MAP

Ujumbe wa Kwaresima 2025:Tutembee Pamoja kwa matumaini Ujumbe wa Kwaresima 2025:Tutembee Pamoja kwa matumaini 

Ujumbe wa Papa Francisko wa Kwaresima 2025:Tutembee Pamoja kwa matumaini

Katika Ujumbe wa Papa wa Kwaresima 2025 wa:“Tutembee pamoja kwa matumaini,"anawataka waamini kusindikiza,kuwasaidia na kuwakaribisha kaka na dada katika hali ya taabu na vurugu katika safari ya pamoja kuelekea nyumba ya Baba.Kutembea katika maisha bega kwa bega bila kukanyaga au kumlemea mwingine,bila kuruhusu mtu yeyote kurudi nyuma au kujisikia kutengwa.Papa anatutaka tukabili hali halisi ya wengine,tuwe wafumaji wa umoja katika safari hii ya matumaini.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumanne tarehe 25 Februari 2025 ametoa Ujumbe wa Kwaresima kwa mwaka 2025. Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka huu kitaanza Jumatano ya Majivu tarehe 5 Machi 2025. Katika ujumbe huo, unaongozwa na kauli mbiu: “Tutembee pamoja kwa matumaini,” Papa anajikita kufafanua vipengele vitatu: Kutembea kama mahujaji wa matumaini kulekea Nchi ya Ahadi. Pili kusafari pamoja ni kuwa wa kisinodi na ndiyo wito wa kila Kanisa ili kutomwacha mtu yeyote nyuma au kutengwa. Tatu, tunatembea njia hii pamoja kwa matumaini ya ahadi ambapoTumaini lisilokatisha tamaa (rej. Rm 5:5),ndiyo ujumbe mkuu wa Jubilei kuu ya Mwaka Mtakatifu 2025 kwamba uwe kwetu upeo wa safari ya Kwaresima kuelekea ushindi wa Pasaka. Ndugu msikilizaji na msomaji tunachapisha ujumbe kamili wa Papa Francisko wa Kwaresima 2025: 

Kaka na dada, kwa ishra hii ya toba ya majivu, juu ya kichwa ni mwanzo wa hija ya kila mwaka ya Kwaresima Takatifu, katika imani na katika matumaini. Kanisa, mama na mwalimu, anatualika kuandaa mioyo yetu na kujifungulia katika neema ya Mungu ili kuweza kuadhimisha kwa furaha kubwa ushindi wa Pasaka ya Kristo, Bwana, juu ya dhambi na juu ya kifo kama Mtakatifu Paulo alivyosema: "Kifo kimemezwa kwa ushindi. U wapi, Ewe mauti, ushindi wako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako?(1Kor 15,54-55 ). Kiukweli, Yesu Kristo, aliyekufa na kufufuka ni kitovu cha imani yetu na ni uhakika wa matumaini yetu  katika ahadi kubwa ya Baba ambaye tayari alihitimisha katika Yeye, Mwanae mpendwa: Maisha ya milele (rej. Yh10,28; 17,3). Katika kwaresima, inayojitajirisha na neema ya Mwaka wa Jubilei(2025), ninapenda kuwapa baadhi ya tafakari kuhusu nini maana ya “kutembea pamoja katika matumaini na kugundua miito ya uongofu ambao huruma ya Mungu, inatuelekea sisi sote kama watu na kama jumuiya.

Kwanza kabisa kutembea. Kauli mbiu ya Jublei: Mahujaji wa Matumaini inatufanya tufikiri safari ndefu ya watu wa Israeli kuelekea Nchi ya ahadi iliyosimuliwa katika Kitabu cha Kutoka: Ni vigumu kutambea katika utumwa kufikia uhuru, uliopendwa na kuongozwa na Bwana, ambaye anapenda watu wake na daima ni mwaminifu kwao. Na hatuwezi kukumbuka Kutoka katika Biblia bila kufikiria kaka na dada zetu wengi ambao wanakimbia hali za shida na  vurugu na wanakwenda kutafuta maisha bora kwa ajili yao na kwa ajili ya wapendwa wao. Katika ili linaibua wito wa kwanza wa uongofu, kwa sababu sisi sote ni mahujaji katika maisha, lakini kila mmoja anaweza kujiuliza: je ni jinsi gani ninajiachia kuguswa na hali hii? Je, kweli niko njiani au tuseme nimepooza, tuli, ninaogopa na sina tumaini, au nimekwama katika eneo langu la faraja?(Confort zone). Ninatafuta njia za kujikomboa katika hali hizi za dhambi na za ukosefu wa hadhi? Ingekuwa mazoezi mazuri ya kwaresima kukabiliana na hali halisi kwa mmojawapo wa wahiaji au Mhujaji na kujiachia kuguswa, kwa namna ya kugundua ni kitu gani Mungu anatuomba ili kuwa wasafiri wema kuelekea nyumba ya Baba. Huu “ndiyo mtihani mwema kwa wasafiri.”

