MAP

2025.08.25 Misa Takatifu ya kufunga Kongamano la 6 kitaifa la vijana wakatoliki wafanyakazi(VIWAWA) huko Mbeya,Tanzania(23 Agosti 2025). 2025.08.25 Misa Takatifu ya kufunga Kongamano la 6 kitaifa la vijana wakatoliki wafanyakazi(VIWAWA) huko Mbeya,Tanzania(23 Agosti 2025). 

Tanzania,Askofu Mapunda kwa VIWAWA:tutende haki,wewe uishi na uwaache wengine waishi!

“Heri wenye njaa na kiu ya haki maana hao watashibishwa.”Haki ni sifa ya Mungu,haki ni fadhila ya kimungu.Maandiko Matakatifu yanatuambia Mungu ni mwenye haki.Ni kutoka katika mahubiri ya Askofu Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida na Mwenyekiti wa Idara ya Kichungaji ya Walei,Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC)wakati wa hitimisho la Kongamano la 6 Kitaifa la VIWAWA lililofanyika huko Mbeya Tanzania.Askofu alihimiza vijana "kutenda na kulinda haki kwani bila haki hakuna uhai."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kurudi nyumbani wamebadilikia kiroho na kimwili, kudumisha haki yenye sifa ya Mungu na fadhila ya kimungu; kuelekea uchaguzi Mkuu kwa kuomba haki na amani itawale, vijana kujitambua wenyewe na mengine mengi, yaliibuka katika mahubiri ya  Askofu Edward Elias Mapunda, wa Jimbo Katoliki la Singida, na Mwenyekiti wa Idaya ya Utume wa Kichungaji kwa ajili ya Walei ya Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania(TEC), wakati akiongoza Ibada ya Misa Takatifu ya kufunga Kongamano la VI Kitaifa, la Vijana  Wakatoliki wafanyakazi(VIWAWA) tarehe 23 Agosti 2025, lililofanyika katika Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya nchini Tanzania.

Misa ya Kufunga Kongamano la Viwawa Tanzania
Misa ya Kufunga Kongamano la Viwawa Tanzania

Askofu Mapunda katika mahubiri yake alianza kusema kuwa: “Heri wenye moyo safi maana hao watamwona Mungu, heri wenye njaa na kiu ya haki maana hao watashibishwa.” Wapendwa mahujaji katika matumaini, mapendo…! Daima…! Leo kwa neema ya Mungu tunahitimisha Kongamano letu la VI la VIWAWA Taifa, hapa katika Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya. Kongamano letu limeongozwa na kauli mbiu: “Jubilei Ishirini ishirini na tano…! Mahujaji katika matumaini...! Naomba tumpe Mungu sifa, shukurani na utukufu kwa kufanikisha Kongamano letu…! Hongereni sana Mahujaji katika matumaini. Mwambie jirani yako, hongera sana…! Naamini Kongamano letu linatupatia wakati mzuri, wakati wa kusali na kutafakari maisha yetu ya kiroho, kutafakari uhusiano wetu na Mungu na binadamu wenzetu, kujitambua na kuutambua utume wetu na nafasi yetu kama vijana katika Kanisa, katika familia zetu, jamii inayotuzunguka na taifa.

"Turudi majimboni kwetu kwa roho mpya na kimwili"

Naamini hatutarudi majimboni kwetu kama tulivyofika, tunarudi tukiwa wapya kiroho na kimwili; si ndio…?  Tunarudi tukiwa na baraka, neema tele,  nguvu na bidii ya kitume na kimisionari. Hongereni sana…! Mki rudi msiende kuishi kama kijana ambaye hakushiriki Kongamano hili, onesha tofauti wewe umetoka Hija, wewe ni hujaji, umeiva na kukomaa katika imani na mwisho wa adhimisho hili la Sadaka ya Misa Takatifu, tutapokea rehema kamili. Ninaomba tumshukuru Mungu.

"Kuungana na wakristo kuomba haki na amani"

Ndugu zangu, leo tunaungana na Wakristo wenzetu, kuomba haki na amani. Katika Injili, Yesu ametuambia “Heri wenye njaa na kiu ya haki maana hao watashibishwa.” Haki ni sifa ya Mungu, haki ni fadhila ya kimungu. Maandiko Matakatifu yanatuambia Mungu ni mwenye haki. Mungu ni hakimu mwenye haki. Tunaposalimiana sisi wa dini mbalimbali Tanzania, nadhani mnafahamu tunavyo salimiana. Naomba nikisema mtaitikia kama mnajua, dini mbalimbali…..! Upendo, Haki na amani….! Basi hivyo ndivyo tunavyo salimiana Dini mbalimbali  na tunaitikia: “Upendo, Haki na amani.” Ndugu zangu, amani ni tunda la haki, bila haki hakuna amani. Dunia isiyo na haki ni jehenamu, halikadhalika, familia isiyo na haki ni jehanamu, Kanisa lisilo na haki ni jehanamu Taifa lisilo na haki ni jehanamu. Kwa hiyo tunaungana na Watanzania wenzetu kuomba fadhila ya haki na amani, kama ilivyo, amani.

