Papa akumbuka Siku ya UKIMWI Duniani na kuomba sala kwa ajili ya safari ya kitume
Na Sr Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe Mosi Desemba 2021 mara baada ya katekesi yake amekumbusha Siku ya Ukimwi Duniani, inayoadhimishwa kila ifikapo tarehe 1 Desemba na kusema kuwa ni tukio muhimu la kukumbuka watu wengi walioathiriwa na virusi hivi, ambao wengi wao katika baadhi ya maeneo ya dunia, upatikanaji wa matibabu muhimu kwa bahati mbaya haupatikani. Akitoa salamu kwa vikundi vya mahujaji wa Italia waliokuwapo katika ukumbi amesema: "Ninatarajia kujitolea kwa upya kwa mshikamano ili kuhakikisha huduma ya afya ya haki na yenye ufanisi." Ombi la Papa linaakisi mada ya 2021 ya Siku ya UKIMWI Duniani, ambayo ni, "Komesha ukosefu wa usawa. Kukomesha UKIMWI. Komesha Magonjwa ya Mlipuko.”
Onyo kutoka kwa UNAIDS
Wakati huo huo shirika la kimataifa linalishughulikia suala hili la virusi vya ukimya ( UNAIDS) lilitoa onyo kali kwamba ikiwa viongozi watashindwa kukabiliana na ukosefu wa usawa dunia inaweza kukabiliwa na vifo milioni 7.7, vinavyo husiana na UKIMWI katika kipindi cha miaka 10 ijayo. Katika taarifa yake, shirika hilo la Umoja wa Mataifa pia lilionya kwamba ikiwa hatua za mageuzi zinazohitajika kukomesha UKIMWI hazitachukuliwa, ulimwengu pia utaendelea kukwama katika janga la COVID-19 na kubaki bila kujiandaa kwa milipuko ijayo.
Ziara ya kitume huko Cyprus na Ugiriki
Baba Mtakatifu Francisko pia amewakumbusha waamini kwamba anajiandaa kusafiri, tarehe 2 Desemba 2021, kuelekea Cyprus na baadaye kuelekea Ugiriki, “kuwatembelea watu wapendwa wa nchi hizo, wenye historia nyingi, kiroho na ustaarabu". Alizitaja ziara hizo kuwa ni safari ya kuelekea katika vyanzo vya imani ya kitume na udugu kati ya Wakristo wa madhehebu mbalimbali.