MAP

Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana,” ni muda wa sala, tafakari na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana,” ni muda wa sala, tafakari na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mpango Mkakati wa Saa 24 Kwa Ajili ya Bwana Kwa Mwaka 2025

Papa Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordiae vultus”, yaani “Uso wa huruma” anawaalika waamini kushiriki kikamilifu katika Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana,” unaoadhimishwa Ijumaa na Jumamosi kabla ya Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima na katika maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, mpango huu unaadhimishwa tarehe 28 na 29 Machi 2025 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Wewe ni tumaini langu” Zab 71:5

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordiae vultus”, yaani “Uso wa huruma” anawaalika waamini kushiriki kikamilifu katika Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana,” unaoadhimishwa Ijumaa na Jumamosi kabla ya Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima na katika maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, mpango huu unaadhimishwa tarehe 28 na 29 Machi 2025 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Wewe ni tumaini langu” Zab 71:5. Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yanayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa maisha na uzima wa milele. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni “Mahujaji wa Matumaini” mahali popote pale walipo! Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana,” unatoa kipaumbele cha kwanza kwa maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho, kuwa ni kitovu cha maisha na shughuli za kichungaji kwa Makanisa mahalia kwa kujikita katika huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu dhaifu na mdhambi. Mwenyezi Mungu anajisikia kuwajibika, kwa maana ya kwamba, anatamani kuwaona watu wake wakiwa na afya njema, furaha na amani tele nyoyoni mwao. Hii ni njia ambayo upendo wa huruma ya Wakristo unaopaswa pia kujimwilisha. Huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole linalouonesha kwa waamini; hakuna chochote katika mahubiri na ushuhuda wake kwa ulimwengu kinachoweza kukosa huruma.

Mpango Mkakati wa Saa 24 kwa ajili ya Bwana 2025
Mpango Mkakati wa Saa 24 kwa ajili ya Bwana 2025   (Carlos Moioli)

Umahiri wa Kanisa unaonekana kwa namna linavyoonesha huruma na upendo. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele kama ilivyokuwa kwa Injili ya Baba Mwenye huruma na Mwana mpotevu, shilingi na kondoo aliyepotea. Huruma ya Mungu inawawezesha watu kutambua na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao hasa wale wanaohitaji kuonjeshwa faraja na upendo. Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini: kuamini na kuyaishi yote haya kama mashuhuda wa Injili ya huruma, furaha na mapendo. Mama Kanisa anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika Sakramenti ya Upatanisho kama mahali muafaka pa kuonja: msamaha wa dhambi, huruma na upendo wa Mungu, tayari kusimama tena na kuendelea na safari ya imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani! Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha Mapadre waungamishaji kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa upatanisho, huruma na upendo wa Mungu na kamwe si wamiliki wa dhamiri za waamini. Wajenge utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa makini, ili wawasaidie waamini wao kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu maisha na wito wao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake! Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu inapaswa kuendelea kumwilishwa katika maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia kama alama ya mwendelezo wa Mwaka wa Huruma ya Mungu.

Ni muda wa kuabudu Ekaristi Takatifu na Kulitafakari Neno la Mungu
Ni muda wa kuabudu Ekaristi Takatifu na Kulitafakari Neno la Mungu   (Vatican Media)

Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana,” ni muda wa sala, tafakari na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Ni wakati wa kuchunguza vyema dhamiri kwa kuongozwa na mwanga wa Neno la Mungu pamoja na Amri za Mungu. Lengo ni kumwezesha mwamini kujitakasa, kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu tayari kuambata huruma, upendo na msamaha wake ili kupyaisha urafiki wa dhati kabisa na Mwenyezi Mungu. Mpango Mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” unaadhimishwa Ijumaa na Jumamosi zinazotangulia Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima. Kila Jimbo linapaswa kufanya maadhimisho haya ili kuwapatia waamini nafasi ya kuweza kuchunguza dhamiri zao, kujuta, kuungama na hatimaye kutimiza malipizi, ili kuambata huruma ya Mungu katika maisha yao, kwa kutambua kwamba, huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wa Mungu kwa binadamu. Kwa njia hii, waamini nao wanapaswa kuwa ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao. Hii ni huruma inayopaswa pia kushuhudiwa katika maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho inayogusa undani wa mtu, kwani hili ni chimbuko la amani na utulivu wa ndani. Ni huruma inayosamehe na kuokoa. Mapadre waungamishi wanao wajibu wa kuwa ni watumishi waaminifu wa huruma na msamaha wa Mungu kwa binadamu, kwa kuwapokea waamini wanaokimbilia kiti cha huruma ya Mungu, au “Mahakama ya Huruma ya Mungu kama alivyofanya Baba mwenye huruma katika mfano wa Mwana mpotevu! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, hata mwaka huu, Makanisa sehemu mbali mbali za dunia yataendelea kubaki wazi ili kutoa nafasi kwa waamini kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, kwa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao katika Sakramenti ya Upatanisho, ili kuonja kwa mara nyingine tena huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Mahakama ya huruma ya Mungu.

Ni muda wa kutafakari kuhusu Fumbo la Msalaba: Huruma ya Mungu
Ni muda wa kutafakari kuhusu Fumbo la Msalaba: Huruma ya Mungu   (Vatican Media)

Itakumbukwa kwamba, Majimbo na Parokia mbalimbali zimejenga Makanisa kwa ajili ya ajili ya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa muda wa masaa 24. Lengo ni kuendelea kukesha pamoja na Kristo Yesu kama sehemu ya mchakato wa majibu endelevu kutoka kwa waamini mintarafu swali la Kristo Yesu, Je, Simoni, umelala? Hukuweza kukesha saa moja? Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi ila mwili ni dhaifu! Rej. Mk. 14 37- 38. Yesu katika maisha na utume wake, alipenda kujitenga na malimwengu ili kuweza kufanya maamuzi mazito katika maisha yake. Alifunga na kusali kwa muda wa siku arobaini jangwani; akafunga na kusali kabla ya kuwachagua Mitume wake, akasali kiasi cha kutokwa matone ya damu alipokuwa anajiandaa kuadhimisha Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake.Kumbe, Mpango mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” ni muda muafaka hata kwa waamini kujitenga kidogo na malimwengu ili kutafakari kuhusu maisha na wito wao kwa: kusali, kuabudu, kuomba, kushukuru, kusifu na kutukuza na hatimaye, kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Haya, kimsingi ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka wa huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku kwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbalimbali!

Mpango Mkakati wa Saa 24 kwa Ajili ya Bwana: 28-29 Machi 2025
Mpango Mkakati wa Saa 24 kwa Ajili ya Bwana: 28-29 Machi 2025   (ANSA)

Huruma ya Mungu inapata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu, ufunuo halisi wa Uso wa huruma ambaye alisimika Ekaristi Takatifu kama ukumbusho wake wa milele na sadaka yake ya Pasaka. Ndiyo maana waamini wanaalikwa kumkazia tena na tena macho ya imani katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Ni muda muafaka wa kuabudu, kusali, kutafakari Neno la Mungu na hatimaye, kujipatanisha na Mungu. Ikumbukwe kwamba, Sakramenti ya Upatanisho ni mahali pa pekee sana ambamo huruma ya Mungu inaadhimishwa. Hapa waamini wanatakatifuzwa, tayari kwenda kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya mwanga na ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili. Mpango mkakati wa “Saa 24 kwa ajili ya Bwana” ni suala Mama katika maisha na utume wa Kanisa, kumbe, linapaswa kuvaliwa njuga ili liweze kuwa ni endelevu katika maisha na utume wa Kanisa. Mpango huu unaweza kumwilishwa katika kila Parokia, walau mara moja kwa mwezi ili kuleta roho ya kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani; roho na ari ya kutaka kukuza na kudumisha utume wa Sala na Biblia kwa kukesha na kusali. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya upendo, zawadi ya Kristo kwa waja wake; ni chakula cha maisha ya uzima wa milele na kwamba, hili ni Fumbo linalopaswa kutangazwa na kushuhudiwa, tayari kutoka kimasomaso kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa!

Saa 24 Kwa Ajili ya Bwana
28 Machi 2025, 16:13