Hija ya Kitume ya Papa Francisko Sudan ya Kusini: Hotuba ya Askofu Justin Welby: Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kuanzia tarehe 3 hadi tarehe 5 Februari 2023 viongozi wa Makanisa wanatembelea Sudan ya Kusini, kielelezo cha hija ya uekumene wa amani na watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Hija inanogeshwa na kauli mbiu “Wote wawe na umoja” Yn 17:21, hiki ni kielelezo cha ushuhuda wa kiekumene, udugu wa kibinadamu, mwaliko wa upatanisho na ujenzi wa umoja wa Kitaifa. Viongozi hawa ni Baba Mtakatifu Francisko, Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland. Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani katika hotuba aliyotoa Ijumaa tarehe 3 Februari 2023 kwa viongozi wa Serikali, vyama vya kiraia pamoja na wanadiplomasia na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa nchini Sudan ya Kusini amekazia: Umoja wa watu wa Mungu, ujenzi wa amani na mshikamano; mateso ya watu wa Mungu nchini Sudan licha ya mikataba na makubaliano ya amani ya mwaka 2019. Hija ya uekumene wa amani isaidie kuganga na kuponya madonda ya vita na utengano, ili kwa pamoja waweze kujenga Kanisa kama familia ya Mungu kwa kuwajibikiana. Askofu mkuu Justin Welby anasema, alibahatika kutembelea Sudan ya Kusini kwa muda wa siku tano mwishoni mwa mwezi Januari 2014. Alipata fursa ya kujionea madhara ya vita, mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu, alijionea pia utajiri, amana na rasilimali kubwa nchini Sudan ya Kusini, bila kusahau matumaini ya vijana wa kizazi kipya.
Askofu mkuu Welby amekuwa na ndoto ya kutaka kutembelea tena Sudan na Kusini na kwa sasa ndoto hii imetimia kwa wakuu wa Makanisa kutembelea Sudan ya Kusini, ili kujibu changamoto ya Kristo Yesu aliyewataka wafuasi wake “Wote wawe na umoja” Yn 17:21. Hii ni ndoto ambayo walitamani kuitekeleza kunako mwaka 2019, wakasali na kumwachia nafasi Roho Mtakatifu kutenda kadiri ya huruma yake. Kama kielelezo cha unyenyekevu kwa ajili ya kuomba amani Sudani ya Kusini, Baba Mtakatifu Francisko mwaka 2019 aliwapigia magoti viongozi wa kisiasa Sudan ya Kusini, na sasa baada ya miaka mitano, wanarejea tena kupiga magoti kama kielelezo cha huduma, ili kuwasikiliza na kusali pamoja nao. Wamefika nchini Sudan ya Kusini ili kuwatia shime waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika mchakato wa ujenzi wa amani na umoja wa Kitaifa nchini Sudan ya Kusini. Wamekuja kuwasikiliza vijana na kuwaambia vìongozi wa kisiasa matumaini yao ya amani na fursa zilizopo, wamekuja kuwatia shime wanawake hata katika shida na mahangaiko yao, bado wameendelea kuwa ni kielelezo cha matumaini katika maisha ya ufufuko, ili wanadiplomasia waliopo nchini Sudan ya Kusini waweze kutambua yale yanayoendelea kujiri, na wao kuendelea kuwa na matumaini ya mabadiliko katika maisha ya watu wa Mungu Sudan ya Kusini.
Utashi wa kisiasa ulioneshwa kunako mwaka 2019 haujatekelezwa, jambo linalomsikitisha sana Askofu mkuu Justin Welby kwani watu wateule wa Mungu kutoka Sudan ya Kusini na historia yao inafahamika sana na sala zao zinamfikia Mwenyezi Mungu. Viongozi hawa wamekuja kusali na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumwokoa mwanadamu kutoka katika lindi la kifo na mauti. Wamekuja kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoa wahusika na wadau wakuu, ili wote wawe na umoja. Hija hii ya uekumene wa amani isaidie kuganga na kuponya madonda ya chuki na vita, ijenge na kuimarisha umoja wa Kanisa kama familia, kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao.