MAP

Kanisa linasali kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko anayekabiliana na changamoto ya afya kwa sasa. Kanisa linasali kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko anayekabiliana na changamoto ya afya kwa sasa.  (ANSA)

Kardinali Pietro Parolin: Sala ya Rozari Takatifu Kwa Ajili ya Papa Francisko!

Ibada hii imehudhuriwa na Makardinali wanaoishi mjini Roma, wafanyakazi wa Sekretarieti kuu na watu wa Mungu katika ujumla wao! Lengo ni kumwombea Baba Mtakatifu ili aweze kupona haraka na hatimaye, kurejea tena kwenye maisha na utume wake. Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, pamoja na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko, Ibada zinazofanywa sehemu mbalimbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Rozari Takatifu ni muhtasari wa upendo na huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Sala ya Rozari ni njia muafaka kabisa ya kutafakari maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kumfahamu, kumpenda, kumfuasa na kumtumikia kwa njia ya upendo kwa Mungu na kwa jirani wenye shida na mahangaiko mbalimbali wanaokumbukwa katika Sala ya Rozari Takatifu. Kwa njia ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, kila mtu ajitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake katika mchakato wa kuponya ulimwengu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumtaza Kristo Yesu aliyeanzisha Ufalme wa Mungu kwa ujasiri, kwa tafakuri na kwa njia ya ushuhuda wa maisha, ili kwa pamoja waweze kuujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani ili kukuza na kudumisha haki, furaha, uponyaji na wokovu kwa wale wote wanaoteseka kwa magonjwa na kifo. Kila mtu katika hali na nafasi yake, ajitahidi kuwa mkarimu, kwa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa leo na kesho iliyo bora zaidi. Waamini wakubali kupokea kwa imani na matumaini majaribu, matatizo na changamoto za maisha, huku wakishirikishana upendo kama sehemu ya ujenzi wa familia ya kweli inayosimikwa katika msingi wa amani na utulivu wa ndani.

Kanisa linasali kwa ajili ya Baba Mtakatifu Francisko
Kanisa linasali kwa ajili ya Baba Mtakatifu Francisko   (ANSA)

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, ili aweze kuwasaidia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, kielelezo cha imani tendaji! Bikira Maria ni mfano na kielelezo cha imani, matumaini na mapendo, kwani amediriki kuwa ni mfuasi amini wa Kristo Yesu na chombo cha huduma makini kwa jirani zake; mtindo na mfumo wa maisha unaopaswa kutekelezwa na Mapadre kama sehemu ya majiundo yao ya awali na endelevu katika Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, ikiwa kweli waamini wanataka kuwa wafuasi amini wa Kristo Yesu na Kanisa lake; ili kuguswa na kuponywa na huruma pamoja na upendo wa Mungu, wanapaswa kuzingatia mambo makuu yafuatayo: Fumbo la Msalaba, Ekaristi Takatifu na Ibada ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Bikira Maria ni Mama wa Mungu na Kanisa, kwani ndani ya Moyo wake safi usiokuwa na doa, watu wote wanapata utambulisho wao, kwa kupenda na kupendwa, hali inayoonesha uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mama wa Mlango wa Mbinguni, ametangazwa kuanzia sasa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni “Bikira Maria Mama wa huruma na matumaini.”

Rozari Takatifu kwa Bikira Maria Afya ya Wagonjwa
Rozari Takatifu kwa Bikira Maria Afya ya Wagonjwa   (ANSA)

Ni Mama ambaye daima ameonesha ulinzi na tunza kwa watu wanaomkimbilia katika shida na mahangaiko yao; upendo ambao umeendelezwa hadi nyakati hizi. Bikira Maria ni dira na kielelezo cha njia ya kwenda mbinguni; Njia ambayo kamwe haiwezi kumpotezesha mtu mwelekeo wa maisha! Njia hii, ni Kristo Yesu ambaye pia ni ukweli na uzima. Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani. Bikira Maria, nyota ya asubuhi anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko ana ibada ya pekee kwa Bikira Maria.

Kardinali Pietro Parolin Akiongoza Sala ya Rozari Takatifu kwa Ajili ya Papa
Kardinali Pietro Parolin Akiongoza Sala ya Rozari Takatifu kwa Ajili ya Papa   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatatu, tarehe 24 Februari 2025 majira ya Saa tatu kwa saa za Ulaya, sawa na Saa tano kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati, amewaongoza waamini na watu wenye mapenzi mema kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa mkamba (Bronchitis) uliopelekea kulazwa tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma. Ibada hii imehudhuriwa na Makardinali wanaoishi mjini Roma, wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican na watu wa Mungu katika ujumla wao! Lengo la Sala hii ya Rozari Takatifu ni kumwombea Baba Mtakatifu ili aweze kupona haraka na hatimaye, kurejea tena kwenye maisha na utume wake. Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, pamoja na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko, Ibada zinazofanywa sehemu mbalimbali za dunia. Kardinali Parolin, amemwweka Baba Mtakatifu Francisko chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Afya ya Wagonjwa “Salus infirmorum.”

Papa Francisko ana Ibada kubwa kwa Bikira Maria.
Papa Francisko ana Ibada kubwa kwa Bikira Maria.   (AFP or licensors)

Waamini wanasali kumwombea Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa sasa yuko katika hatari ya kifo, ili kwa sala na maombezi ya Bikira Maria aweze kupata faraja na nafuu katika mahangaiko yake. Kwa upande wake Kardinali Lazzaro You Heung-sik, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Wakleri, amefurahishwa sana na kitendo cha watu wa Mungu kuungana kwa ajili ya kusali na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko wakati huu anapokabiliana na changamoto ya afya. Baba Mtakatifu ni Khalifa wa Mtakatifu Petro ambaye ameonesha upendo mkubwa kwa watu wa Mungu, sasa ni zamu ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha upendo wao kwake, ili aweze kupona haraka. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwilisha ndani mwao, tunu msingi za Kiinjili hususan upendo kwa Mungu na jirani.

Kanisa zima lina sali kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko
Kanisa zima lina sali kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Na habari zaidi kutoka kwa Dr Matteo Bruno, Msemaji mkuu wa Vatican zinaonesha kwamba, hali ya afya ya Baba Mtakatifu Francisko inaendelea kuimarika taratibu na kwamba vipimo mbalimbali vinaonesha matumaini ingawa tatizo la figo kushindwa kufanya kazi yake barabara ni jambo linalowatia wasiwasi madaktari. Baba Mtakatifu anaendelea kupumua kwa kutumia mirija. Jopo la Madaktari wanaomtibu Baba Mtakatifu Francisko linasema, hali yake ya afya bado ni tete. Jumatatu tarehe 24 Februari 2025 aliweza kupokea Ekaristi Takatifu na kufanya shughuli ndogo ndogo. Jioni aliweza kuzungumza la Paroko wa Parokia moja huko Ukanda wa Ghaza, ili kuonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wanaoteseka huko. Baba Mtakatifu kutoka katika undani wa moyo wake, anawashukuru kwa dhati watu wote wa Mungu wanaomwombea ili aweze kupona haraka iwezekanavyo. Baba Mtakatifu Francisko usiku wa kuamkia tarehe 25 Februari 2025 amelala vizuri.

Kardinali Parolin Rozari
25 Februari 2025, 08:27