Chama cha Kitume cha Wakarismatiki Wakatoliki na kilizinduliwa rasmi tarehe 8 Desemba 2018, Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Hii ni siku ambayo ilizindua rasmi Katiba inayosimamia shughuli za kitengo hiki kama dira na mwongozo wa kusimamia na kukuza imani ya Kanisa Katoliki. Zote hizi ni kazi za Roho Mtakatifu zinazoendelea kupyaisha maisha na utume wa Kanisa. Kimsingi kitengo hiki, hakina mamlaka juu ya Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki, bali wataendelea kutekeleza dhamana na shughuli zao kama kawaida, chini ya ulinzi na usimamizi wa Maaskofu mahalia. Kila tawi linaweza kupata huduma na msaada wa kiufundi utakaokuwa unatolewa na CHARIS sehemu mbalimbali za dunia. Viongozi wa Kitengo cha CHARIS walianza kutekeleza dhamana na wajibu wao tangu wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste ya Mwaka 2019. Tangu wakati huo, Chama cha Huduma ya Upyaisho ya Wakarismatiki Wakatoliki Kimataifa “International Catholic Charismatic Renewal Services”, Chama cha Kidugu cha Wakarismatiki wa Jumuiya za Agano “Fraternity of Charismatic Covenant Communities” pamoja na Chama cha Umoja wa Wakarismatiki, “Fellowship” vilikoma kutoa huduma. Rasilimali yote ya vyama hivi ilipaswa kuhamishiwa kwenye kitengo cha CHARIS, ili kukijengea uwezo wa kiuchumi wa kutekeleza dhamana na wajibu wake kadiri ya matakwa ya Baba Mtakatifu Francisko. Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki, wengine wanapenda kukiita kama “Mkondo” unaovuviwa na Roho Mtakatifu ambaye ndiye aliyepewa dhamana ya kumshuhudia Kristo Yesu kwa kutakatifuza, kufundisha, kuongoza, kukumbusha pamoja na kuwasaidia waamini kutumia karama zao kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Hiki ni kikundi kinachopaswa kustawisha karama za binadamu, ili waweze kupata wokovu kwa kuendelea kumakinika na karama zao za kiroho kwa utukufu wa Mungu, ukuaji wa Kanisa na wokovu wa walimwengu wote.

Papa Francisko anawataka Charis kuwa ni vyombo vya amani na upatanisho
Papa Francisko anawataka Charis kuwa ni vyombo vya amani na upatanisho

Baba Mtakatifu Francisko anatambua na kuthamini mchango wa Wakarismatiki Wakatoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Wakarismatiki wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya uekumene wa kiroho, huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii sanjari na kudumisha umoja na mshikamano wa Kanisa. Wanachama wake wanapaswa kujikita katika toba na wongofu wa kitume na kimisionari, kwa kuonesha upendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, ili Mwenyezi Mungu atukuzwe na binadamu atakatifuzwe na hatimaye, akombolewe! Hiki ni chama ambacho kina tofautiana kwa mtindo wa maisha ya sala na huduma, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko amependa kuwaunganisha wanachama wake wote katika utofauti wao, ili kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa. CHARIS inaendelea kuratibu shughuli za Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki mintarafu Mafundisho ya Mababa wa Kanisa, lakini kwa namna ya pekee, mchango wa Baba Mtakatifu Francisko tangu mwaka 2014 na kilele chake ni katika hotuba yake aliyoitoa tarehe 3 Juni 2017 wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki duniani. Hii ni sehemu ya marekebisho makubwa yanayoendelea kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kukazia umoja na utofauti kadiri ya karama na mapaji ya Roho Mtakatifu. Kristo Yesu ni mlango wa huruma na faraja, wema na uzuri usiokuwa na kifani. Huu ndio mlango wanamopita watu wenye haki. Kristo Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Yesu anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani. Bikira Maria, nyota ya alfariji anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma ya Mungu.

Papa anakazia heshima na nidhamu ndani ya Chama hiki
Papa anakazia heshima na nidhamu ndani ya Chama hiki   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Maadhimisho ya Jubilei ni fursa ya kuimarika: kiroho na kiutu! Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” Matumaini ya waamini yako katika Msalaba, yaani katika Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu aliyezaliwa katika Familia Takatifu iliyopata baraka ya kuwa na Mungu yaani Emanueli kati yake. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupita katikati ya Mlango wa Imani kwani Kristo Yesu anasema “Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho.” Rej. Yn 10: 1-18. Huu ni mwaliko kwa Wakristo wote kuwa ni mahujaji wa matumaini yasiyo danganya; umoja unaopaswa kuimarishwa; kukuzwa na kujenga haki, amani na furaha ya kweli katika Kristo Yesu. Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; huruma inayowakumbatia binadamu wote pasi na ubaguzi, changamoto na mwaliko wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Huu ni mlango unawaohamasisha waamini kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani kwa kuambata Injili ya furaha, daima wakimwangalia Kristo Yesu waliyemtoboa kwa mkuki ubavuni, kimbilio la wakosefu na wadhambi; watu wanaohitaji msamaha, amani na utulivu wa ndani.

Charis wawe ni wajenzi wa haki, amani na maridhiano
Charis wawe ni wajenzi wa haki, amani na maridhiano   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Kitengo kinachotoa huduma ya Kimataifa kwa Chama cha Kitume cha Wakarismatiki Wakatoliki, CHARIS kinaadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo na Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuwaandikia ujumbe, unaowatia shime, kuadhimisha Jubilei hii katikati ya moyo wa Kanisa, huku wakiinua sala zao kwa Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya watu wa Mungu, ustawi, maendeleo na mafanikio ya walimwengu. Kitengo hiki kinataka kujisadaka kwa ajili ya Kanisa pamoja na kutekeleza kwa dhati kabisa nia za Baba Mtakatifu kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu, lakini zaidi kwa ajili ya kuombea amani na upatanisho. Wanapaswa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu ni zawadi ya Kristo Mfufuka, ni chemchemi ya ushirika, amani, utulivu na udugu wa kibinadamu.Kimsingi, Kanisa ni kielelezo cha ubinadamu mpya uliopatanishwa na kwamba, huu ni uzoefu unaowakumbatia na kuwaambata watu wote wa Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika wanachama wa CHARIS kushiriki kikamilifu na ulimwengu ili waweze kuwa ni chanzo cha matumaini na amani. Roho Mtakatifu anaweza kutoa amani ya kweli kwa mioyo ya wanadamu, ambayo ni muhimu kwa kushinda migogoro katika familia, katika jamii na kati ya Mataifa. Baba Mtakatifu anawataka CHARIS kuwa ni mashuhuda, mafundi na wajenzi wa amani na umoja, huku wakijitahidi kujenga na kudumisha ushirika katika vikundi na jumuiya zao; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu katika Kristo Yesu. Wawe na heshima na nidhamu kwa viongozi wao na wala kamwe wasiwe ni chanzo cha kinzani na migogoro. Wawe tayari kushirikiana na kushikamana na wengine katika maisha na utume wao kwenye Parokia, ili waweze kupata baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo kuzaa matunda mengi. 

Jubilei Charis 2025
03 Aprili 2025, 16:46