MAP

Baba Mtakatifu ameendelea kupokea Ekaristi Takatifu, kujisomea magazeti na nyaraka mbalimbali pamoja na kupata kifungua kinywa hali inayomwezesha kutekeleza walau kazi ndogo ndogo akiwa hospitalini hapo. Taarifa ya 21 Februari 2025 Baba Mtakatifu ameendelea kupokea Ekaristi Takatifu, kujisomea magazeti na nyaraka mbalimbali pamoja na kupata kifungua kinywa hali inayomwezesha kutekeleza walau kazi ndogo ndogo akiwa hospitalini hapo. Taarifa ya 21 Februari 2025  (ANSA)

Maandalizi ya Maadhimisho ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa Kwanza wa NICEA, 325

Patriaki Bartolomeo wa kwanza amemwandikia Papa Francisko ujumbe wa matashi mema, huku akimwombea kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kupona haraka na kuendelea na utume wake mtakatifu pamoja na kazi nzito zilizoko mbele yake. Ujumbe huu ulioandikwa kwa mkono, umewasilishwa kwa Kardinali George Koovakad, aliyekuwa anaongoza ujumbe wa Vatican, uliotembelea Makao makuu ya Kanisa la Kiorthodox, tarehe 18 Februari 2025: Maandalizi ya Sherehe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Taarifa kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, iliyoko Mjini Roma Nchini Italia Ijumaa asubuhi tarehe 21 Februari 2025 inaonesha kwamba, afya ya Baba Mtakatifu Francisko inaendelea kuimarika zaidi na anapata mapumziko ya kutosha, lakini madaktari wanamtaka apumzike zaidi. Baba Mtakatifu kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa mkamba (Bronchitis) uliopelekea kulazwa tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 na kwamba, hadi sasa anaendelea na matibabu. Ameendelea kupokea Ekaristi Takatifu, kujisomea magazeti na nyaraka mbalimbali pamoja na kupata kifungua kinywa hali inayomwezesha kutekeleza walau kazi ndogo ndogo akiwa hospitalini hapo. Baba Mtakatifu anawashukuru watu wote wa Mungu wanaoendelea kusali, kumwombea na kumwandikia ujumbe wa matumaini wakati huu anapoendelea na matibabu kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli. Anawakumbuka na kuwaombea wote kwa wema na ukarimu wao! Na habari kutoka Uturuki zinasema kwamba, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, amemwandikia Baba Mtakatifu Francisko ujumbe wa matashi mema, huku akimwombea kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo ili aweze kupona haraka na kuendelea na utume wake mtakatifu pamoja na kazi nzito zilizoko mbele yake. Ujumbe huu ulioandikwa kwa mkono, umewasilishwa kwa Kardinali George Koovakad, aliyekuwa anaongoza ujumbe wa Vatican, uliotembelea Makao makuu ya Kanisa la Kiorthodox, tarehe 18 Februari 2025, kama sehemu ya maandalizi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Uturuki kama sehemu ya kumbukizi ya Jubilei ya Miaka 1700 tangu maadhimisho ya Mtaguso wa kwanza wa Nicea, baadaye mwaka huu 2025.

Patriaki Bartholomeo wa Kwanza: Ujumbe wa Matashi mema na uponyaji
Patriaki Bartholomeo wa Kwanza: Ujumbe wa Matashi mema na uponyaji   (Vatican Media)

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kuimarisha majadiliano ya kitaalimungu na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, ili kurahisisha ukaribu wa Makanisa haya mawili, unaofumbatwa katika dhana ya Sinodi, kwa kutambua kwamba, Kanisa, kimsingi tayari ni Sinodi, kwa sababu limeanzishwa na Kristo Yesu na linaongozwa na Roho Mtakatifu na kwamba, mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ni muhimu sana. Hizi ni juhudi pia zinazoendelea kutekelezwa katika majadiliano ya taalimungu ya kiekumene mintarafu ukulu wa Mtakatifu Petro na Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Ile sentensi “Atokaye kwa Baba na Mwana: “Filoque” na Mafundisho kuhusu kutokukosea kwa Papa anapofundisha akiwa ameungana na Maaskofu wengine, “Infallibility” yamefikia mahali pazuri, kwani huu ni mchakato ambao umesimikwa katika unyenyekevu, upendo na uponyaji na ukweli, ili Wakristo wote kwa pamoja waweze kuufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, kiasi cha kufikia kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo Yesu. Rej. Efe 4: 13.

Mwaka 2025 Wakristo Wanaadhimisha kwa pamoja Pasaka ya Bwana
Mwaka 2025 Wakristo Wanaadhimisha kwa pamoja Pasaka ya Bwana

Kwa hakika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi umekuwa ni chombo cha majadiliano ya kiekumene, amani na upatanissho na kwamba, Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli linaungana na Baba Mtakatifu kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia, ili vita ikome, na hatimaye, Mwenyezi Mungu aweze kuiongoza “miguu yetu kwenye njia ya amani.” Lk 1: 49. Madhara ya vita ni makubwa kamwe hayawezi kubebwa na mtu mmoja. Mji wa Roma umepambwa kwa damu ya mashuhuda wa imani: Mtakatifu Petro na Paulo, Mitume, ni mwaliko wa Kanisa kujikita katika kutafuta, kujenga na hatimaye kudumisha amani. Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Kwanza Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana. Mwaka 2025 wakristo wote wanaadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake.

Kimsingi Kanisa ni la Kisinodi limeanzishwa na Kristo na Kuongozwa na Roho Mt.
Kimsingi Kanisa ni la Kisinodi limeanzishwa na Kristo na Kuongozwa na Roho Mt.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kanuni ya Imani ya Nicea-Constantinopoli ni formula rasmi ambayo ilipitishwa na Mababa wa Mtaguso wa Kwanza wa Nicea (325) ikakamilishwa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381) ili kubainisha imani sahihi ya Kanisa Katoliki dhidi ya uzushi, hasa wa Ario na wafuasi wake. Katika mazingira hayo, lengo kuu lilikuwa kwanza kabisa ni kumkiri Kristo Yesu “Mungu kweli kwa Mungu kweli” yaani Mungu kweli sawa na Baba, halafu kwamba: Roho Mtakatifu anastahili kuabudiwa pamoja na Baba na Mwana (Utatu Mtakatifu). Wakristo wanataka kutembea pamoja na Kristo Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima. Watu wanamtafuta Kristo Yesu hata bila ya kutambua. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anamwomba Mwenyezi Mungu ili awakirimie waja wake afya na nguvu, ili kwa pamoja waweze kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 ya Mtaguso wa kwanza wa Nicea.

Jubilei ya Miaka 1700 NICEA
21 Februari 2025, 09:02