Papa asalimia wanahija waliofika ukumbi wa Paulo VI na katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro
Na Angella Rwezaula - Vatican
Baada ya katekesi yake, tarehe 1 Februari 2025 , akiwageukia waamini na mahujaji waliofika katika Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican Papa Francisko aliwajulisha “kuwasalimia hata washiriki wa Katekesi ya Jubilei waliokuwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakifuatilia. Papa alisema kuwa Hawa ni mahujaji kutoka Jimbo Katoliki la Sulmona-Valva) Italia ambapo baadaye alikwenda hata Kanisa Kuu na kuwasalimia huku akiwashukuru uwepo wao na kuwapa baraka zake. Lakini hata hivyo aliomba wasali sala ya Baba Yetu kabla ya kuwazungukia wote.
Papa hakuishia hapo bali aliongeza: “Mawazo yangu sasa yanakwenda kwenye hija ya Jimbo la Sulmona-Valva, pamoja na Askofu Michele Fusco, na kwa waseminari wa Bergamo. Wapendwa kaka na dada, ninawahimiza kuelewa na kukaribisha zaidi upendo wa Mungu, chanzo na sababu ya furaha yetu ya kweli. Pia ninawasalimu Waseminari wa Bergamo na kuwahimiza daima kumweka Yesu katikati ya maisha yao. Baraka yangu kwa kila mtu!”