ĐÓMAPµĽş˝

Jubilei ya Mashemasi:Kupokea sakramenti ya daraja ni kushuka

Mashemasi wa kudumu 23 wamewekwa wakfu,Dominika 23 Februari 2025 katika Ibada ya Misa Takatifu iliyongozwa na Askofu mkuu Fisichella,Mwenyekiti mwenza,Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro,Vatican.Ni katika Jubilei ya mashemasi iliyoanza tarehe 21 Februari.Katika Mahubiri yaliyotayarishwa Baba Mtakatifu ametafakari mwelekeo wa msingi wa maisha ya Kikristo na huduma:msamaha, huduma ya bure na ushirika.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Dominika tarehe 23 Februari 2025 kwenye Ibada ya Misa Takatifu iliyongozwa na Askofu Mkuu Salvatore Rino Fisichella, Mwenyekiti mwenza, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu; aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuadhimisha Ibada ya misa Takatifu hii ya Jubilei ya Mashemasi, iliyoanza tarehe 21 Februari Mashemasi wa kudumu 23 wamewekwa wakfu. Misa iliaadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia Saa 3: 00 kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 5:00 kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati. Mara baada ya Masomo yote, Askofu Mkuu Fisichella kabla ya mahubiri alisema kuwa: “Kaka na dada, na zaidi ya yote ninyi, mashemasi wapendwa, na ninyi ambao hivi karibuni, kwa kuwekewa mikono, mtaingia katika daraja takatifu la ushemasi, ninafurahi sana kusoma Homilia ambayo Papa Francisko mwenyewe angewasilisha kwenu nyote Dominika hii maalum. Katika adhimisho la Ekaristi, ambapo ushirika unachukua mwelekeo wake kamili na muhimu zaidi, tunahisi Papa Francisko, ingawa yuko katika kitanda cha hospitali, yuko karibu nasi, na tunahisi yuko kati yetu. Na hii inatuwajibisha kufanya maombi yetu kuwa na nguvu zaidi na mazito zaidi, ili Mungu amsaidie katika wakati wake wa majaribu na ugonjwa.”

Misa iliongoza na Askofu Mkuu Fisichella
Misa iliongoza na Askofu Mkuu Fisichella   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Katika mahubiri yaliyoandaliwa na Baba Mtakatifu, Askofu Mkuu alianza kusoma kuwa Ujumbe wa Masomo ambao tumesikia unaweza kufupishwa kwa neno moja: kutoa bure. Ni neno pendwa kwenu Mashemasi, mliokusanyika hapa kwa ajili ya kusherehekea Jubilei. Hebu basi tutafakari juu ya mwelekeo huu wa msingi wa maisha ya Kikristo na huduma yenu, hasa chini ya vipengele vitatu: msamaha, huduma ya bure na ushirika. Kwanza: msamaha. Kutangaza msamaha ni kazi muhimu ya shemasi. Kwa hakika ni jambo la lazima kwa kila safari ya kikanisa na sharti kwa kila mtu kuishi pamoja. Yesu anatuonesha hitaji na upeo wa hili anaposema: “Wapendeni adui zenu” (Lk 6:27). Na hivyo ndivyo ilivyo: kukua pamoja, kugawana taa na vivuli vya kila mmoja, mafanikio na kushindwa, ni muhimu kujua jinsi ya kusamehe na kuomba msamaha, kuunganisha mahusiano na sio kuwatenga kutoka katika upendo wetu hata wale wanaotuumiza na kutusaliti.

Ulimwengu ambao kuna chuki tu kwa wapinzani ni ulimwengu usio na matumaini, usio na mustakabali, uliokusudiwa kusambaratika na vita, migawanyiko na kisasi kisicho na mwisho, kama tunavyoona kwa bahati mbaya hata leo, katika viwango vingi na sehemu mbali mbali za ulimwengu. Kusamehe, basi, kunamaanisha kuandaa makao ya kukaribisha, salama kwa siku zijazo, ndani yetu na katika jamii zetu. Na shemasi, ambaye yeye binafsi amewekezwa na huduma inayompeleka kwenye viunga vya ulimwengu, anajitolea kuona na kufundisha wengine kuona kwa kila mtu, hata kwa wale wanaofanya makosa na kusababisha mateso, dada na kaka waliojeruhiwa katika nafsi zao, na kwa hiyo ni muhimu zaidi kuliko mtu yeyote wa upatanisho, mwongozo na msaada.

