ĐÓMAPµĽş˝

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo, Wakleri wa Jimbo kuu la Roma, Alhamisi tarehe 6 Machi 2025 watakuwa na muda wa kufunga, kusali, kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo, Wakleri wa Jimbo kuu la Roma, Alhamisi tarehe 6 Machi 2025 watakuwa na muda wa kufunga, kusali, kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao.  (Vatican Media)

Wakleri wa Jimbo Kuu la Roma Mahujaji wa Matumaini, Toba na Wongofu wa Ndani

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo, Wakleri wa Jimbo kuu la Roma, Alhamisi tarehe 6 Machi 2025 watakuwa na muda wa kufunga, kusali, kujipatanisha na Mungu pamoja na kupitia Lango la Huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Lateran. Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo”, anawaalika wakleri wa Jimbo kuu la Roma kushiriki kwa wingi, ili waweze kujichotea neema na baraka katika kipindi hiki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” Matumaini ya waamini yako katika Msalaba, yaani katika Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu aliyezaliwa katika Familia Takatifu iliyopata baraka ya kuwa na Mungu yaani Emanueli kati yake.  Huu ni muda muafaka wa kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu; kwa kuweka kando mizigo ya zamani, na kupyaisha msukumo kuelekea siku zijazo; ili kusherehekea uwezekano wa mabadiliko katika maisha, kwa kujitahidi kupyaisha utambulisho wa waamini na kuwa jinsi walivyo, kwa njia ya imani, tayari kushuhudia ubora wao katika maisha ya kila siku. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupita katikati ya Mlango wa Imani kwani Kristo Yesu anasema “Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho.” Rej. Yn 10: 1-18. Uzinduzi wa Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Mwaka 2025 ya Ukristo uliwahusisha wajumbe kutoka katika Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo, ili kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani, Kristo Yesu, Mungu kweli na Mtu kweli. Huu ni mwaliko kwa wajumbe hawa kuunganika na Kanisa Katoliki kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu, Mlango wa uzima wa milele. Huu ni mwaliko kwa Wakristo wote kuwa ni mahujaji wa matumaini yasiyo danganya; umoja unaopaswa kuimarishwa; kukuza na kujenga haki, amani na furaha ya kweli katika Kristo Yesu. Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; huruma inayowakumbatia binadamu wote pasi na ubaguzi, changamoto na mwaliko wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.

Mapadre wanafundisha, ongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu
Mapadre wanafundisha, ongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu   (Vatican Media)

Huu ni mlango unawaohamasisha waamini kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani kwa kuambata Injili ya furaha, daima wakimwangalia Kristo Yesu waliyemtoboa kwa mkuki ubavuni, kimbilio la wakosefu na wadhambi; watu wanaohitaji msamaha, amani na utulivu wa ndani.Kristo Yesu ni mlango wa huruma na faraja, wema na uzuri usiokuwa na kifani. Huu ndio mlango wanamopita watu wenye haki. Kristo Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Yesu anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani. Bikira Maria, nyota ya asubuhi anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anasema, kunako mwaka 2015, Kanisa liliadhimisha Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu; mwaka ambao uliwawezesha waamini wengi kuvuka Lango la Huruma ya Mungu, ili kuonja upendo unaofariji, unaosamehe na kutoa matumaini. Hii ndiyo hamu inayopaswa kushuhudiwa na watu wote wa Mungu kwa kuwaonjesha jirani zao wema na huruma ya Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu anawataka waamini kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amejishusha ili kuwaokoa, mwaliko kwao pia ni kujishusha na kuwainamia jirani zao wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali, kwa kuwa na jicho la huduma kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, ili kuwaonjesha watu wanaoteseka, ile “divai ya furaha na matumaini pamoja na kuwapaka mafuta ya faraja,” kama ilivyotokea kwenye Injili ya Msamaria Mwema.

