Papa atuma ujumbe kwa Askofu Mkuu wa Tirana,Durrës na Albania yote
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika siku ya kusimikwa rasmi kwa Askofu Mkuu wa Kirothodox Joan Pelushi, wa Kanisa Kuu la Tirana, Durrës na Albania yote, Jumamosi tarehe 29 Machi 2025, Baba Mtakatifu Francisko alituma ujumbe wake ambao ulisomwa na mwakilishi wake, Askofu Mkuu Flavio Pace, Katibu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Kikristo ambaye aliongozana na wajumbe wengine, Monsinyo Andrea Palmieri, Katibu Msaidizi wa Baraza hilo hilo na Monsinyo IonuÅ£ Paul Strejac, Mhusika wa masuala ya jumla ya Ubalozi wa Vatican. Katika ujumbe huo, Baba Mtakatifu Francisko anaonesha furaha pekee kwamba anatoa salamu zake za heri ya kidugu katika upendo wa Kristo wakati wa kusimikwa kwake rasmi kama Askofu Mkuu wa Tirana, Durrës na Albania Yote.
Katika kueleza ukaribu wake wa kiroho, amemhakikishia maombi yake kwa kwamba Mungu Baba, chanzo cha mema yote, na kwamba atampatia karama tele za Roho Mtakatifu anapoliongoza kundi lililokabidhiwa uangalizi wake. Papa Francisko amebanisha kuwa “Sasa yeye ni mrithi wa ndugu yetu mpendwa wa kumbukumbu ya Patriaki Anastas, ambaye ushuhuda wake wa maisha ya Kikristo na bidii ya kitume uliacha urithi wa kina na wa kudumu nchini Albania. Miongoni mwa shughuli zake nyingi wakati wa huduma yake, Anastas alijipambanua kwa kujitolea kwake kuishi pamoja kwa amani wanaume na wanawake wa Makanisa tofauti na mapokeo ya kidini, na alichangia kwa kiasi kikubwa kuboresha mahusiano kati ya Makanisa yetu.
Kutokana na hilo Papa Francisko anao uhakika kuwa tabia njema yake kwa kufuata mfano wa mtangulizi wake, itaendelea kukuza mazungumzo kama njia ya kushinda migawanyiko na kuendeleza utafutaji wa ushirika kamili kati ya wanafunzi wote wa Kristo. Kwa hakika, katika nyakati hizi ngumu zenye vita na ghasia, ni jambo la dharura zaidi kwamba Wakristo watoe ushuhuda wa kuaminika wa umoja, ili walimwengu waweze kukumbatia kikamilifu ujumbe wa Injili wa mshikamano wa kidugu na amani. Papa aidha alsisitiza kwamba “kwa hivyo tunabeba jukumu la kuendelea pamoja ili kudhihirisha kwa njia inayoonekana zaidi ule ushirika halisi, ikiwa ule ambao bado haujakamilika, na ambao tayari unatuunganisha.
Kwa hiyo, ni matumaini ya dhati ya Baba Mtakatifu kwamba chini ya uongozi wake wa kibaba, mahusiano kati ya Kanisa la Korthodox la Albania na Kanisa Katoliki yatastawi zaidi, huku tukitafuta aina mpya za ushirikiano wenye matunda katika kutangaza Injili, kuwahudumia wale wanaohitaji zaidi na kufanya upya dhamira yetu ya kutatua masuala ambayo bado yanatutenganisha kwa njia ya mazungumzo ya upendo na ukweli. Kwa hisia hizo na kwa mara nyingine tena Papa alielezea uhakikisho wa maombi yake na matashi mema huku akimwomba Mwenyezi Mungu ampatie kila neema na baraka za mbinguni katika huduma yake ya juu na amemtume heri nyingi na mkubatio wa kidugu katika Kristo Bwana wetu.