Kardinali Parolin: Uvumi Kuhusu Kujiuzuru Kwa Papa Francisko Hauna Mvuto Wala Mashiko
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, kuna uvumi usio na maana, mvuto wala mashiko kuhusu kujiuzuru kwa Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuugua na hatimaye kulazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, iliyoko mjini Roma. Jambo la msingi kwa wakati huu ni kuhakikisha kwamba, Baba Mtakatifu anapata matibabu muafaka, ili aweze kusimama tena na hatimaye, kurejea mjini Vatican kuendelea na utume wake. Haya ni majibu yaliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin katika mahojiano maalum na Gazeti la “Corriere della Sera” linalochapishwa kila siku nchini Italia. Tangu Baba Mtakatifu Francisko alazwe, tarehe 14 Februari 2025, kumekuwepo na uvumi, uzushi na habari za kughusi kuhusu afya ya Baba Mtakatifu na kwamba, ameonesha dalili za kutaka kung’atuka kutoka madarakani.
Huu ni uvumi unaoihusisha Vatican na kwamba, Kardinali Parolin binafsi hajasikia uvumi huu, wala mipango ya Baba Mtakatifu Francisko kutaka kung’atuka. Katika hali na mazingira kama haya, si ajabu kuona watu wakiandika habari za kughushi zisizo kuwa na mvuto wala mashiko na kwamba, hii si mara ya kwanza uzushi kama huu kutolewa na watu wenye nia mbaya. Kardinali Parolin, hivi karibuni amerejea kutoka Burkina Faso na alipozungumza na Baba Mtakatifu, akamwambia kwamba, yuko tayari kumtembelea hospitalini ikiwa kama ataona inafaa, lakini hadi sasa hakuna sababu msingi za kumtembelea Baba Mtakatifu Francisko hospitalini, kwani anatakiwa kuwa na muda wa mapumziko. Habari kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli zinaendelea kutia moyo kwamba, hali ya afya ya Baba Mtakatifu inaendelea kuimarika kila kukicha!
Wakati huo huo, Kardinali Víctor Manuel Dias Fernández, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafunfundisho Tanzu ya Kanisa, katika mahojiano maalum na Gazeti la La Naciòn” linalochapishwa nchini Argentina anasema, haina maana kwa baadhi ya makundi yanayotaka kumshinikiza Baba Mtakatifu Francisko kung’atuka kutoka madarakani. Hii ni kampeni ambayo kwa miaka kadhaa sasa wanaifanya. Lakini ikumbukwe kwamba, kung’atuka kwa halali kwa Baba Mtakatifu Francisko kutoka madarakani lazima iwe ni kwa ridhaa yake mwenyewe na wala si vinginevyo. Kumbe, hapa hakuna habari mpya, yote ni ya zamani! Kardinali Víctor Manuel Dias Fernández anakaza kusema, jambo la muhimu kwake ni kuona kwamba, afya ya Baba Mtakatifu Francisko inaendelea kuimarika zaidi.