Hija ya Kitume ya Papa Francisko Nchini Iraq: Ibada Kwa B. Maria
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Iraq, kuanzia Ijumaa tarehe 5 hadi Jumatatu tarehe 8 Machi 2021 imenogeshwa na kauli mbiu “Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu” Mt. 23:8. Hii ni hija ambayo ilifumbata mambo makuu matatu: Ukaribu wa Baba Mtakatifu kwa Wakristo nchini Iraq, uhamasishaji wa ujenzi wa Iraq mpya katika haki na usawa na kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene ili kudumisha udugu wa kibinadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu akiwa nchini Iraq, amekuwa ni hujaji wa toba, ili kumwomba Mungu msamaha na kuanza mchakato wa upatanisho wa kitaifa. Amekuwa hujaji wa amani ili kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Na amebahatika kukutana mubashara na Kanisa la mashuhuda wa imani, ili kunogesha hija ya matumaini.
Kama sehemu ya desturi na utamaduni wake, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu mchana tarehe 8 Machi 2021 baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Ciampino ulioko mjini Roma amekwenda moja kwa moja kutembelea na kusali kwenye Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” iliyoko kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, lililoko Jimbo kuu la Roma. Lengo lilikuwa ni kumshukuru Bikira Maria kwa maombezi, ulinzi na tunza yake ya Kimama wakati wote wa hija yake ya kitume ya 33 huko nchini Iraq, ambako alikwenda kama hujaji wa toba, amani, imani na matumaini ili kuweza kunogesha fadhila hizi katika maisha ya watu wa Mungu nchini Iraq. Ameweka shada la maua kutoka Iraq. Itakumbukwa kwamba, hata kabla ya kuondoka kwenda Iraq, Baba Mtakatifu alikwenda kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu na kujikabidhi katika ulinzi na tunza yake ya Kimama!
Falsafa ya Neno Asante ni kuomba tena! Wachunguzi wa mambo wanasema, Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu lililoko Jimbo kuu la Roma ni kati ya Makanisa ambayo Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ameyatembelea mara nyingi zaidi kwa ajili ya sala ya binafsi: kuomba na kushukuru kila wakati anapoadhimisha matukio makuu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Bikira Maria ni mfano na kielelezo cha imani, matumaini na mapendo, kwani amediriki kuwa ni mfuasi amini wa Kristo Yesu na chombo cha huduma makini kwa jirani zake; mtindo na mfumo wa maisha unaopaswa kutekelezwa na waamini wote kama sehemu ya mchakato wa majiundo yao ya awali na endelevu ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, ili aweze kuwasaidia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, kielelezo cha imani tendaji.
Baba Mtakatifu anasema, ikiwa kweli waamini wanataka kuwa wafuasi amini wa Kristo Yesu na Kanisa lake; ili kuguswa na kuponywa na huruma pamoja na upendo wa Mungu, wanapaswa kuzingatia mambo makuu yafuatayo: Fumbo la Msalaba, Ekaristi Takatifu na Ibada ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Bikira Maria ni Mama wa Mungu na Kanisa, kwani ndani ya Moyo wake safi usiokuwa na doa, watu wote wanapata utambulisho wao, kwa kupenda na kupendwa, hali inayoonesha uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Mama wa Mlango wa Mbinguni, ametangazwa kuanzia sasa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni “Bikira Maria Mama wa huruma na matumaini”. Ni Mama ambaye daima ameonesha ulinzi na tunza kwa watu wanaomkimbilia katika shida na mahangaiko yao; upendo ambao umeendelezwa hadi nyakati hizi. Bikira Maria ni dira na kielelezo cha njia ya kwenda mbinguni; Njia ambayo kamwe haiwezi kumpotezesha mtu mwelekeo wa maisha! Njia hii, ni Kristo ambaye pia ni ukweli na uzima. Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani.
Bikira Maria, nyota ya asubuhi anawaongoza waamini kwa Kristo Yesu, ambaye ni Lango la huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anasema, kunako mwaka 2015, Kanisa liliadhimisha Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu. Huu ni mwaka ambao umewawezesha waamini wengi kuvuka Lango la Huruma ya Mungu, ili kuonja upendo unaofariji, unaosamehe na kutoa matumaini. Hii ndiyo hamu inayopaswa kushuhudiwa na watu wote kwa kuwaonjesha jirani zao wema na huruma ya Mungu katika maisha yao. Bikira Maria Mama wa huruma na matumaini, asaidie watu kusambaza na kueneza wema na huruma ya Mungu kama njia ya kuganga na kuponya madonda yanayomwandama mwanadamu, tayari kusimama na kupiga moyo konde, ili kusonga mbele kwa neema na baraka ya Mungu.
Baba Mtakatifu anawataka waamini kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amejishusha ili kuwaokoa, mwaliko kwao pia ni kujishusha na kuwainamia jirani zao wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali, kwa kuwa na jicho la huduma kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, ili kuwaonjesha watu wanaoteseka, ile “divai ya furaha”, kama ilivyotokea kwenye Arusi ya Kana. Bikira Maria awe ni mfano na kielelezo cha wanawawake wote ambao wamekuwa kweli ni tabernakulo ya Injili ya uhai, ili kuwaheshimu na kutambua dhamana, wito na utume wao kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Hata katika ukimya wao, wanawake ni nguvu ya matumaini.