Hija ya Papa Francisko Msumbiji: Injili ya Msamaria mwema! DREAM
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Msumbiji kwenye hija yake ya Kitume, Ijumaa tarehe 6 Septemba 2019 ametembelea Hospitali ya “Santo Egidio de Zimpeto” iliyozinduliwa tarehe 7 Juni 2018. Inaendesha mradi mkubwa wa kuzuia maambukizi ya Ugonjwa wa Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto unaojulikana kama “DREAM” yaani “Disease Relief Through Excellent and Advanced Means”. Mradi wa “The Dream” unapania kutoa dawa za kurefusha maisha sanjari na kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama kwenda kwa mtoto unaendelea kuonesha mafanikio makubwa Barani Afrika. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inakuwa na kizazi ambacho hakina virusi vya Ukimwi. Mradi huu pia unawajengea uwezo wa kiuchumi waathirika wa Virusi vya Ukimwi, ili kujitegemea na kuzisaidia familia zao kusonga mbele kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa. “The Dream” utaendelea kuonesha maajabu katika mapambano dhidi ya Ukimwi, ikiwa kama Serikali, Mashirika na Wafadhili binafsi, wataendelea kushikamana na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio katika kutekeleza Malengo na Mikakati yake ya Maendeleo.
Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amejikita zaidi kuhusu Injili ya Msamaria mwema ili kusikiliza na kujibu kilio cha wagonjwa wa UKIMWI, kwa njia ya ushauri nasaha pamoja na tiba dhidi ya magonjwa nyemelezi, ili kuwajengea waathirika wa UKIMWI matumaini ya kusonga mbele na maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza wafanyakazi pamoja wagonjwa wote, lakini kwa namna ya pekee kabisa wagonjwa walioathirika kwa Virusi vya Ukimwi, hali iliyomfanya kutafakari kwa kina Injili ya Msamaria mwema, mutasari wa historia ya ukombozi inayojikita katika ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa maskini. Kumpenda Mungu ni kuishika imani: kumkiri Kristo na kushikamana naye katika maisha ili kuufikia utimilifu wa upendo halisi ambao ni Mungu mwenyewe. Huu ni upendo unaovuka vikwazo vya utengano na matabaka ya kijamii. Msamaria mwema ni kielelezo cha upendo unaojipambanua katika kiini chake cha kweli, huduma na wokovu.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, kishawishi kikubwa dhidi ya mapambano ya UKIMWI duniani ni kukata tamaa kwamba, hakuna linaloweza kufanyika dhidi ya UKIMWI. Lakini kuna kilio cha wanawake na watoto wanaoendelea kuathirika kwa ugonjwa wa UKIMWI; watu wanaosukumizwa pembezoni pamoja na kutengwa na jamii. Hospitali hii ni kwa ajili ya wagonjwa wa: Kifua kikuu, wagonjwa wa Saratan na watoto wanaoteseka kwa utapiamlo wa kutisha. Hospitali ya “Santo Egidio de Zimpeto” ni kielelezo cha huruma na upendo wa Kristo unaowahakikishia wale wote wanaolia na kuomboleza, uwepo wake endelevu kwa njia ya huduma makini inayotolewa na ndugu zao katika Kristo Yesu; watu wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza ili kusikiliza na kujibu kilio cha maskini kwa njia ya kinga na tiba hata kama bado haitoshelezi mahitaji ya wagonjwa; lakini jambo la msingi ni kwamba, utu, heshima na haki msingi za wagonjwa zinalindwa na kudumishwa sanjari na kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Mradi huu ni mfano hai wa fadhila ya unyenyekevu unaotambua uwezo na udhaifu wa binadamu; pamoja kuendeleza kipaji cha ubinifu.
Hospitali ya “Santo Egidio de Zimpeto” ni kielelezo cha imani tendaji na mshikamano wa kiutu, ili kupambana na umaskini kwa njia ya upendo wa Kiinjili ili kuweza kujibu kilio cha maskini na kujitosa kimaso maso katika huduma inayomwilishwa katika sekta mbali mbali Hospitalini hapo. Zaidi ya wafanyakazi 5000 wa sekta ya afya wameshiriki katika kutoa mafunzo; tiba na kinga kama ushuhuda wa tunu msingi za kiutu na Kiinjili. Huduma ya utunzaji wa Injili ya uhai inakwenda sanjari na utunzaji bora wa mazingira, kwani haya ni mambo yanayoambatana na kukamilishana kama inavyojionesha kwenye vinyago vya “Ujamaa” kama vilivyochongwa na Wamakonde. Baba Mtakatifu anakazia umoja na mshikamano wa dhati ili kulinda na kutunza mazingira; kwa kukusanya na kuhifadhi maji, ili kudhibiti athari za uchafuzi wa mazingira.
Injili ya Msamaria mwema inahitimishwa kwa kumpeleka yule mgonjwa ili aweze kutunzwa. Hospitali ya “Santo Egidio de Zimpeto” imewasaidia watoto zaidi ya 100, 000 wanaoweza kuandika kurasa mpya za historia ya maisha yao, wakiwa hawana maambukizi ya Virusi vya UKIMWI. Watoto hawa wanaweza kutabasamu kwa sababu wametibiwa kwa heshima na utu wao umethaminiwa na kwa sasa ni alama ya matumaini kwa watoto wengine, mfano bora wa kuigwa katika ukarimu. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wale wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, watalipwa na Kristo Yesu atakapokuja mara ya pili. Huu ni ujumbe wa chemchemi ya furaha kwa sababu watoto hawa wamebarikiwa sana machoni pa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kusema, Hospitali ya “Santo Egidio de Zimpeto” ni chemchemi ya matumaini mapya!