Kung'ara Kwa Kristo Yesu Mbele ya Wafuasi Wake: Kielelezo Cha Upendo Usiokuwa na Kifani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka C wa Kanisa inasimulia jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyowachukua Mitume wake watatu yaani: Petro, Yakobo na Yohane wakajitenga na hapo akang’ara sura mbele, kiasi cha kuwafunulia ukuu, utukufu na utakatifu wake ambao walipaswa kuupokea kwa njia ya imani, mahubiri pamoja na miujiza mbalimbali aliyotenda katika maisha yake. Tukio la kung’ara kwa Yesu linasindikizwa na uwepo wa Musa na Eliya waliokuwa wanazungumza na Kristo Yesu, kielelezo cha utimilifu wa Sheria na Unabii katika Maandiko Matakatifu. Mwanga angavu uliokuwa kiini cha tukio hili ni kielelezo cha mwanga unaopaswa kuangaza akili na mioyo ya Mitume wa Kristo Yesu ili waweze kumfahamu Bwana wao. Ni mwanga unaoangaza Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu na hivyo, kufunua maisha na utume wake wote! Aliwachagua mitume watatu kati ya wale kumi na wawili ili: kuwaimarisha katika imani, matumani na mapendo thabiti mbele ya Kashfa ya Fumbo la Msalaba. Rej. Lk 9:28-36. Kristo Yesu alimchagua Petro, ili amwiimarishie imani, tayari kumtangaza na kumshuhudia mbele ya Mataifa kama kiongozi mkuu wa kwanza wa Kanisa la Kristo Yesu. Mtume Yohane alikuwa ni kati ya wale wanafunzi aliowapenda upeo, aliyekabidhiwa kumtunza Bikira Maria na yeye alikuwa ni Mtume wa mwisho kuitupa mkono dunia, baada ya kushuhudia vifo dini vya Mitume wengine, akabaki kuwa ni shuhuda wa huruma na upendo wa Kristo Yesu kwa walimwengu. Yakobo alikuwa ni Mtume wa kwanza kuyamimina maisha yake kama shuhuda wa tunu msingi za Kiinjili.
Kristo Yesu anadhihirisha utukufu kwa wafuasi wake, akiwaandaa kuweza kupokea vyema Fumbo la Msalaba, kwa imani, matumaini na mapendo makuu. Kristo Yesu anaufunua Umungu wake kwa njia ya mwili uliotukuka, ndiyo maana Kanisa linamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa utukufu kwani ukuu una Yeye milele hata na milele!Hili ni tukio la Ufunuo wa mwanga utakaozima giza la Kashfa ya Fumbo la Msalaba, tayari kutoa nafasi kwa binadamu kumwabudu, kumsifu, kumtukuza na kumwomba Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa, kuisikiliza sauti ya Mwenyezi Mungu na kutekeleza mapenzi yake katika uhalisia wa maisha yao, kwani Neno la Mungu ni dira na mwongozo wa maisha. Neno la Mungu ni Ufunuo wa utambulisho wa Mwana wa Mungu. Injili ya Marko inafikia kilele chake katika Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Utukufu wa Kristo unajionesha katika Fumbo la Ufufuko wake! Kiri ya imani ya yule akida aliyesema “Hakika mtu huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu” Mk. 15:39, kwa Mwinjili Marko, hiki ni kipeo cha hali ya juu kabisa cha Injili yake na kwa hakika Kristo Yesu ni “Mwana wa Mungu.” Mk 1:1. Waamini wanakumbushwa kwamba, Kristo Yesu anaendelea kujifunua kwa waja wake katika: Maandiko Matakatifu, Maisha ya Sala na Sakramenti za Kanisa na katika huduma ya Injili ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi; hii ni nuru ya upendo wake usiokuwa na kifani.
Baba Mtakatifu Francisko tangu tarehe 14 Februari 2025 amelazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma. Afya ya Baba Mtakatifu Francisko inaendelea kuimarika siku kwa siku na kwamba, anaendelea kupata tiba, kufanya mazoezi ya viungo na kupumua. Siku ya Baba Mtakatifu hospitalini hapo inanogeshwa na: tiba, sala, tafakari pamoja na kazi ndogo ndogo kwani anapaswa kutumia muda mrefu kwa ajili ya mapumziko. Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima, tarehe 16 Machi 2025 akiwa Hospitalini Gemelli akisema, Yesu kung’ara sura mbele ya wafuasi wake ni kudhihirisha ufunuo wa upendo wake usiokuwa na kifani. Anasema, yuko katika kipindi cha majaribu na kwamba, anaungana na wagonjwa wote sehemu mbalimbali za dunia, kuendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya imani, mapendo na matumaini thabiti. Baba Mtakatifu anawashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaoendelea kumwombea ili aweze kupona haraka na kwamba, yeye pia anaendelea kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa wakati huu anapokabiliana na changamoto ya afya anapenda kujiunga na wagonjwa wote mahali popote pale walipo na wale walio dhaifu kwani hakuna kitu chochote kile kinachoweza kuwazuia kupenda, kusali na kujisadaka kwa ajili ya wengine kama ishara ya matumaini katika imani. Hata leo hii, kuna nuru na mwanga angavu unaoangaza huduma ya upendo: hospilitani, kwenye Zahanati na Vituo vya Afya mahali ambapo huduma ya upendo na unyenyekevu hutekelezwa. Baba Mtakatifu anapenda kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana naye kumsifu Mwenyezi Mungu ambaye kamwe hawezi kuwaacha watumbukie katika upweke hasi, kwani nyakati za magumu na uchungu wa maisha, huwaweka watu kando yao; na kwamba, hawa ni watu wanaoakisi mionzi ya upendo wa Mungu usiokuwa na kifani.
Baba Mtakatifu anawashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanaoendelea kusali na kumwombea afya njema. Anatambua fika kwamba, kuna umati mkubwa wa watoto wanaomwombea afya njema na kwamba, kuna baadhi yao, Dominika tarehe 16 Machi 2025 wamekwenda kumtembelea Hospitalini Gemelli, kama ishara ya uwepo wao wa karibu hasa katika kipindi hiki anapokabiliana na changamoto za afya. Kwa hakika, Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwaambia kwamba, anawapenda sana kutoka katika sakafu ya moyo wake na kwamba, anasubiri fursa ya kuweza kukutana na watoto hawa! Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani, lakini zaidi katika nchi zile ambazo zimejeruhiwa kwa vita yaani: Palestina na Israeli, Lebanon, Mynmar, Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuliombea Kanisa linaloitwa kutafasiri na hatimaye, kumwilisha mang’amuzi yaliyofanywa katika Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yaliyonogeshwa na kauli mbiu: “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pamoja na mambo mengine: kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha adili na matakatifu. Baba Mtakatifu anaishukuru Sekretarieti kuu ya Sinodi kwa kuandaa mpango mkakati unaopaswa kutekeleza na Makanisa Mahalia katika kipindi cha Miaka mitatu kuanzia sasa. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko anawaweka waamini na watu wenye mapenzi mema, chini ya ulinzi na tunza za Bikira Maria, ili awasaidie kuwa ni vyombo na mashuhuda wa mwanga wa amani ya Kristo Yesu.