Sala Kwa Ajili ya Kumwombea Baba Mtakatifu Francisko Wakati Huu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa mkamba (Bronchitis) uliopelekea kulazwa tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli. Hali ya afya ya Baba Mtakatifu Francisko inaendelea kuimarika, lakini bado inabaki kuwa ni tete chini ya uangalizi maalum wa jopo la madaktari wanaomtibu. Usiku wa kuamkia Jumatatu tarehe 24 Februari 2025, Baba Mtakatifu amelala vyema na kwamba kwa sasa anaendelea na mapumziko. Changamoto ya kupumua bado inaendelea na kwamba, anatumia mipira kupumlia. Damu aliyoongezewa inaendelea kuonesha kwamba, seli nyekundu zinaendelea kuongezeka na kwamba, kwa sasa limeibuka tatizo jingine la figo kuanza kushindwa kufanya kazi kwa asilimia ndogo, hali ambayo hadi sasa imedhibitiwa kwa kutumia dawa. Baba Mtakatifu anaendelea kujitambua na kwamba, Dominika ya Saba ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa, tarehe 23 Februari 2025, Baba Mtakatifu ameshiriki Ibada ya Misa takatifu, iliyoadhimishwa kwenye Ghorofa ya 10 Kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli; Ibada ambayo wameshiriki pia wale wanaomtunza Baba Mtakatifu Francisko hospitalini hapo.
Kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaopenda kusali na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko wakati huu anapoendelea kukabiliwa na changamoto ya afya, wanaweza kuadhimisha Ibada ya Misa kwa ajili ya Baba Mtakatifu “Ad Diversa” inayopatikana kwenye Misale ya Kiroma. Waamini pia wanaweza kusali Sala ya Kanisa kwa kuongeza maombi yafuatayo: Mungu Baba asili ya maisha, tunakuomba, uwe faraja kwa Baba Mtakatifu Francisko: Umjalie nafuu ya kiroho na kimwili! Tuombe!
Ee Baba Mwema, wewe unayehifadhi moyoni mwako maisha ya watoto wako, mwangalie kwa macho ya huruma na mapendo, Mtumishi wako Baba Mtakatifu Francisko, ili upende kumwimarishia afya, ili aweze kuendelea kutekeleza utume na huduma yake kwa Kanisa lako. Tuombe.
Kwa ajili ya Baba Mtakatifu Francisko, aendelee kuonja uwepo angavu wa kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; mshikamano wa upendo na ukaribu kutoka katika Jumuiya ya Kikristo. Tuombe.
Ukombozi wa waamini na kimbilio la wale wanaoteseka, Ee Mungu Baba Mwenyezi upende kumfariji Baba Mtakatifu Francisko, ili kwamba, kwa njia ya msaada wako wenye huruma, aweze kupata faraja katika mateso na mahangaiko yake ya ugonjwa. Tuombe!
Na Habari zaidi kutoka Vatican zinasema kwamba, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatatu tarehe 24 Februari 2025 kwa kushirikiana na Makardinali wanaoishi mjini Roma pamoja na wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican watakusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko anayepambana na changamoto ya afya kwa wakati huu. Huu ni utekelezaji wa ombi lililotolewa na watu wa Mungu, ili kumkumbuka na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kupona na kurejea tena katika maisha na utume wake.