Papa Francisko:vita vya Ukraine ni uchungu na aibu ya ubinadamu
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko aliyelazwa katika hospitali ya Gemelli tangu tarehe 14 Februari, aliwasilisha Ujumbe wake wa Sala Malaika wa Bwana Dominika tarehe 23 Februari 2025 uliotangazwa na Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Vatican. Katika maandishi yakePapa anabainisha kuwa: Kaka na dada, Dominika njema. “Asubuhi ya leo katika Basilika ya Mtakatifu Petro, imeadhimisha Misa Takatifu kwa ajili ya kuwawekwa wakfu baadhi ya wakandidati wa wakishemasi. Ninawasalimia wao na washiriki wa Jubilei ya Mashemasi ambao kwa siku hizi wamekuwa Vatican; Ninashukuru Mabaraza ya Kipapa kwa ajili ya Makleri na kwa ajili ya Unjilishaji kwa maandalizi ya tukio hilo.”
Msiogope kuhatarisha upendo
Papa akiwageukia mashemasi hao anaeleza kuwa: “Ndugu wapendwa mashemasi, ninyi mnajikita katika kutangaza Neno na katika huduma na huruma ya Mungu kwa wote. Ninawahimiza muendelee kwa furaha utume wenu na kama inavyotushauri Injili ya leo, ya kuwa ishara ya upendo ambao unawakumbatia wote, unaobadilisha ubaya kwa wema na kuzaa Ulimwengu wa kidugu. Msiogope kuhatarisha upendo!”
Shukrani kwa huduma huko Gemelli
Akifafanua kuhusu afya yake, Papa anabainisha “Kwa upande wangu, ninaendelea kwa imani kulazwa katika Hospitali ya Gemelli, kwa kupeleka mbele matibabu ya lazima; na hata kupumziko ni sehemu ya matibabu! Ninawashukuru kwa moyo madaktari na wafanyakazi wa afya, wa Hospitali hii kwa umakini ambao wananionesha na kwa kujikita na huduma zao kati ya watu wagonjwa.”
Miaka mitatu ya vita Ukraine
Baba Mtakatifu Francisko akirejea juu ya kumbukizi ya vita vya Ukraine na Urusi vilivyoibuka tangu tarehe 24 Februari, alibainisha: "Miaka mitatu ya vita inatimia kesho(Jumatatu 24 Februari) iliyowakumba ukraine. Ni Siku ya uchungu na aibu kwa ubinadamu mzima! Wakati ninasasisha ukaribu wangu kwa watu walioteseka huko Ukraine, ninawaalika kukumbuka waathirika wa migogoro yote ya kisilaha na kusali kwa ajili ya zawadi ya amani nchini Palestina, nchini Israel na Mashairiki ya Kati, huko Myanmar, Kivu na Sudan.”
Shukrani kwa maombi na ujumbe aliopokea Papa
Baba Mtakatifu aidha akifikiria maombi kutokana na kulazwa kwake hospitalini amebainisha: “Katika siku hizi zimenifikia jumbe nyingi za upendo na zimenishangaza kwa namna ya pekee barua na michoro ya watoto. Ninawashukuru kwa ukaribu huu na kwa sala za kunitia nguvu ambazo nimezipokea kutoka Ulimwenguni kote! Ninawakabidhi nyote kwa maombezi ya Maria na kuwaomba kusali kwa ajili yangu.”