Tafakari ya pili, tufanye safari hiyo pamoja. Kutembea pamoja, kuwa wa kisinodi, ndiyo wito wa kila Kanisa. Wakristo wanaitwa kutembea pamoja katika njia, kamwe wasiwe wasafiri peke yao. Roho Mtakatifu anatusukuma kuondoka ndani mwetu  binafsi ili kwenda kuelekea kwa Mungu na kuelekea kwa ndugu, na kamwe tusijifungie ndani mwetu binafsi. Kutembea pamoja maana yake ni kuwa wafumaji wa umoja, kuanzia na hadhi ya pamoja ya kuwa wana wa Mungu (Gal 3,26-28); Inamaanisha kuendelea bega kwa bega, bila kumkanyaga au kumlemea mwingine, bila kutunza husuda au unafiki, bila kuruhusu mtu yeyote kuachwa nyuma au kuhisi kutengwa. Twende katika mwelekeo uleule, kuelekea lengo moja, tukisikilizana kwa upendo na subira. Katika Kwaresima hii, Mungu anatutaka tuhakikishe kama katika maisha yetu, katika familia zetu, mahali tunapofanya kazi, katika parokia au jumuiya za kitawa, tuna uwezo wa kutembea na wengine, wa kusikiliza, wa kushinda jaribu la kurudi nyuma katika kujirejea kibinafsi na kujali mahitaji yetu wenyewe tu. Hebu tujiulize mbele za Bwana ikiwa tunaweza kufanya kazi pamoja kama maaskofu, mapadre, watu waliowekwa wakfu na walei, katika huduma ya Ufalme wa Mungu; ikiwa tuna tabia ya kukaribisha, kwa ishara thabiti, kuelekea wale wanaokuja karibu nasi na kwa wale walio mbali; ikiwa tunawafanya watu wajisikie kuwa sehemu ya jumuiya au kuwaweka pembeni. Huu ndiyo wito pili wa “uongofu wa kisinodi.”

Tatu, tunatembea njia hii pamoja kwa matumaini ya ahadi. Tumaini lisilokatisha tamaa (rej. Rm 5:5), ujumbe mkuu wa Jubilei, uwe kwetu upeo wa safari ya Kwaresima kuelekea ushindi wa Pasaka. Kama vile Papa Benedikto XVI alivyotufundisha katika Waraka wa Spe Salvi, “wanadamu wanahitaji upendo usio na masharti.” Anahitaji uhakika huo unaomfanya aseme: “Wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu” (Rm 8:38-39). Yesu, upendo wetu na tumaini letu, amefufuka na anaishi na kutawala kwa utukufu. Kifo kimegeuzwa kuwa ushindi na hapa ndipo penye imani na tumaini kuu la Wakristo: katika ufufuko wa Kristo! Huu hapa ni mwito wa tatu wa kuongoka: ule wa tumaini, wa kumtumaini Mungu na katika ahadi yake kuu, uzima wa milele. Ni lazima tujiulize: Je, nina hakika kwamba Mungu husamehe dhambi zangu? Au ninafanya kana kwamba ninaweza kujiokoa? Je, ninatamani wokovu na kuomba msaada wa Mungu ili kuupokea? Je, ninaishi kwa uthabiti tumaini ambalo hunisaidia kusoma matukio ya historia na kunisukuma kujitolea kwa haki, kwa udugu, kwa utunzaji wa nyumba yetu ya kawaida, nikihakikisha kwamba hakuna mtu anayeachwa nyuma?

Dada na kaka, shukrani kwa upendo wa Mungu katika Yesu Kristo, tunalindwa katika tumaini lisilokatisha tamaa (Rej. Rm 5:5). Tumaini ni "nanga ya nafsi", hakika na imara. Ndani yake Kanisa linasali kwamba “watu wote waokolewe” (1 Tim 2:4) na kungoja kuwa katika utukufu wa mbinguni kuunganishwa na Kristo, mwenzi wake. Hivi ndivyo Mtakatifu Teresa wa Yesu alivyojieleza: “Tumaini, nafsi yangu, tumaini. Hujui siku wala saa. Kesha kwa kufikiri kuwa kila kitu kinapita kwa haraka, ingawa kutokuwa na subira kwako kunaweza kufanya kile ambacho hakika kitakosekana, na kwa muda mfupi sana" (Mshangao wa roho kwa Mungu, 15, 3). Bikira Maria, Mama wa Tumaini, atuombee na atusindikize katika safari yetu ya Kwaresima.

Ujumbe ulitiwa saini: Roma, Mtakatifu Yohane huko Laterano, tarehe 6 Februari 2025, katika Kumbukizi ya Watakatifu Paulo Miki na wenzake, mashahidi.

Francisko.

Ujumbe wa Papa wa Kwaresima 2025
25 Februari 2025, 12:42