MAP

Papa Francisko anawapongeza vijana kwa kuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea mazingira nyumba ya wote. Papa Francisko anawapongeza vijana kwa kuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea mazingira nyumba ya wote. 

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Vijana na Mazingira: Ndoto na Miradi

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake aliowatumia kwa njia ya video, anapenda kuwapongeza vijana kwa kuwa na ndoto na miradi; kwa kuweka nia ya kutaka kujenga na kudumisha mafungamano ya kijamii sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Lengo ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanayojikita katika mfumo mpya wa elimu kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni changamoto inayojikita katika kanuni maadili na utu wema sanjari na misingi ya haki na amani kwani mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Francisko anavyofafanua katika Waraka wake wa Kitume wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Utunzaji bora wa mazingira ni sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki kwani uharibifu wa mazingira ni kati ya vyanzo vikuu vya umaskini, magonjwa, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Jamii inayotunza na kuheshimu mazingira, hiyo inaweza kudumisha furaha, amani, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Uharibu wa mazingira unahitaji toba na wongofu wa kiikolojia, ili kuleta mageuzi makubwa katika maisha ya mwanadamu kwa kuwajibika katika utunzaji wa nyumba ya wote. Vijana wanaonekana kucharuka katika mchakato wa kutaka kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote! Kuanzia tarehe 1 hadi 28 Septemba 2021 kumekuwa kukifanyika semina ya vijana na mazingira “Youth4Climatechange” kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii, kwa kufanya upembuzi yakinifu kuhusu nafasi na dhamana ya vijana wa kizazi kipya katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira. Vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia wamekuwa wakishiriki katika semina hii huko Milano, Kaskazini mwa Italia.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake aliowatumia kwa njia ya video, anapenda kuwapongeza vijana kwa kuwa na ndoto na miradi; kwa kuweka nia ya kutaka kujenga na kudumisha mafungamano ya kijamii sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.  Lengo ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni mwelekeo unaotoa changamoto kwa ulimwengu wa watu wazima, kwa sababu vijana wameonesha kwamba wanataka: kusikiliza, kutekeleza, kuanzisha mchakato wa majadiliano na hatimaye kuwa na uelewa wa pamoja. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii, kuwatia shime vijana wa kizazi kipya kuendeleza elimu ya mafungamano, ili waweze kujijenga zaidi katika ukomavu, ili kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kwa kawaida, Jumuiya ya Kimataifa inapenda kusema, vijana ni matumaini ya baadaye, lakini, katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, vijana wanaonekana kwa sasa kushika hatamu!

Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” ulioanzishwa kunako mwaka 2019 unatekelezwa kwenye nchi mbalimbali, kwa kuwekeza nguvu zaidi na vipaji ili kuanzisha mchakato wa ushirikiano na vyama vya kiraia ili kuleta mageuzi. Mafundisho Jamii ya Kanisa kadiri ya Ufunuo wa utu mpya ndani ya Kristo Yesu unaiwezesha jamii kujenga msingi thabiti pamoja na kuwa na rejea makini zinazonesha dira na mwongozo wa kufuata wakati wa dharura. Uwekezaji huu unafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa, katika mafungamano ya mshikamano na udugu wa kibinadamu, ambayo ni wazi, ili kuhakikisha kwamba watoto na vijana wanapata elimu bora kadiri ya utu na heshima ya binadamu, ili kutekeleza wito wake wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Ni wakati wa kuangalia ya mbeleni kwa ujasiri, matumaini, haki na amani. Elimu maana yake ni mchakato unaowajengea wanafunzi matumaini ya kuondokana na ubinafsi wao; kwa kutambua, kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza, ili hatimaye kujenga na kudumisha: utamaduni wa ukarimu, mshikamano, mafungamano na hofu ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ndio mwelekeo mpya wa mfumo wa elimu unaotaka kuleta mabadiliko makubwa ya kihistoria yanayomgusa mwanadamu kama inavyojidhihirisha katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Jumuiya ya Kimataifa inahitaji majibu muafaka ya kiteknolojia na kisiasa yanayofumbatwa na uwajibikaji wa kila mwananchi na mfumo wa utamaduni na maendeleo fungamani ya binadamu. Udugu wa kibinadamu, mafungamano ya kijamii na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee, ili kustawisha utulivu na kuendeleza mazingira ili yaweze kuwa bora zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake kwa vijana na mazingira kwa kusema, hakuna sababu ya kujenga uadui wala kuangaliana kwa shingo upande, kwani wote ni sehemu ya ulimwengu unaopaswa kusimikwa katika amani na utulvu. Changamoto zote hizi zisaidie kupata suluhu ya umaskini wa nishati, kwa kulinda na kudumisha amana na utajiri wa nchi; uzalishaji endelevu; uchumi shirikishi pamoja na teknolojia rafiki kwa mazingira. Huu ni wakati wa kufanya maamuzi magumu, ili uzoefu na mang’amuzi yaliyojitokeza kwa miaka ya hivi karibuni, yaweze kuunda utamaduni wa jamii inayowajibika na kushirikishana.

Papa Vijana na Mazingira

 

30 Septemba 2021, 16:17