Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko Kwa Kipindi Cha Kwaresima 2025: Mahujaji wa Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Mwaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu: Mahujaji wa matumaini “Peregrinantes in spem” ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Kipindi cha Kwaresima ni fursa ya kuamsha na kupyaisha ari na mwamko wa kimisionari, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuwakumbuka na kuwaombea wainjilishaji wote, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa kile wanacho amini, kufundisha na kuadhimisha. Iwe ni fursa ya kugundua na kutambua kwamba, wao kama waamini ni Mitume wa Yesu, changamoto na mwaliko wa kutafuta na kuambata mapenzi ya Mungu katika maisha.
Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha na kuboresha imani, matumaini na mapendo kwa: kufunga na kusali; kwa kufanya toba na malipizi ya dhambi; kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa; Kwa kusoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji.Lengo ni kujitakasa na kuambata utakatifu wa maisha, ili hatimaye, kushiriki furaha ya Kristo Mfufuka wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana, huku wakiwa wamepyaishwa kwa neema ya Roho Mtakatifu. Waamini watambue kwamba wanaitwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa watu wanaowazunguka na wale wote ambao Mwenyezi Mungu anawajalia fursa ya kukutana nao katika hija ya maisha yao, ili waweze kujaliwa mwanga na furaha ya Injili katika maisha yao. Mateso na kifo cha Kristo Msalabani, kiwe ni kikolezo cha toba na wongofu wa ndani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anayesema: “Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.” Gal 1: 22-24. Waamini wajitahidi kuwa na kumbukumbu hai ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Ni wakati wa kuuvua utu wa kale na kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Kipindi cha Kwaresima kinasimikwa katika nguzo kuu nne: yaani; Sala, Kufunga, Neno la Mungu na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji. Baba Mtakatifu Francisko aawatakia ndugu zake Wakristo kheri na baraka katika Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2025.
Wakati huo huo, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema: “Katika kipindi hiki cha siku arobaini za ibada, kufunga na kufanya toba, tuendelee kuiombea nchi yetu amani, upendo, umoja, utulivu na yote yaliyo mema, huku tukiwakumbuka wenye uhitaji. Tutumie pia kipindi hiki kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu azidi kutuongoza katika kuuishi ukweli na uadilifu kwenye utekelezaji wa majukumu yetu kwa wenzetu, na kwa nchi yetu.” Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 unanogeshwa na kauli mbiu “Tutembee kwa pamoja katika matumaini.” Kwaresima ni kipindi cha imani na matumaini; toba na wongofu wa ndani, ili kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa mtu mmoja mmoja na kama Jumuiya ya waamini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya hija ya imani na matumaini, kama ilivyokuwa kwa Waisraeli, waliotembea Jangwani kwa muda wa miaka arobaini, wakapata fursa ya toba na wongofu wa ndani. Hii ni safari ya pamoja kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kwa kutoka katika ubinafsi wao na hivyo kujielekeza katika ujenzi wa umoja kwa kujitambua kwamba, wao wote wamekuwa ni wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Rej. Gal 3:26-28, mwaliko wa kuweka nia ya kuweza kufikia lengo kwa kusikilizana katika upendo na uvumilivu.
Kipindi cha Kwaresima ni fursa kwa watu wa Mungu kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana, kwa kutembea na kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu; kwa kuonesha upendo na ukarimu kwa wahitaji zaidi, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani mintarafu ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Watu wa Mungu wanaalikwa kutembea katika mwanga wa matumaini kwani “tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5, kiini cha ujumbe wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo na kwamba, hatima ya Kipindi cha Kwaresima ni maadhimisho ya ushindi wa Pasaka, kielelezo cha upendo mkamilifu. “Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Rum 8: 38-39. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Kristo Yesu ni upendo na tumaini la waamini, ndiye aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ushindi wa ufufuko wa wafu ndicho kiini cha imani na matumaini ya Wakristo. Waamini wanaalikwa kuambata toba na wongofu wa ndani, kwa kujiaminisha kwa Mwenyezi mungu, ili kupata maisha na uzima wa milele. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, anasamehe dhambi, mwaliko kwa waamini kujikita katika matumaini ili waweze kusoma alama za nyakati tayari kujidhatiti katika haki, ujenzi wa udugu wa kibinadamu, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote bila kumwacha mtu yeyote nyuma. Kwa hakika upendo wa Mungu unawafanya waamini kuwa ni watunzaji wa matumaini ambayo kamwe hayatahayarishi, matumaini ambayo ni nanga ya maisha, yenye uhakika na imara na kwamba, ndani ya Kanisa wote wanapata wokovu. Rej. 1Tim 2: 4 na kusubiri utukufu wa Kristo Yesu atakapounganika na Kanisa mchumba wake mwaminifu. Bikira maria Mama wa matumaini, awaombee na kuwasindikiza katika hija hii ya kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025.