Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani 2023
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa mwaka huu wa 2023 ni hapo Dominika tarehe 23 Julai 2023 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi” Lk. 1:50. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa mwaka 2023 anagusia kuhusu: Bikira Maria akiwa amejazwa na nguvu ya Roho Mtakatifu akaondoka kwa haraka, Mkutano kati ya Bikira Maria na Elizabeti, Kati ya vijana na wazee; Iwe ni siku ya kukutana kwa furaha na kwa upya kati ya vijana wa kizazi kipya na vijana wa zamani, yaani wazee. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee kwa mwaka 2023 inaonesha ile furaha aliyokuwa nayo Bikira Maria aliyekuwa amejazwa nguvu ya Roho Mtakatifu alipokutana na binadamu yake Elizabeti na kumwakia akisema, “Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Lk 1:42. Na Bikira Maria akamjibu kwa utenzi wake wa “Magnificat” unaotangaza huruma ya Mungu kutoka kizazi hadi kizazi. Roho huyo huyo hubariki na kuambatana na kila mkutano wenye baraka kati ya vizazi na vizazi; kati ya babu, wazee na vijana. Mwenyezi Mungu anawataka vijana walete furaha katika nyoyo za wazee, kama BikiraMaria alivyomfanyia binamu yake Elizabeti na hivyo kupata hekima kutokana na uzoefu wao. Mwenyezi Mungu anawataka waja wake kamwe wasiwaache wazee huku wakisukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii, kama inavyotokea mara nyingi sana katika nyakati hizi.
Mwaka huu maadhimisho ya Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani yanaadhimishwa karibu sana na Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 yanayoanza kutimua vumbi huko Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1- 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Sherehe zote mbili zinagusia “haraka” ambayo Bikira Maria alipanga kumtembelea binamu yake Elizabeti, mwaliko kwa watu wa Mungu kutafakari dhamana na wajibu unaowaunganisha vijana na wazee. Mwenyezi Mungu kwa njia ya mahusiano na mafungamano kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee, wanatambua kwamba, wameitwa kukuza na kudumisha kumbukumbu na kutambua uzuri wa kuwa ni sehemu ya historia kubwa zaidi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, urafiki na wazee unaweza kuwasaidia vijana kuona maisha yao si tu kwamba, ni jambo la mpito na kwamba, si kila kitu kinawategemea wao na uwezo wao. Kwa wazee, uwepo wa kijana katika maisha yao unaweza kuwapa matumaini kwamba, uzoefu wao hautapotea na kwamba, ndoto zao zinaweza kupata utimilifu. Hija ya Bikira Maria kwa binamu yake Elizabeti na ufahamu wao wa pamoja kwamba, huruma ya Mungu ni kutoka kizazi hata kizazi, inawakumbusha waamini kwamba, peke yao, hawawezi kusonga mbele, sembuse, kujiokoa na kwamba, uwepo wa Mwenyezi Mungu ni sehemu ya historia ya watu. Bikira Maria aliyatamka haya katika utenzi wake wa “Magnificat”, akielezea furaha yake inavyopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliyefanya nguvu kwa mkono wake, akawatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao, amewaangusha wakuu kutoka katika viti vyao vya enzi; na wanyonge amewakweza; wenye njaa amewashibisha mema, na wenye mali amewaondoa mikono mitupu, amekumbuka rehema zake kama alivyowaambia Baba zetu, Ibrahimu na uzao wake. Rej. Lk. 1: 51-55.
Waamini wajitahidi kufahamu utendaji wa Mungu, kwa kukumbuka kwamba, Mwenyezi Mungu anakusudia maisha ya waja wake, yafikie utimilifu na kwamba, matumaini na ndoto za maisha zinapitia mchakato wa ukuaji na ukomavu katika majadiliano pamoja na mahusiano na watu wengine, changamoto na mwaliko wa kuondokana na upofu unaojikita katika fedha, mali na usasa, kwani Mwenyezi Mungu hatendi kwa jinsi hii. Mpango wa upendo wa Mungu unakumbatia na kuviunganisha vizazi; unajumuisha na kuwasaidia watu kusonga mbele. Huu ni mwaliko kwa vijana kuwa tayari kujiondoa katika tafakuri ya muda mfupi ambayo inaweza kuwazuia kufanya kitu chenye tija. Wazee wanahamasishwa kutopoteza nguvu zao za kimwili na kuanza kufikiri kwa majuto juu ya fursa na nafasi walizokosa au kupoteza na badala yake, Baba Mtakatifu anawahimiza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, huku wakiruhusu neema ya Mwenyezi Mungu kuwaunda upya. Hii ni neema ambayo kutoka kizazi hadi kizazi inamkomboa mwanadamu kutoka katika hofu na kuwaza ya zamani! Katika mkutano kati ya Bikira Maria na binamu yake Elizabeti; kati ya vijana na wazee, ni mikutano inayofungua mbele ya macho ya waamini mwanzo wa wokovu katika kukumbatiana kwao katika hali ya ukimya, huruma ya Mungu inaleta wingi wa furaha katika historia ya maisha ya mwanadamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutafakari juu ya mkutano huu, kwa kuweka mbele ya macho yao, picha inayoonesha ishara ya kukumbatiana kati ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na binamu yake Elizabeti, Mama wa Yohane Mbatizaji na hivyo kuitengeneza katika akili na nyoyo zao kama umbo lenye kuleta mvuto!
Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kutowaacha wazee katika upweke wao, kwani uwepo wao katika familia na jamii ni wa thamani kubwa, kwa sababu binadamu wote wanashiriki urithi huo huo na ni sehemu ya watu waliojitolea kuhifadhi mizizi yake. Kutokana na uwepo wa wazee, waamini wamepokea zawadi ya kuwa ni watu watakatifu wa Mungu. Kanisa na jamii katika ujumla wake, linawahitaji wazee kwa sababu wanarithisha ya kale ambayo yanahitajika ili kujenga ya mbeleni kwa siku zijazo. Huu ni mwaliko kwa kushirikiana na kushikamana na wazee; kwa kuwaheshimu na kuwathamini na kamwe wazee wasitelekezwe pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Maadhimisho ya Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani ni ishara ndogo lakini yenye thamani ya matumaini kwao na kwa Kanisa zima. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuifanya siku hii kuwa ni fursa ya kukutana kwa furaha na upya kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee. Baba Mtakatifu anawaalika vijana wanaojiandaa kuadhimisha Siku ya Vijana Ulimwenguni katika ngazi mbalimbali, kuanza maadhimisho hayo kwa kuwatembelea babu, bibi na wazee wanaoishi peke yao. Sala na maombi yao, ni zawadi na amana kubwa na kwamba, ndani mwa vijana watabeba baraka na neema ya kukutana na wazee hawa. Baba Mtakatifu anawaalika wazee kuwasindikiza vijana wa kizazi kipya wanaojiandaa kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani kuanzia tarehe 1-6 Agosti 2023 huko Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno. Vijana ni jibu la maombi ya wazee kwa Mwenyezi Mungu, matunda ya kazi waliyoipanda, ishara na kielelezo kwamba, Mwenyezi Mungu hawaachi waja wake, lakini daima huwahuisha upya kwa ubunifu wa Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani kwa mwaka huu wa 2023 anawatakia heri na baraka zinazobubujika kutoka kwenye kumbatio kati ya Bikira Maria na Elizabeti, ili liwajaze amani na hatimaye, anatoa baraka zake za kitume.