MAP

Kwaresima ni kipindi maalum cha kuwaandaa Wakristo kuweza kuteseka, kufa na hatimaye kufufuka na Kristo Yesu. Kwaresima ni kipindi maalum cha kuwaandaa Wakristo kuweza kuteseka, kufa na hatimaye kufufuka na Kristo Yesu.   (Vatican Media)

Kwaresima Ni Kipindi Cha Kuzama Katika Utajiri Na Amana ya Imani

Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, tayari kukimbiliana na kuambata huruma, upendo na msamaha wa Mungu. Ni kipindi cha kukesha kiroho kwa kusali, kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anakumbusha kwamba, tangu zamani, Kwaresima kilikuwa ni kipindi pia cha kuwaandaa wakatekumeni kuweza kuzaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu, katika mkesha wa Sherehe ya Pasaka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha na kuboresha imani, matumaini na mapendo kwa: kufunga na kusali; kwa kufanya toba na malipizi ya dhambi; kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa; Kwa kusoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji.Lengo ni kujitakasa na kuambata utakatifu wa maisha, ili hatimaye, kushiriki furaha ya Kristo Mfufuka wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana, huku wakiwa wamepyaishwa kwa neema ya Roho Mtakatifu. Waamini watambue kwamba wanaitwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa watu wanaowazunguka na wale wote ambao Mwenyezi Mungu anawajalia fursa ya kukutana nao katika hija ya maisha yao, ili waweze kujaliwa mwanga na furaha ya Injili katika maisha yao. Mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani, kiwe ni kikolezo cha toba na wongofu wa ndani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anayesema: “Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.” Gal 1: 22-24. Waamini wajitahidi kuwa na kumbukumbu hai ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Ni wakati wa kuuvua utu wa kale na kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Kipindi cha Kwaresima kinasimikwa katika nguzo kuu nne: yaani; Sala, Kufunga, Neno la Mungu na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji.

Kwaresima ni kipindi cha kuzama katika amana na utajiri wa Imani.
Kwaresima ni kipindi cha kuzama katika amana na utajiri wa Imani.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 unanogeshwa na kauli mbiu “Tutembee kwa pamoja katika matumaini.” Kwaresima ni kipindi cha imani na matumaini; toba na wongofu wa ndani, ili kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa mtu mmoja mmoja na kama Jumuiya ya waamini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya hija ya imani na matumaini, kama ilivyokuwa kwa Waisraeli, waliotembea Jangwani kwa muda wa miaka arobaini, wakapata fursa ya toba na wongofu wa ndani. Hii ni safari ya pamoja kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kimisionari na Kisinodi, kwa kutoka katika ubinafsi wao na hivyo kujielekeza katika ujenzi wa umoja kwa kujitambua kwamba, wao wote wamekuwa ni wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Rej. Gal 3:26-28, mwaliko wa kuweka nia ya kuweza kufikia lengo kwa kusikilizana katika upendo na uvumilivu. Kipindi cha Kwaresima ni fursa kwa watu wa Mungu kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana, kwa kutembea na kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu; kwa kuonesha upendo na ukarimu kwa wahitaji zaidi, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani mintarafu ujenzi wa Kanisa la Kimisionari na Kisinodi. Watu wa Mungu wanaalikwa kutembea katika mwanga wa matumaini kwani “tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5, kiini cha ujumbe wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo na kwamba, hatima ya Kipindi cha Kwaresima ni maadhimisho ya ushindi wa Pasaka, kielelezo cha upendo mkamilifu. “Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Rum 8: 38-39.

