Jubilei ya Mashemasi Wa Kudumu Vyombo Na Mashuhuda wa Injili ya Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI katika Waraka wake wa Kitume “Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika” anakazia kuhusu umuhimu wa wito walioupokea Mashemasi wa kudumu. Katika uaminifu kwa umisionari wa kale, Mashemasi wa kudumu wanakaribishwa kufanya kazi kwa unyenyekevu na kwa ushirikiano wa karibu zaidi na Maaskofu, huku wakiendelea kutoa kipambaule kwa kile ambacho Kristo Yesu anawafundisha waja wake katika Injili, huku wakiendelea kujivunia kazi wanayoitekeleza vyema; huku wakiendelea kujikita katika nguvu ya kimaadili, kwa kuheshimu tunu za: Uaminifu, ukweli, furaha ya mmoja kuongeza jiwe lake katika jengo la Kristo na jamii, kulinda uasili, kujali maslahi ya wote. Mashemasi wa kudumu waisaidie jamii ya Kiafrika katika kila ngazi kuhimiza uwajibikaji; Kwa upande wa wanaume ambao ni watu wa ndoa na mababa, wajitahidi kuheshimu wanawake ambao ni sawa na wanaume kwa heshima, na kujali watoto walioachwa bila elimu. Maaskofu wawe na jicho la pekee kwa wagonjwa; wale ambao ni dhaifu na maskini katika Jumuiya. Wote hawa waonjeshwe upendo wa dhati. Katika kazi ya kichungaji ya maparokia, Mashemasi wa kudumu wakumbuke kwamba maisha mazuri ya kiroho huruhusu Roho wa Kristo Yesu kumkomboa mtu ili aweze kutenda kwa ufanisi katika jamii. Maaskofu wanapaswa kuwa waangalifu ili kuhakikisha kwamba, Mashemasi wa kudumu wanapata malezi ya awali na endelevu ili waweze kuchangia katika mchakato wa maboresho ya utendaji wa huduma yao. Kama Mtakatifu Stefano, Mtakatifu Laurenti na Mtakatifu Vinsenti, Mashemasi na mashahidi, wajitahidi kutambua na kukutana na Kristo Yesu katika Ekaristi na katika huduma kwa maskini. Huduma hii ya Altare na ya upendo itawafanya watazamie kukutana na Kristo Yesu aliyepo Altareni na katika maskini. Na hivi wataweza kujitoa maisha yenu kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake hata ikibidi kuyamimina maisha yao. Rej. Africae munus n. 115-116.
Mashemasi ni wapanzi wa imani, matumani na mapendo. Ni vyombo na mashuhuda wa matumaini; ni vyombo vya Injili ya huduma ya mapendo kwa maskini na kwamba, Mashemasi hawana budi kufunzwa ili waweze kuwa ni vyombo vya amani na mashuhuda wa Injili ya huduma ya matumaini. Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo inawakusanya Mashemasi wa kudumu elfu sita kutoka katika nchi mia moja; ambao wengi wao wana watoto na familia; hii ni fursa kwao kuweza kukutana na wenzi wao katika wito na utume wa huduma ya huruma na upendo katika Jumuiya za Kikristo. Ni muda wa kusali, kutafakari sanjari na kupyaisha ari na mwamko wa huduma ya kimisionari kwa kutambua kwamba, huruma ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Itakumbukwa kwamba, Mashemasi wa kudumu wanatekeleza dhamana na utume wao katika Liturujia ya Kanisa sanjari na huduma ya upendo kwa familia ya Mungu. Italia inawakilishwa na idadi kubwa ya Mashemasi wa kudumu wapatao elfu nne, Marekani 1300, Ufaransa 656, Hispania 350, Brazili 230, Ujerumani 150. Kuna idadi kubwa ya Mashemasi wa kudumu kutoka Cameroon, Nigeria, India, Indonesia pamoja na Australia. Mashemasi wa kudumu, Ijumaa tarehe 21 Februari 2025 wameanza katekesi, wameshirikishana uzoefu na mang’amuzi ya maisha na utume wao, huku wakiongozwa na Maaskofu kumi na wawili, alama makini ya matumaini katika utume wao.
Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Mashemasi wa kudumu ishirini na tatu, watawekwa wakfu, hapo Dominika tarehe 23 Februari 2025 kwenye Ibada ya Misa Takatifu itakayongozwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Mwenyekiti mwenza, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu; aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko. Ibada hii itaadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia majira ya Saa 3: 00 kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 5:00 kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati. Maadhimisho ya Jubilei ya Mashemasi ni kuanzia tarehe 21 hadi tarehe 23 Februari 2025. Mashemasi wa kudumu wanaalikwa kwa namna ya pekee kuwa kweli ni wahudumu wa upendo katika Jumuiya za Kikristo. Zote hizi ni changamoto ambazo Mashemasi wa kudumu wanakabiliwa nazo, ili hatimaye, waweze kujichotea nguvu na ari ya kusimama kidete katika ushuhuda wa maisha yao. Jumamosi tarehe 22 Februari 2025 washiriki watapita kwenye lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. “Hawa ni Mashemasi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari: Ili wawe ni mashuhuda wa matumaini. Baadaye, jioni kutakuwa na mkesha wa Sala na hatimaye, Jubilei hii itahitimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu Dominika tarehe 23 Februari 2025 kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Itakumbukwa kwamba, kuna makundi mawili ya Mashemasi ndani ya Kanisa Katoliki. Kuna Mashemasi wa mpito kuelekea Daraja Takatifu la Upadre na kuna Mashemasi wa kudumu ambao wengi wao ni watu wa familia, lakini wanajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa kadiri ya Sheria za Kanisa, lakini zaidi huduma ya upendo inayomwilishwa katika matendo ya huruma kiroho na kimwili.Huduma ya Sakramenti ya Daraja Takatifu tangu mwanzo, imegawanyika katika sehemu kuu tatu: Uaskofu ambao ni utimilifu wa Sakramenti ya Daraja; Upadre na Ushemasi. Kumbe, Mashemasi ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu na Mapadre. Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo Yesu kwa kupewa chapa isiyofutika na hufananishwa na Kristo aliyejifanya “Shemasi” yaani mtumishi wa wote. Mashemasi ni wahudumu wakuu wakati wa maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, hasa wakati wa Ibada ya Misa Takatifu. Mashemasi wanaweza kusimamia na kubariki Ndoa Takatifu. Ni wahudumu wa Neno kwa kutangaza, kuhubiri na kulishuhudia katika huduma mbali mbali za upendo. Dhana ya Mashemasi wa kudumu, ambao kimsingi wanapewa Ushemasi wa huduma kadiri ya mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Barani Afrika ni wachache sana, lakini kazi ya huduma kwa kiasi kikubwa inatekelezwa na Makatekista.