ÐÓMAPµ¼º½

Kuanzia Jumamosi, hadi Dominika tarehe 9 Machi 2025, Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kupata tiba, kufanya mazoezi ya viungo, kusali, kutafakari pamoja na kufanya kazi ndogo ndogo. Kuanzia Jumamosi, hadi Dominika tarehe 9 Machi 2025, Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kupata tiba, kufanya mazoezi ya viungo, kusali, kutafakari pamoja na kufanya kazi ndogo ndogo.  (ANSA)

Hali ya Afya ya Baba Mtakatifu Francisko Hospitalini Gemelli, Mjini Roma!

Baba Mtakatifu Francisko katika Tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 9 Machi 2025, anasema, wakati huu anapoendelea kulazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025; kwa hakika anaonja: umakini wa huduma na huruma kutoka kwa madaktari na wafanyakazi katika sekta ya afya. Baba Mtakatifu anaendelea na tiba, sala pamoja na kazi ndogo ndogo hospitalini hapo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kristo Yesu anawaalika wafuasi wake kuwa ni Wasamaria wema kwa kuwekeza katika huduma ya tiba, ili kuokoa maisha ya watu, kielelezo cha upendo wa Mungu, ambaye kimsingi ni chanzo, maana na hatima ya maisha ya binadamu. Wajibu wa kimaadili, ukiongozwa na imani, uwasaidie watu kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, chanzo cha uhai. Kifo ni sehemu ya maisha ya mwanadamu na wanasayansi wanapaswa kutambua ukweli huu. Daima mgonjwa apewe tiba hata wale wenye magonjwa sugu na ya muda mrefu. Hii ni huduma ya tiba: kimwili, kisaikoljia, kijamii, kifamilia na katika maisha ya kiroho, kwa kuzingatia taalimungu ya maisha ya mwanadamu. Wadau mbalimbali wamsaidie mgonjwa kujiandaa kufa kifo chema, akiwa anasindikizwa na neema ya utakaso na upendo wa Mungu. Pale ambapo imani na matumaini vinakosekana wakati mgonjwa anapokaribia kifo kuna hatari ya kutumbukia katika kifolaini au msaada wa kutaka kujinyonga. Mang’amuzi ya maisha mintarafu mateso ya Kristo Yesu sanjari na kutangaza Injili ya matumaini kwa watu wanaoteseka kimwili, kisaikolojia, kimaadili na kiroho. Mama Kanisa anawaalika watoto wake kumwangalia Kristo Yesu aliyeteswa na kufa Msalabani. Wagonjwa katika mateso yao, wanaonja pia upweke hasi, hali ya kukataliwa pamoja na kuteswa kutokana na maumivu, kiasi cha kudhani kwamba, hawana tena thamani wala ubora wowote kiasi kwamba, wamegeuka kuwa ni mzigo mzito usioweza kubebeka tena. Msalaba wa Kristo Yesu uwe ni tumaini kwa wale wote wanaoteseka: kimwili, kisaikolojia, kimaadili na kiroho. Wasindikizwe kwa uwepo, sala na maombezi ya Bikira Maria aliyethubutu kusimama chini ya Msalaba wa Kristo Yesu, akatiwa shime na upendo wa Baba wa milele. Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kuwaacha waja wake katika upweke!

Afya ya Baba Mtakatifu Francisko inaendelea kuimarika
Afya ya Baba Mtakatifu Francisko inaendelea kuimarika   (ANSA)