Jubilei ya mashemasi
Jubilei ya mashemasi   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Somo la kwanza linatuzungumzia juu ya uwazi huu wa moyo, likituonesha upendo wa Daudi mwaminifu na wa ukarimu kwa Sauli, mfalme wake, lakini pia mtesi wake (taz 1 Sam 26:2,7-9,12-13,22-23). Pia tunasikia juu yake, katika muktadha mwingine, kwa mfano katika kifo cha shemasi Stefano, ambaye alianguka chini kwa kupigwa mawe, huku akiwasamehe wale waliompiga kwa mawe (taz.Mdo 7:60). Lakini zaidi ya yote tunaiona kwa Yesu, kielelezo cha kila ushemasi, ambaye pale msalabani, “akijiweka utupu” hadi kufikia hatua ya kutoa uhai wake kwa ajili yetu (taz.Flp 2:7), anawaombea watesi wake na kufungua milango ya Mbingu kwa mwizi mwema (taz Lk 23:34.43).

Na tunakuja kwenye hatua ya pili: huduma ya bure. Bwana, katika Injili, anaielezea kwa maneno rahisi kama ilivyo wazi: "Fanyeni mema na kukopesha, bila kutarajia malipo yoyote" (Lk 6:35). Ni maneno machache ambayo hubeba ndani yake harufu nzuri ya urafiki. Kwanza kabisa, upendo wa Mungu kwetu sisi, kisha upendo wetu pia. Kwa shemasi, mtazamo huu si sehemu ya nyongeza ya matendo yake, bali ni sehemu kubwa ya utu wake. Kwa hakika, anajiweka wakfu kuwa, katika huduma yake, “mchongaji” na “mchoraji” wa uso wenye huruma ya Baba, shahidi wa fumbo la Mungu Utatu. Katika vifungu vingi vya Injili Yesu anazungumza juu yake mwenyewe katika nuru hii. Anafanya hivyo pamoja na Filipo, katika Chumba cha karamu Kuu, muda mfupi baada ya kuosha miguu ya wale Kumi na Wawili, akimwambia: "Yeyote aliyeniona mimi amemwona Baba" (Yh 14:9). Vile vile anapoanzisha Ekaristi, akithibitisha: “Mimi niko miongoni mwenu kama mhudumu” (Lk 22:27). Lakini tayari hapo awali, akiwa njiani kuelekea Yerusalemu, wanafunzi wake walipokuwa wakibishana wao kwa wao kuhusu ni nani aliyekuwa mkuu zaidi, alikuwa amewaeleza kwamba “Mwana wa Adamu hakuja kutumikiwa, bali kutumikia, na kutoa nafsi yake kwa ajili ya fidia ya wengi” (taz. Mk 10:45).

Jubilei ya mashemasi
Jubilei ya mashemasi   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ndugu Mashemasi, kazi ya huduma ya bure mnayoifanya, kwa hiyo, kama onesho la kujitoa kwenu kwa upendo wa Kristo, ni kwenu tangazo la kwanza la Neno, chanzo cha uaminifu na furaha kwa wale wanaokutana nanyi. Kusindikizana nao kadiri iwezekanavyo kwa tabasamu, bila kulalamika na bila kutafuta kutambuliwa, mmoja katika kumuunga mkono mwingine, hata katika uhusiano na Maaskofu na mapadre, "kama kielelezo cha Kanisa lililojitolea kukua katika huduma ya Ufalme kwa kuthaminishwa kwa ngazi zote za huduma zilizowekwa wakfu" (C.E.I., mashemasi wa kudumu Katika Kaisa la Italia. Maelekezo na kanuni 1993, 55 ). Matendo yenu ya umoja na ukarimu hivyo yatakuwa ni daraja linalounganisha Altare barabarani, Ekaristi kwa maisha ya kila siku ya watu; Upendo utakuwa liturujia yenu nzuri zaidi na liturujia itakuwa huduma yenu ya unyenyekevu zaidi.

Jubilei ya mashemasi
Jubilei ya mashemasi   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Na tunafika kwenye hatua ya mwisho: Kutoa bure kama chanzo cha ushirika. Kutoa bila kuomba chochote kwa malipo huunganisha, hujenga vifungo, kwa sababu huonesha na kulisha kiumbe cha pamoja ambacho hakina lengo lingine isipokuwa zawadi ya mtu mwenyewe na mema ya watu. Mtakatifu Lawrence, mlinzi wenu, alipoombwa na washtaki wake kukabidhi hazina za Kanisa, aliwaonesha maskini na kusema: "Hazina zetu hapa!" Hivi ndivyo ushirika unavyojengwa: kwa kuwaambia kaka na dada zetu, kwa maneno, lakini zaidi ya yote kwa vitendo, kibinafsi na kama jumuiya: "ninyi ni muhimu kwetu", "tunawapenda", "tunataka muwe sehemu ya safari yetu na maisha yetu." Hivi ndivyo mnavyofanya: waume, baba na babu tayari, katika huduma, kupanua familia zenu kwa wale wanaohitaji, mahali mnapoishi. Kwa hivyo misheni yenu, ambayo inawatoa kutoka katika jamii ili kuiingiza tena na kuifanya mahali panapozidi kukaribishwa wazi kwa wote, ni mojawapo ya maneno mazuri sana ya Kanisa la kisinodi na “linalotoka nje.”