Kwaresima ni hija ya Ubatizo, Sala, Kufunga na matendo adili na matakatifu
Kwaresima ni hija ya Ubatizo, Sala, Kufunga na matendo adili na matakatifu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, mwenye umri wa miaka 88, katika tafakari yake ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025, anakazia umuhimu wa waamini kuzama zaidi katika amana na utajiri wa imani; kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano binafsi na ya kijamii na Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu. Kristo Yesu, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kumbe Kwaresima ni muda muafaka wa kusali, kufunga na kujisadaka kwa ajili ya wahitaji mbalimbali. Ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, tayari kukimbiliana na kuambata huruma, upendo na msamaha wa Mungu. Ni kipindi cha kukesha kiroho kwa kusali, kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anakumbusha kwamba, tangu zamani, Kwaresima kilikuwa ni kipindi pia cha kuwaandaa wakatekumeni kuweza kuzaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu, katika mkesha wa Sherehe ya Pasaka. Kumbe, Patriaki Bartolomeo wa kwanza anakaza kusema, Kwaresima ni kipindi maalum cha kuwaandaa Wakristo kuweza kuteseka, kufa na hatimaye kufufuka na Kristo Yesu. Katika Mkesha wa Sherehe ya Pasaka, waamini wanapyaishwa tena katika Ubatizo, kwa kurudia tena ahadi zao za Ubatizo, mwanzo mpya wa maisha ya Mkristo. Liturujia ya Kipindi cha Kwaresima inakita mizizi yake katika mapambano ya maisha ya kiroho, ili hatimaye kuweza kusherehekea Pasaka ya Bwana kwa furaha kubwa.

Kwaresima ni kipindi cha kuzama katika amana na utajiri wa Kanisa kiimani
Kwaresima ni kipindi cha kuzama katika amana na utajiri wa Kanisa kiimani

Mfungo wa Kwaresima, usiwe ni kwa waamini kutaka kujionesha na kujimwambafai, bali hufanyike mintarafu uhuru wa watoto wa Mungu; katika ukweli na haki unaofumbatwa katika Injili ya huduma ya upendo, kama anavyosimulia Mwinjili Luka 10: 30-37: Injili ya Msamaria mwema. Katika hukumu ya mwisho, waamini  wataulizwa jinsi walivyomwilisha Injili ya upendo kwa jirani zao. Rej Mt 25: 31-46. Kufunga kwa Mkristo kueleweke pia ni kupambana na vishawishi, dhambi na nafasi za dhambi; ni mapambano dhidi ya uchoyo na ubinafsi; kwa kujikita katika ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kwaresima ni hija ya maisha ya kiroho, kuelekea maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa wafu: “kwa kuwa viumbe vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibifu, hata viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.” Rum 8:21. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yana mwelekeo wa Kiekumene kwani wakristo wanataka kutembea pamoja na Kristo Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima. Watu wanamtafuta Kristo Yesu hata bila ya kutambua. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupita katikati ya Mlango wa Imani, sanjari na kutangaza na kushuhudia kanuni ya Imani ya Nicea. Kristo Yesu anasema “Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho.” Rej. Yn 10: 1-18. Huu ni mwaliko kwa Wakristo wote kuwa ni mahujaji wa matumaini yasiyo danganya; umoja unaopaswa kuimarishwa; kukuza na kujenga haki, amani na furaha ya kweli katika Kristo Yesu. Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; huruma inayowakumbatia binadamu wote pasi na ubaguzi, changamoto na mwaliko wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.

Injili ya Matumaini dhidi ya hofu, mashaka na ukosefu wa imani thabiti
Injili ya Matumaini dhidi ya hofu, mashaka na ukosefu wa imani thabiti

Huu ni mlango unawaohamasisha waamini kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani kwa kuambata Injili ya furaha, daima wakimwangalia Kristo Yesu waliyemtoboa kwa mkuki ubavuni, kimbilio la wakosefu na wadhambi; watu wanaohitaji msamaha, amani na utulivu wa ndani. Kristo Yesu ni mlango wa huruma na faraja, wema na uzuri usiokuwa na kifani. Huu ndio mlango wanamopita watu wenye haki. Kristo Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Yesu anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani tayari kuambata utakatifu wa maisha. Bikira Maria, nyota ya alfajiri anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma ya Mungu.

Kwaresima 2025
27 Machi 2025, 13:49