Barua ya Papa kwa Padre Mavrič:Shirika linafanya kazi mpya za ubunifu kati ya wahitaji!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko alituma barua kwa Mkuu wa Shirika la Utume lijulikanalo (Lazzarist) , Padre Tomaž Mavrič. Katika barua hiyo iliyotiwa saini tarehe 11 Desemba 2024 katika Kiti cha Papa huko Mtakatifu Yohane, Laterano na ambayo ilichapishwa tarehe 20 Januari 2025, kuwa: "Wakati Shirika la Utume linapojiandaa kufanya kumbukumbu ya miaka 400 ya kuanzishwa kwake, anawapa salamu wote, mapadre na ndugu wa Shirika, na kwa washiriki wote wa Familia kuu ya Vicent. Papa anaomba kwamba “maadhimisho haya muhimu yawe tukio la furaha kuu na uaminifu upya kwa dhana ya uanafunzi wa kimisionari, wanaotokana na kuiga upendo wa Kristo kwa maskini. Mwanzo wa Shirika lao wamejikita katika uzoefu wa kina wa kibinafsi wa Mtakatifu Vincent wa Paulo, katika ule “moto wa upendo” uliowaka ndani ya moyo wa Mwana wa Mungu aliyefanyika mwili na uliompelekea kujihusisha na maskini na wale waliotengwa (Mkutano wa 207 kuhusu upendo mnamo 30 Mei 1659).
Mafundisho ya msingu wa katekesi
Papa amesisitiza kuwa Mtakatifu huyo akiwa amehuzunishwa na ukosefu wa huduma ya kichungaji katika nchi ya Ufaransa, mapema mnamo mwaka 1617 aliamua kuandaa utume wenye lengo la kutoa mafundisho ya msingi ya katekesi na kuhimiza kurejea kwa sakramenti. Ndoto ambayo angetimiza, karibu miaka minane baadaye, kwa kuanzishwa kwa Shirika la Utume mnamo. tarehe 17 Aprili 1625. Katika miaka saba ya kwanza ya maisha, makuhani na ndugu wa Shirika walifanya utume 140. Kati ya 1632 na 1660, wamisionari kutoka Nyumba Mama huko Paris walipanga tume nyingine 550. Kuanzia 1635, na kuzaliwa kwa jumuiya nje ya Paris, mamia ya misheni nyingine zilianzishwa. Upanuzi huu wa ajabu unashuhudia matunda ya kidini na kimisionari ya bidii ya kipadre ya Mtakatifu Vincent na kiu yake ya kugeuza mioyo na akili kwa Kristo.
Mtakatifu Vincent na juhudi kwa maskini
Katika kazi yake ya kuongeza ufahamu miongoni mwa maskini, Mtakatifu Vincent alitambua haraka kwamba kazi za upendo zilipaswa kupangwa vizuri. Wanawake walikuwa wa kwanza kuchukua changamoto hii. Mnamo 1617, katika parokia ya Châtillon, alianzisha shirika la kwanza la "Upendo ambalo linaendelea leo kama Jumuiya ya Kimataifa ya Upando au Wavincent wa kujitolea. Mnamo 1633, pamoja na Mtakatifu Luisa de Marillac, alianzisha aina ya mapinduzi ya Jumuiya ya wanawake,waitwao "Mabinti wa Upendo." Hadi wakati huo, watawa hao waliishi katika nyumba za monansteri; na kwa hiyo Mabinti wa Upendo badala yake walitumwa kwenda kwenye mitaa ya Paris kuwahudumia wagonjwa na maskini. Ubunifu huu utazaa matunda katika kuenea kiukweli kwa Shirika la kitawa la kike lililojitolea kwa kazi za kitume katika karne mbali mbali. Kuanzia mwaka 1628, kwa kuitikia ombi la Askofu wa Beauvais, Shirika la Utume pia lilianza kujishughulisha na malezi ya mapadre. Kazi hii, ambayo ni muhimu sana kwa mageuzi na kufanywa upya kwa Kanisa katika karne ya 17 Ufaransa, ilikua na kustawi. Wakati wa kifo cha Mtakatifu, seminari ishirini zilikuwa zimeanzishwa na vijana 12,000 walikuwa wameshiriki katika mafungo kwa ajili ya maandalizi ya kuwekwa wakfu wa ukuhani.