Jubilei ya mashemasi
Jubilei ya mashemasi   (Vatican Media)

Muda mfupi baadhi yenu, wakipokea sakramenti ya daraja, "watashuka" katika hatua za huduma. Ninasema kwa makusudi na kusisitiza kwamba "watashuka", na sio kwamba "watapanda", kwa sababu katika Daraja mtu hapandi, lakini anashuka, mtu anakuwa mdogo, anajishusha na anajivua. Kutumia maneno ya Mtakatifu Paulo, katika huduma tunamwacha “mtu wa dunia” na, kwa upendo, tunajivika “mtu wa mbinguni” (rej. 1Kor 15:45-49). Hebu sote tutafakari juu ya kile tunachokaribia kufanya, wakati tunajikabidhi kwa Bikira Maria, mtumishi wa Bwana, na kwa Mtakatifu Lawrence, mlinzi wenu. Na tusaidiwe kuishi kila moja ya huduma zetu kwa moyo mnyenyekevu uliojaa upendo na kuwa, kwa ukarimu, mitume wa msamaha, watumishi wasio na ubinafsi wa ndugu zetu na wajenzi wa ushirika. Alihitimisha.

Ikumbukwe Mashemasi wa kudumu wanatekeleza dhamana na utume wao katika Liturujia ya Kanisa sanjari na huduma ya upendo kwa familia ya Mungu. Italia inawakilishwa na idadi kubwa ya Mashemasi wa kudumu wapatao elfu nne, Marekani 1300, Ufaransa 656, Hispania 350, Brazili 230, Ujerumani 150. Kuna idadi kubwa ya Mashemasi wa kudumu kutoka Cameroon, Nigeria, India, Indonesia pamoja na Australia. Mashemasi wa kudumu, Ijumaa tarehe 21 Februari 2025 walifanya katekesi, walishirikishana uzoefu na mang’amuzi ya maisha na utume wao, huku wakiongozwa na Maaskofu kumi na wawili, alama makini ya matumaini katika utume wao.

Jubilei ya mashemasi
Jubilei ya mashemasi   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Jumamosi tarehe 22 Februari 2025 washiriki walipitia kwenye lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Na jioni kulikuwa na mkesha wa Sala na hatimaye, Jubilei ikahitimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu Dominika tarehe 23 Februari 2025 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Kuhusiana na suala la Mashemasi: kuna makundi mawili ya Mashemasi ndani ya Kanisa Katoliki. Kuna Mashemasi wa mpito kuelekea Daraja Takatifu la Upadre na kuna Mashemasi wa kudumu ambao wengi wao ni watu wa familia, lakini wanajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa kadiri ya Sheria za Kanisa, lakini zaidi huduma ya upendo inayomwilishwa katika matendo ya huruma kiroho na kimwili. Huduma ya Sakramenti ya Daraja Takatifu tangu mwanzo, imegawanyika katika sehemu kuu tatu: Uaskofu ambao ni utimilifu wa Sakramenti ya Daraja; Upadre na Ushemasi. Kumbe, Mashemasi ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu na Mapadre.

Jubilei ya mashemasi
Jubilei ya mashemasi   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo Yesu kwa kupewa chapa isiyofutika na hufananishwa na Kristo aliyejifanya “Shemasi” yaani mtumishi wa wote. Mashemasi ni wahudumu wakuu wakati wa maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, hasa wakati wa Ibada ya Misa Takatifu. Mashemasi wanaweza kusimamia na kubariki Ndoa Takatifu. Ni wahudumu wa Neno kwa kutangaza, kuhubiri na kulishuhudia katika huduma mbali mbali za upendo. Dhana ya Mashemasi wa kudumu, ambao kimsingi wanapewa Ushemasi wa huduma kadiri ya mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Barani Afrika ni wachache sana, lakini kazi ya huduma kwa kiasi kikubwa inatekelezwa na Makatekista.

Mahubiri 23 Februari katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro

 

23 Februari 2025, 10:46