Mapadre ni Mahujaji wa Matumaini, Toba na Wongofu wa ndani
Mapadre ni Mahujaji wa Matumaini, Toba na Wongofu wa ndani   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Huu ni wito wa kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu, Mlango wa uzima wa milele na hivyo wakristo wote wanaalikwa kuwa ni mahujaji wa matumaini yasiyo danganya; umoja unaopaswa kuimarishwa; kukuza na kujenga haki, amani na furaha ya kweli katika Kristo Yesu. Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; huruma inayowakumbatia binadamu wote pasi na ubaguzi, changamoto na mwaliko wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Maadhimisho ya Jubilei ni fursa ya kuimarika: kiroho na kiutu! Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ni mwaliko wa kufanya mabadiliko katika maisha; Ni Pasaka ya kufanywa upya, kuingia katika maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu; Hii ni Pasaka ya kupyaishwa katika maisha na utu wa ndani, kwa kukutana na Kristo Yesu. Kristo Yesu katika maisha na utume wake wa hadhara alijitambulisha kuwa ni Mchungaji mwema, hali ambayo ilijidhihirisha katika ushuhuda wa maisha yake ya kila siku kiasi cha kusema kwamba, Yeye ndiye mchungaji mwema anayeutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Kristo Yesu ni mlango salama wa kondoo na kondoo humsikia sauti yake kwa sababu huwaita kwa majina na kuwapeleka nje kwa kuwatangulia nao humfuata nyuma. Anawajua walio wake na walio wake wanamjua fika. Rej. Yn. 10: 1-18. Wito na maisha ya Kipadre ni zawadi na sadaka kubwa inayotolewa kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Huu ni utimilifu wa wito unaowawezesha Mapadre kuwa ni Kristo mwingine kwa kutenda kama Kristo Yesu “In persona Christi”. Maisha na utume wa kipadre yanatekelezwa kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa kuadhimisha Sakramenti za Kanisa pamoja na kuwahudumia watu wa Mungu kwa upendo.

Kristo Yesu ni Mlango wa matumaini, maisha na uzima wa milele
Kristo Yesu ni Mlango wa matumaini, maisha na uzima wa milele   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kwa ufupi kabisa, Mapadre wanashiriki katika huduma ya: Kufundisha, Kuongoza na Kuwatakatifuza watu wa Mungu. Huu ni mwendelezo wa kazi ya ukombozi ambayo Kristo Yesu amekuja kuitekeleza hapa duniani, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu, kielelezo makini cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Mapadre wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili baada ya kukutana na Kristo Mfufuka. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha; ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali ubinafsi ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya mang’amuzi ya huruma inayowakirimia furaha, hata kama maisha yao bado yanasheheni matatizo na changamoto mbalimbali, ili kuondokana na utamaduni wa huzuni, utupu na upweke unaopelekea msongo wa mawazo kwa watu wengi! Huruma ya Mungu inajidhihirisha kwa namna ya pekee, katika maadhimisho ya Sakramenti za Uponyaji yaani: Sakramenti ya Upatanisho na Mpako wa wagonjwa. Baba Mtakatifu anapenda kutoa mkazo wa pekee katika Sakramenti ya Upatanisho inayowaonjesha waamini huruma, upendo na msamaha wa dhambi; mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kumwilisha upendo wa Mungu katika maisha.  Mapadre wanakumbushwa kwamba, utume wao wa Kipadre unajikita katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho zinazofumbatwa katika ukarimu, ushuhuda, huruma; ukweli na uwazi katika kanuni maadili.

Kristo Yesu ni Mchungaji mwema
Kristo Yesu ni Mchungaji mwema   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mapadre wawe tayari kuwasindikiza waamini katika hija ya toba na wongofu wa ndani, kwa kuonesha uvumilivu; kwa kuwa na mawazo mapana na wakarimu katika kutoa msamaha wa Mungu. Mapadre pia wanapaswa kuwa ni kielelezo cha toba na wongofu wa ndani na kwamba, Sakramenti ya Upatanisho inapaswa kuwa ni kiini cha maisha ya Kikristo kwani Mapadre ni vyombo vya Upatanisho. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo, Wakleri wa Jimbo kuu la Roma, Alhamisi tarehe 6 Machi 2025 watakuwa na muda wa kufunga, kusali, kujipatanisha na Mungu pamoja na kupitia Lango la Huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Lateran. Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo”, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wakleri wa Jimbo kuu la Roma kushiriki kwa wingi, ili waweze kujichotea neema na baraka katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” Matumaini ya waamini yako katika Msalaba, yaani katika Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu.

Hija ya Makleri wa Roma 2025
05 Machi 2025, 15:08