Askofu Mapunda wakati wa misa ya kufunga Kongamano la Viwawa Tanzania
Askofu Mapunda wakati wa misa ya kufunga Kongamano la Viwawa Tanzania

 

Haki ni nini? Kwa kifupi haki ni kutenda mema, mtu yeyote anayetenda mema maana yake anatenda haki. Yesu ametuambia, “mtendee mwenzako kama wewe unavyotaka kutendewa.” Yesu na Mama Kanisa anatualika sisi sote tuwe vyombo vya haki, vijana muwe vyombo vya haki, mtende haki. Sifa ya kijana ni kutenda haki, muwatendee wengine kama ninyi wenyewe mnavyotaka tutendewe, tutende haki kwenye familia, tutende haki katika mazingira yote. Tunapotenda haki tunaishi fadhila ya kimungu ambayo ni fadhila ya haki. Haki ni wokovu. Wengine wanasema haki yako inaishia pale inapoanza haki ya mwingine. Tutende haki. Haki ni kumtendea binadamu mwenzako kama wewe unavyotaka kutendewa. Haki inayoheshimu uhai. Haki inayolinda utu wa binadamu. Haki inalinda utu, haki inalinda heshima na uhai wa mwanadamu. Bila haki hakuna uhai. Kwa hiyo, tunapotenda haki tunalinda uhai wa wenzetu. Tunaalikwa tutende haki, wewe uishi na uwaache wengine nao waishi.

Kuekelea uchaguzi 2025: "Ufanyike kwa haki na tuliombee Taifa letu"

Tunaelekea kwenye uchaguzi tumeambiwa hivyo Oktoba. Sasa, tunamwomba Mungu ili uchaguzi huo ufanyike kwa haki ndiyo maana tunaomba haki, aliyeshinda ashinde kwa haki na aliyeshindwa ashindwe kwa haki, basi akubali sasa ameshindwa kwa haki, haki itendeke, hilo ndilo tunaloliomba. Na haki itaepusha migogoro mingi, haki inaleta furaha. Haki inaleta upendo na mshikamano wa kweli. Ndugu zangu tusichoke kuliombea taifa letu, tusichoke kuziombea familia zetu na tusichoke kujiombea wenyewe ili tuwe watu wa haki. Kijana uwe mtu wa haki, hii ndiyo iwe sifa yako! Kwa hiyo usikubali kupokea rushwa yoyote;  Usikubali kupokea rushwa wala usikubali kutoa rushwa, rushwa ni adui wa haki. Kama nilivyosema dunia isiyokuwa na ahaki ni jihenamu, inamilikiwa na shetani. Kama hamna haki shetani anatawala, kwa hiyo, sisi tutende haki, na Mama Kanisa anatualika tuwe vyombo vya haki.

Misa ya kufunga Kongamano la Viwawa Tanzania
Misa ya kufunga Kongamano la Viwawa Tanzania

Vijana kujitambua: "wewe ni wa thamani kubwa"

Ndugu zangu Mahujaji katika Matumaini, jambo la msingi ni vijana kujitambua. Ninaomba vijana mjitambue. Wewe ni wa thamani kubwa, hebu mwambie mwenzako wewe ni wathamani kubwa…! Kwa nini wewe ni wa thamani kubwa! Ni kwa sababu Mungu anakupenda, upendo wa Mungu unakuinua wewe kijana na kuwa wa thamani kubwa. Ninaomba umshangilie Mungu kwa kukuinua…! Wewe ni wa thamani kubwa kwa sababu umekombolewa, tena kwa damu Azizi ya Yesu! Mwambie jirani yako umekombolewa kwa damu Azizi ya Yesu. Tumshangilie Yesu...! Mtakatifu Petro anatukumbusha anaposema: “nanyi mfahamu kwamba mmekombolewa si kwa vitu viaribikavyo, kwa fedha au dhahabu ili mpate kutoka katika mwenendo wenu usiyo faa mliyo upokea kwa Baba zenu,  bali kwa damu ya thamani kama ya mwanakondoo asiye na hila, Asiye na waa,  yaani wa Kristo”.

Misa ya Kufunga Kongamano la Viwawa Tanzania
Misa ya Kufunga Kongamano la Viwawa Tanzania

Wewe ni wa thamani kubwa kwa sababu wewe ni Kanisa, wewe kijana, wewe ni Kanisa, Kanisa la Mungu, wewe ni nyumba ya Mungu, wewe ni Hekalu la Roho Mtakatifu. Hapa ndipo ilipo lala thamani yako: “Wewe ni Kanisa la Mungu, wewe ni nyumba ya mungu, wewe ni Hekalu la Roho Mtakatifu, wewe ni wa thamani kubwa kwa sababu Mungu anakaa ndani yako.”Wewe kijana, wewe ni wa thamani kubwa kwa sababu Mungu anakaa ndani yako, ukilitambua hilo kwamba wewe ni Kanisa la Mungu, wewe ni nyumba ya Mungu, wewe ni hekalu na Roho Mtakatifu, Mungu anakaa ndani yako.” Kwa hiyo tambua ulivyo na thamani hiyo kubwa, na ukisha tambua thamani hii hutakata tamaa katika maisha, hutakata tamaa kwa sababu Mungu hakati tamaa, Mungu haja kata tamaa kwa ajili  yako na hatakata tamaa kwa ajili yako. Kwa hiyo na wewe usikate tamaa kwa sababu wewe ni Kanisa, wewe ni Nyumba ya Mungu, wewe ni hekalu la Roho Mtakatifu, na hivyo anakaa ndani yako.

Kongamano la Viwawa Taifa

Sehemu ya Pili ya mahubiri:

Askofu Mapunda kwa VIWAWA II

Sehemu ya Tatu na ya mwisho itafuata...

25 Agosti 2025, 13:11