Papa alilala salama na amepokea Ujumbe wa ukaribu na upendo kwa kulazwa hospitalini Gemelli
Vatican News
Kutoka kwa Msemaji wa Vyombo vya habari vya Vatican Dk. Matteo Bruni, akikutana na waadishi wa habari tarehe 15 Februari 2025, alitoa taarifa kuhusu Papa. Kwa mujibu wake alisema kuwa: “ Papa alilala salama usiku na kusinzia vizuri, katika usiku mzuri wa usingizi. Na Asubuhi amepata kifungua kinywa na kusoma baadhi ya habari za kila siku. Tiba inaendelea, kama vile kuchukuliwa vipimo. Taarifa za matibabu zitakuwa, pengine baada ya saa kumi na moja jioni. Na homa haijapanda (asubuhi hii hakuwa na homa).”
Habari za kuugua Papa zimeenea ulimwenguni
Habari za kulazwa kwa Papa Francisko katika hospitali ya Agostino Gemelli jijini Roma, kutokana na ugonjwa wa mkamba(Bronchitis), zimeenea Ulimwenguni kote. Ujumbe wa ukaribu umefika kutoka pande nyingi, hasa kutoka Makanisa mbali mbali, lakini pia kutoka kwa waamini wengi wenye mapenzi mema ambao katika mitandao ya kijamii, wanatoa maoni yao kuhusu habari hizo, na ambao wameonesha mapendo yao hasa kumuombea Papa.
Maombi kwa ajili ya Papa
Kutoka Jimbo la Roma katika maombi: “Jumuiya ya jimbo la Roma inaeleza ukaribu wake kwa Baba Mtakatifu, baada ya kupata habari za kulazwa kwake katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli. Watu wote wa Mungu walioko Roma wanakusanyika karibu zaidi na Askofu wao katika wakati huu, wakimhakikishia maombi yao ya kupona haraka." Na Baraza la Maaskofu wa Italia(CEI),liko kwenye ukurasa huohuo kwamba: “Tunamtakia matashi mema Baba Mtakatifu apone haraka, huku tukiungana katika sala kwa ajili yake.”
Wakati huohuo, Kutoka katika Basilika ya Mtakatifu Petro mjini Vatican, asubuhi tarehe 15 Februaria 2025, mahujaji wapatao elfu tano, waliofika Roma kwa ajili ya kushiriki Katekesi ya Jubilei iliyokatishwa baadaye, walisali kwa ajili ya afya ya Baba Mtakatifu Francisko “anayefanya mengi kwa ajili ya Kanisa,” alisema hayo Padre Enzo Fortunato, Rais wa Kamati ya Kipapa ya Siku ya Mtoto Duniani ambaye alifanya katekesi kwa waamini ambao baadhi yao walitoka majimbo ya Parma, Benevento na Viterbo.
Ujumbe wa CELAM
Na kwa upande wa Urais wa Baraza la Maaskofu wa Amerika ya Kusini,(CELAM) wakiongozwa na Kardinali Jaime Spengler, Askofu Mkuu wa Porto Alegre, aliandika barua inayoonesha ukaribu na Papa "katika nyakati hizi ambazo Bwana alitaka kumuunganisha kwa karibu zaidi na msalaba wa udhaifu wa binadamu." Ujumbe huo unasomeka kwamba: "Tumehakikishiwa kwamba anapokea uangalizi wa kutosha na tunaamini kwamba atapona hivi karibuni.” Maaskofu waliongeza wakimwambia Papa: "Maombi ya waamini wengi ni dhihirisho kwamba wewe uko mioyoni mwetu kama Baba na Mchungaji. Na tumwombee, ili apate kuhisi nguvu na faraja ya Bwana, na kwamba ampe saburi nyingi." Hatimaye, tunakukabidhi kwa ulinzi wa kimama wa Mama Yetu wa Guadalupe, Msimamizi wa Bara la Amerika ya Kusini.
Hata hivyo Ijimaa tarehe 14 Februari 2025, jioni taarifa ilitolewa kutoka kwa Msemaji wa Vyombo vya habari vya Vatican ambapo ilitangaza kwamba "Papa alifanyiwa vipimo vya kitaalam na kuanza matibabu ya dawa hospitalini." Msemaji Mkuu huyo Dk. Matteo Bruni kisha aliwaambia waandishi wa habari kwamba "ungalizi wa Papa ni wa haki, licha ya kuwa na homa kidogo, lakini yuko mtulivu na ana roho tulivu na amesoma baadhi ya magazeti."
Imesasishwa saa 7:05 mchana.