MAP

2025.02.19.Kitabu cha Austen Ivereigh "Kuwa mali ya Mungu kwanza: Mafungo ya Kiroho ya Papa Francisko (LEV/Paulinus). 2025.02.19.Kitabu cha Austen Ivereigh "Kuwa mali ya Mungu kwanza: Mafungo ya Kiroho ya Papa Francisko (LEV/Paulinus). 

Mafungo ya Kiroho yenye Tafakari ya Papa Francisko

Toleo la Kiitaliano la kitabu cha Austen Ivereigh:Kuwa Mali ya Mungu kwanza:Mafungo ya kiroho na Papa Francisko”kilichochapishwa kwa pamoja na Duka la Vitabu la Vatican LEV na Paulinus,kimetolewa Jumatatu tarehe 24 Februari 2025.

Vatican News

Maandishi ya kufanya mafungo ya kiroho, kibinafsi na kama Jumuiya, yakiambatana na tafakari ya Jorge Mario Bergoglio na kulingana na Mafungo ya kiroho ya Mtakatifu Ignatius wa Loyola.  Ni kitabu cha Austen Ivereigh kiitwacho Kuwa Mali ya Mungu kwanza: Mafungo ya Kiroho na Papa Francisko”, kilichochapishwa kwa pamoja na Duka la Vitabu la Vatican na Paulinus, katika maduka ya vitabu kuanzia Jumatatu tarehe 24 Februari 2025. Kitabu hicho kilichapishwa  katika Kiingereza mwaka 2024  chenye kichwa kilichotajwa hapo awali na (Messenger Publications - Loyola Press), kikiwa na dibaji ya Papa Francisko ambapo anaeleza umuhimu wa mafungo ya kiroho kwa safari ya imani ya kila Mkristo. Hapa chini tunachapisha maandishi kamili ya dibaji ya Papa.

Papa Francisko

Kwa sababu ya uzoefu wake wa maisha, Mtakatifu Ignatius wa Loyola alielewa kwa uwazi sana kwamba kila Mkristo anahusika katika vita vinavyofafanua maisha yake. Ni pambano la kushinda jaribu la kujifunga wenyewe, ili upendo wa Baba uweze kukaa ndani yetu. Tunapomtengenezea nafasi Bwana ambaye anatuokoa kutokana na utoshelevu wetu, tunajifungua kwa viumbe vyote na kwa kila kiumbe. Tunakuwa njia za maisha na upendo wa Baba. Hapo ndipo tunapotambua maisha ni nini hasa: zawadi kutoka kwa Baba, ambaye anatupenda sana na anataka tuwe mali yake na ya kila mmoja wetu.

Vita hivi tayari vimeshashinda kwa ajili yetu na Yesu: kwa kifo chake cha aibu msalabani na kufufuka kwake. Kwa hivyo Baba amefunua, kwa uhakika na milele, kwamba upendo wake una nguvu zaidi kuliko nguvu zote za ulimwengu huu. Na bado kukaribisha na kuufanya ushindi huu kuwa halisi kunaendelea kuwa mapambano: tunaendelea kujaribiwa kujifungia kutoka katika neema, kuishi katika njia ya kidunia, chini ya udanganyifu wa kuwa na uhuru na kujitegemea.

Migogoro yote ya kuhatarisha maisha ambayo inatusumbua ulimwenguni, kutoka kwa shida ya kiikolojia hadi vita, hadi ukosefu wa haki kwa maskini na walio hatarini, yanatokana na kukataa huku kuwa mali ya Mungu na ya kila mmoja wetu. Kanisa linatusaidia kwa njia nyingi kupambana na jaribu hili. Mapokeo na mafundisho yake, mazoea ya sala na maungamo, na adhimisho la kawaida la Ekaristi ni “njia za neema” ambazo hutufungua ili kupokea zawadi ambazo Baba anataka kumimimina juu yetu.

Miongoni mwa tamaduni hiyo ni mafungo ya kiroho, na kati ya hiyo ya mwisho, Mafungo ya  Kiroho ya Mtakatifu Ignatius wa Loyola.  Kwa sababu ya shinikizo na matatizo ya jamii yenye ushindani wa kupindukia, kurejea kuchaji  upya betri zako zimekuwa maarufu zaidi. Lakini mafungo ya Kikristo ni tofauti sana na likizo ya ‘uzuri’. Kiini cha umakini sio sisi, lakini Mungu, Mchungaji Mwema, ambaye, badala ya kututendea kama mashine, anajibu mahitaji yetu ya kina kama watoto wapendwa. Mafungo ni wakati ambapo Muumba anazungumza moja kwa moja na viumbe vyake, akizitia moto roho zetu "katika upendo na sifa zake," ili tuweze "kumtumikia vyema zaidi wakati ujao," kama Mtakatifu Ignatius asemavyo (Mafungo ya Kiroho 15).

