MAP

Kardinali James Michael Harvey, Kiongozi mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Kuta za Roma, Dominika tarehe 5 Januari 2025 amefungua Lango kuu la Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Kardinali James Michael Harvey, Kiongozi mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Kuta za Roma, Dominika tarehe 5 Januari 2025 amefungua Lango kuu la Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Lango Kuu la Jubilei ya Miaka 2025 Ni Kielelezo cha Fumbo la Pasaka: Furaha na Matumaini

Kardinali James Michael Harvey, Kiongozi mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Kuta za Roma, Dominika tarehe 5 Januari 2025 amefungua Lango kuu la Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Katika mahubiri yake amekazia zaidi kuhusu furaha na matumaini. Lango kuu la Jubilei ni kielelezo cha Fumbo la Pasaka; Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa watu waliokata tamaa na kuvunjika moyo: Furaha na Matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, katika mkesha wa Noeli tarehe 24 Desemba 2024 amefungua Lango Kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, mwanzo wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo. Hili ni Lango la: Imani, matumaini na chemchemi ya watu wote wa Mungu. Tayari Lango la Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano lilikwisha funguliwa. Tarehe Mosi, Januari 2025 Lango kuu la Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma lilifunguliwa, mwaliko kwa waamini kujizatiti zaidi kutembea katika umoja na mshikamano kumwelekea Kristo Yesu, huku wakiwa na wasiwasi wa kweli na wa dhati kwa wapendwa wao, maskini, wagonjwa na wale ambao wamepoteza njia ya ukweli, furaha na amani. Wote wanaitwa kuwa ni mahujaji wa tumaini la furaha. Kwa hakika Bikira Maria ni ishara ya tumaini la hakika na faraja. Kumbe, Maadhimisho ya Jubilei ni kwa ajili ya watu wote, ili kuwaonjesha tena matumaini ya Injili, matumaini ya mapendo na matumaini ya msamaha wa kweli.

Lango la Jubilei, Kanisa Kuu la Mt. Paulo Nje ya Kuta za Roma limefunguliwa
Lango la Jubilei, Kanisa Kuu la Mt. Paulo Nje ya Kuta za Roma limefunguliwa   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ni katika muktadha huu, Kardinali James Michael Harvey, Kiongozi mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Kuta za Roma, Dominika tarehe 5 Januari 2025 amefungua Lango kuu la Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Katika mahubiri yake amekazia zaidi kuhusu furaha na matumaini. Lango kuu la Jubilei ni kielelezo cha Fumbo la Pasaka na kwamba, waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem" yaani “Mahujaji wa Matumaini” na kwamba, Msalaba ni kielelezo cha ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Kuvuka Lango la Jubilei ni tukio la furaha, kwa sababu Mama Kanisa anaendelea kusherehekea kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, kadiri ya mpango wa Mungu. “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo” na hivyo kufanyika watoto wake wateule. Hiki ndicho kiini cha Fumbo la Umwilisho, kilicho mpelekea Kristo Yesu, kuwa ni chemchemi ya maisha na uzima wa milele; kwa kuwaunganisha tena watu pamoja na Mungu wao. Mwinjili Yohane anasema: “Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema.” Yn 1:16.

Kristo Yesu ni lango la imani, matumaini na mapendo
Kristo Yesu ni lango la imani, matumaini na mapendo   (ANSA)

Waamini wanafurahi kwa sababu ya kazi ya ukombozi iliyoletwa na Kristo Yesu; ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu. Kristo Yesu, Mwana wa Baba wa milele alijinyenyekesha, akatimiza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni, akateswa, akafa Msalabani na hatimaye akafufuka siku ya tatu kadiri ya Maandiko Matakatifu na hivyo kuwapatanisha watu na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao, chemchemi ya uthabiti wa moyo ambalo ni tumaini; na tumaini halitahayarishi. Rej. Rum 5:5. Watu wengi walipondekeza na kuvunjika moyo wakati wa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Watu wamekata tamaa kutokana na vita, kinzani na migogoro mbalimbali inayoendelea kumwandama mwanadamu kila kukicha bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchini; matukio yote haya yanawafanya binadamu kujikita katika matumaini yanayojenga mahusiano na mafungamano yake na Kristo Yesu, ili kuweza kupambana na yale yajayo kwa ari na moyo mkuu. Habari Njema ya Wokovu ni kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa watu ni chemchemi ya matumaini kwa waja wake.

Jubilei ni kipindi cha toba, wongofu wa ndani na upatanisho
Jubilei ni kipindi cha toba, wongofu wa ndani na upatanisho   (Vatican Media)

Mababa wa Kanisa wanasema: Matumaini ni fadhila ya Kimungu inayowawezesha waamini kutamani heri ya Ufalme wa mbinguni na uzima wa milele kwa kutumainia ahadi za Kristo Yesu na kutegemea, siyo nguvu zao wenyewe, bali msaada wa neema ya Roho Mtakatifu kwa sababu Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu katika utekelezaji wa ahadi zake. Kwa njia ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, waamini wanaweza kuhesabiwa haki kwa neema yake ili wapate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama tumaini lao. Fadhila ya matumaini inajibu tamaa ya heri ilivyowekwa na Mungu katika moyo wa kila mtu. Yachota matumaini yanayovuvia matendo ya watu. Huyatakasa ili kuyapanga kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni nyakati za upweke. Hufungua moyo katika kungoja heri ya milele. Akielekezwa na matumaini anakingwa na ubinafsi na anaongozwa kwenye furaha itokanayo na mapendo. Matumaini ya Kikristo yanakita mizizi yake katika Heri za Mlimani ambazo kimsingi ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wanafunzi wake. Matumaini ni “nanga ya roho”, hakika na thabiti; ni silaha inayowalinda waamini katika mapambano ya wokovu. Matumaini ni fadhila ya Kikristo inayojikita katika unyenyekevu na nguvu ya kuweza kusonga mbele katika safari ya maisha, licha ya vikwazo na magumu yaliyopo. Matumaini kwa Mwenyezi Mungu kamwe hayawezi kumdanganya mwamini kwani Mwenyezi Mungu daima ni mwaminifu katika kutekeleza ahadi zake. Mungu ni chemchemi ya furaha na amani mioyoni mwa waja wake. Rej. KKK 1817-1821.

Kardinali James M. Harvey akiongoza Ibada ya Ufunguzi wa Lango kuu
Kardinali James M. Harvey akiongoza Ibada ya Ufunguzi wa Lango kuu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kimsingi, matumaini ni chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem" yaani “Mahujaji wa Matumaini” ni mwaliko wa kuendelea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu juu ya Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Maadhimisho ya Jubilei ni muda muafaka wa toba na wongofu wa ndani; muda wa msamaha na maondoleo ya dhambi yanayosimikwa katika fadhila ya matumaini. Matumaini yananogesha hija ya maisha ya hapa duniani. Chini ya Msalaba wa Kristo Yesu unaohifadhiwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, Nje ya Kuta za Roma kuna maneno yanayosema “Spes unica” yaani “Tumaini pekee.” Yaani Msalaba wa Kristo ni kielelezo cha ushindi dhidi ya dhambi na mauti na Msalaba ni tumaini pekee la waamini. Kumbe, waamini wanaitwa na kutumwa kama mahujaji na vyombo vya matumaini.

Lango la Jubilei 2025
05 Januari 2025, 15:10