Orodha ya watakatifu walioiga roho ya Mtakatifu Vincent
Mtakatifu Vincent alisadikishwa juu ya umuhimu wa “huduma hii ya juu na ya hali ya juu,” ambayo ingekuwa sifa ya Shirika (Mkutano wa Kusudi la Shirika mnamo tarehe 6 Desemba 1658). Kanuni za Kawaida zinasema wazi kwamba, kwa asili ya Shirika, huduma hii inapaswa kufanywa "kwa kipimo sawa" na ile ya utume wa kuhubiri (Kanuni za Kawaida, XI, 12). Baba Mtakatifu Francisko anaongeza kuandika kuwa “Katika maadhimisho haya, inafaa kutafakari juu ya urithi wa kiroho, ari ya kitume na huduma ya kichungaji ambayo Mtakatifu Vincent de Paulo alikabidhi kwa Kanisa la kiulimwengu. Orodha ya wale ambao wameiga hali ya kiroho ya Vincent na kuiishi kishujaa kwa miaka mingi ni ndefu na limeenea mabara yote. “ Kwa hiyo anasihi wafikirie Mtakatifu John Gabriel Perboyre, Mtakatifu Francis Regis Clet, Mtakatifu Justin de Jacobis, Mtakatifu Luisa de Marillac, Mtakatifu Jeanne Antide Thouret, Mtakatifu Catherine Labouré, Mtakatifu Elizabeth Anne Seton, Mwenyeheri Frédéric Ozanam na wengine wengi, akiwemo Jân Havlik, waliotangazwa kuwa Mwenyeheri tarehe 31 Agosti 2024 nchini Slovakia. Hata leo hii, Papa anaisistiza katika nyayo za Mtakatifu Vincent, familia yake inaendelea kuanza kazi za upendo, kufanya misheni mpya na kusaidia katika malezi ya mapadre na walei. Zaidi ya matawi 100 ya mapadre, kaka, dada, walei na wanaume wanaunda familia ya Vincent leo.
Jumuiya iliyoanzishwa na Mwenyeheri Ozanam
Jumuiya ya Mtakatifu Vincent de Paulo, iliyoanzishwa mwaka 1833 na Mwenyeheri Frédéric Ozanam, imekuwa nguvu ya ajabu kwa ajili ya wema katika huduma ya maskini, ikiwa na mamia ya maelfu ya wanachama duniani kote. Shirika la Kitume Papa anasisitiza kwa sasa linapitia ishala mpya za ukuaji. Majimbo machanga, hasa katika bara la Asia na Afrika, ambako miito kwa Shirika liinashamiri, yameitikia wito wa kuanza misheni katika nchi nyingine. Shirika pia linaendelea kufanya kazi mpya za ubunifu miongoni mwa wahitaji. Papa alifikiria juu ya “Muungano wa Familia ya Vincent na Wasio na Makazi,” mpango wa kimataifa wa kutoa nyumba za bei nafuu kwa watu wasio na makazi, ukichochewa na mfano wa Vincent de Paul, ambaye alianza kazi yake pamoja nao mwaka wa 1643, kujenga nyumba kumi na tatu kwa ajili ya maskini jijini Paris. Mpango huu una nia ya kuendeleza katika nchi ambapo Wavicenti wapo na ujenzi wa nyumba nyingine, hivyo kuvuka lengo la awali la kukaribisha watu 10,000.
Karne nne za shirika la Mtakatifu Vincent linaendelea kutajirisha Kanisa
Karne nne tangu kuanzishwa kwa Shirika la Utume, hapana shaka kwamba, karama ya Mtakatifu Vincent de Paulo inaendelea kulitajirisha Kanisa kwa njia ya utume na matendo mema ya Familia nzima ya Vicent. Ni matumaini ya Papa kwamba, maadhimisho ya miaka mia nne yataakisi umuhimu wa huduma ya Mtakatifu Vinsenti kwa Kristo kwa ajili ya maskini katika upyaisho wa Kanisa la wakati wetu, katika kufuata kimisionari na kuwasaidia wahitaji na waliotelekezwa katika kando nyingi za ulimwengu wetu na kwenye ukingo wa utamaduni wa juu juu na "kutupwa". Papa ana imani kwa mfano wa Mtakatifu Vincent wanaweza kuwatia moyo vijana kwa namna ya pekee, ambao kwa ari yao, ukarimu wao na kujali kwao kwa ajili ya kujenga ulimwengu bora, wanaitwa kuwa mashahidi shupavu wa Injili kati ya wenzao na mashahidi shupavu wa Injili mahali popote walipo (Waraka wa Kitume wa Baada ya Sinodi Christus Vivit uliochapishwa tarehe 25 Machi 2019, kipengele cha 178).
Unyenyekevu na bidii ya kitume
Kwa hiyo, Papa Francisko kwa upendo mkuu, anawahakikishia mapadre na ndugu wa Shirika la Kimisionari ukaribu wake wakipekee katika sala katika Mwaka wa Jubilei. Papa anasali kwamba, wakiongozwa na Mwanzilishi wao, waendelee kutengeneza maisha yao na kufanya kazi kulingana na himizo la unyenyekevu na bidii ya kitume ambalo aliwaambia washiriki wa kwanza wa Shirika: “Basi, ndugu, tuwe na moyo mkuu, na tujiweke wakfu kwa kufanywa upya, upendo kwa huduma ya maskini, kwa hakika tutafute walio duni na walioachwa zaidi. Tunakiri mbele za Mungu kwamba wao ni walimu na mabwana wetu, na kwamba hatustahili kuwatolea huduma zetu duni” (Hotuba ya 164 kuhusu Upendo kwa Maskini, Januari 1657). Papa alihitimisha Barua yake kwa kuwakabidhi washiriki wote wa Familia ya Vincent kwa maombezi ya kinamama ya Maria, Mama wa Kanisa, na kutoa Baraka yake ya Kitume kama dhamana ya amani na furaha katika Bwana. Na aliwaomba , tafadhali, wamkumbuke katika maombi yao pia..