Upendo na huduma: hizi ni mada kuu mbili za Mafungo ya Kiroho. Yesu anakuja kukutana nasi, akivunja minyororo yetu ili tuweze kutembea pamoja naye kama wanafunzi na waandamani wake.

Ninapofikiria matunda ya Mafungo ya ninamwona Yesu akimwambia yule aliyepooza kwenye bwawa la Bethzatha: “Simama, chukua machela yako na utembee!” (Yoh 5:8 ). Ni agizo ambalo lazima kulitii na, wakati huo huo, mwaliko wake mtamu na wa upendo zaidi. Mtu huyo alikuwa amepooza ndani. Alijiona kuwa hafai katika ulimwengu wa wapinzani na washindani. Akiwa amejaa chuki na uchungu kwa kile alichohisi amenyimwa, alinaswa katika mantiki ya kujitosheleza, akiamini kwamba kila kitu kinategemea yeye na nguvu zake pekee.

Na kwa kuwa wale wengine walikuwa na nguvu na kasi zaidi kuliko yeye, alikuwa amekata tamaa. Lakini ni pale ambapo Yesu anakuja kukutana naye kwa huruma yake na kumwalika atoke ndani yake mwenyewe. Mara tu anapojifungua kwa nguvu za uponyaji za Yesu, kupooza kwake, kwa ndani na nje, kunaponywa. Ana uwezo wa kuamka na kutembea, akimsifu Mungu na kufanya kazi kwa ajili ya Ufalme Wake, akiwa huru kutokana na hekaheka ya kujitosheleza na kujifunza zaidi na zaidi kila siku kutegemea neema yake. Kwa njia hii, mwanadamu anakuwa mfuasi mwenye uwezo wa kukabiliana vyema na si tu changamoto za ulimwengu huu, bali pia kutoa changamoto kwa ulimwengu kufanya kazi kulingana na mantiki ya zawadi na upendo.

Kama Papa, nilitaka kutia moyo “kuwa mali ya Mungu kwanza,” na kisha kwa uumbaji na kwa ndugu zetu, hasa kwa wale wanaotuita kwa sauti kubwa. Hii ndiyo sababu nilitaka kukumbuka mikasa  miwili mikuu ya wakati wetu: kuzorota kwa makazi yetu ya kawaida na uhamiaji na harakati za watu wengi.  Zote mbili ni ishara za "mgogoro wa kutokuwa wa mali" iliyoelezewa katika kurasa hizi. Kwa sababu hiyohiyo nilitaka kulitia moyo Kanisa ligundue tena karama ya mapokeo yake yenyewe ya sinodi, kwa sababu linapojifungua kwa Roho anenaye ndani ya watu wa Mungu, Kanisa zima huinuka na kutembea, likimsifu Mungu na kusaidia kuleta Ufalme wake.

Ninafurahi kuona jinsi ambavyo mada hizi zinavyopatikana katika “kuwa mali ya Mungu kwanza,” zinazohusishwa na tafakari za Mtakatifu Ignatius ambazo zimenifunda kwa miaka mingi. Austen Ivereigh alifanya huduma nzuri kwa kuunganisha tafakari za mafungo nilizohubiri miongo mingi iliyopita na mafundisho yangu kama papa. Kwa njia hii, inaruhusu wote kuangaziwa na Mafungo ya Kiroho ya Mtakatifu Ignatius. Huu sio wakati wa kufungua na kufunga milango. Ninaona wazi kwamba Bwana anatuita tutoke ndani yetu, tuinuke na tutembee. Anatuomba tusigeuze visogo kutoka katika maumivu na vilio vya wakati wetu, lakini tuingie ndani yao, tukifungua njia za neema yake.  Kila mmoja wetu ni njia hiyo kwa sababu ya ubatizo wetu. Ni juu ya kuifungua na kuiweka wazi.

Siku hizi nane za kuonja upendo wake zikusaidie kusikia mwito wa Bwana wa kuwa chanzo cha uzima, tumaini na neema kwa wengine, na hivyo kugundua furaha ya kweli ya kuwepo kwako. Na ili muweza kupata mafundisho ambayo Mtakatifu Ignatius anazungumzia, kwamba "zaidi" ambayo inatuita kugundua kina cha upendo wa Mungu katika zawadi kubwa zaidi ya sisi wenyewe. Na tafadhali, kila unapokumbuka,usisahau kuniombea, ili niweze kusaidia sisi sote kuwa  daima Mali ya  Mungu kwanza.

Dibaji ya Papa katika kitabu cha Austen
24 Februari 2025, 12:42