Baada ya mateso na kifo cha Msalaba, kuna ufufuko na uzima wa milele, kielelezo cha imani ya Kanisa na upendo wa Mungu Baba. Huduma shufaa haziwezi kufua dafu, ikiwa kama mgonjwa ametumbukia katika kishawishi na hali ya kujikatia tamaa, mwaliko ni kuendelea kuandamana na Kristo Yesu Msalabani. Wale wote wanaomhudumia mgonjwa wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini, tayari kutangaza na kushuhudia upendo wa Kristo Yesu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba. Hii ndiyo maana ya maisha ambayo Fumbo la kifo, kamwe haliwezi kuiondoa.Moyo wa Msamaria Mwema Unaoona: Hii ni huduma inayofumbatwa katika huruma na upendo kwa kutambua na kuheshimu Injili ya uhai kwani maisha ni matakatifu na ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Utambuzi huu unaweza kufanywa kwa akili ya kawaida. Ni katika muktadha huu, Mama Kanisa anapenda kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema na waamini wa dini mbalimbali duniani ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu tangu pale anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Maisha, utu na heshima ya binadamu ni kielelezo cha Fumbo la Utatu Mtakatifu. Maisha daima ni mazuri. Kumbe, huu ni mwaliko kwa watu wote kuheshimu na kuthamini utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mwenyezi Mungu ni chanzo na hatima ya maisha ya mwanadamu anayepaswa kuwajibika mbele yake. Thamani na utakatifu wa maisha ya binadamu yanaongozwa na kanuni maadili na sheria zote. Ni kinyume cha kanuni maadili na utu wema, kukatisha maisha ya mgonjwa hata kama mgonjwa mwenyewe ameonesha nia hii kwa uhuru kamili. Mwenyezi Mungu ndiye mwenye mamlaka halali ya kuondoa uhai wa binadamu. Ni kutokana na muktadha huu, utoaji mimba, kifolaini na tamaa ya mtu kutaka kujinyonga au kutoa sumu kwa jumuiya ni matendo yanayokwenda kinyume cha utashi wa Mwenyezi Mungu kwa binadamu.

Mahujaji wa Injili ya Matumaini wanamwombea Papa Francisko
Mahujaji wa Injili ya Matumaini wanamwombea Papa Francisko   (Vatican Media)

Taarifa rasmi kutoka kwa Dr. Matteo Bruno, Msemaji mkuu wa Vatican inaonesha kwamba, hali ya afya ya Baba Mtakatifu Francisko inaendelea kuimarika zaidi kwa kupumua kama kawaida pamoja na kuendelea na mazoezi ya kupumua kwa viungo bila mashine. Kuanzia Jumamosi, hadi Dominika tarehe 9 Machi 2025, Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kupata tiba, kufanya mazoezi ya viungo, kusali, kutafakari pamoja na kufanya kazi ndogo ndogo pamoja na kujipatia mapumziko marefu. Baba Mtakatifu Francisko katika Tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 9 Machi 2025, anasema, wakati huu anapoendelea kulazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025; kwa hakika anaonja: umakini wa huduma na huruma kutoka kwa madaktari na wafanyakazi katika sekta ya afya. Baba Mtakatifu anawashukuru kutoka katika sakafu ya moyo wake wote na anawakumbuka wote wanaowahudumia wagonjwa sehemu mbalimbali za dunia, kama ishara ya uwepo na ukaribu wa Mungu kwa waja wake na kwamba, binadamu katika udhaifu wake anahitaji kuonjeshwa “Muujiza wa huruma ya Mungu, unaowaambata na kuwashindikiza wale wote walioko kwenye majaribu na kuwakirimia mwanga mdogo katika usiku mnene wa maumivu. Baba Mtakatifu anawashukuru kwa dhati kabisa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanaoendelea kumwonesha uwepo wao wa karibu kwa njia ya Sala na Sadaka zao na kwamba, yeye pia anawakumbuka na kuwaombea. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea zawadi ya amani duniani, lakini zaidi, huko Ukraine, Palestina, Israeli na Lebanon; Mnyamar, Sudan pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC. Wote hawa wamewekwa na Baba Mtakatifu Francisko nchini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Na habari zaidi zinasema, Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican akiwa ameambatana na Askofu mkuu Edga Pena Parra, Dominika tarehe 9 Machi 2025 wamemtembelea Baba Mtakatifu Francisko hospitalini Gemelli, ili kumtakia hali na kumtaarifu kwa ufupi hali ya maisha na utume wa Kanisa kwa wakati huu.

Hali ya Afya ya Papa Francisko
09 Machi 2025, 15:08