Tafakari Dominika 19 Mwaka C wa Kanisa! Kesheni!
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo ni Dominika ya 19 MWAKA C wa Kanisa. Tafakari ya leo imebeba ujumbe wa imani ambayo ni msingi na chanzo cha tumaini la kweli na mwanzo wa uzima wa milele kwani hutujalia kuonja furaha na mwanga wa heri ya mbinguni. Ni mwaliko wa kutekeleza vyema nyajibu kwa kutimiza vyema mapenzi ya Mungu na kuendelea kujibidiisha kuufanya ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, ili kudhihirisha Utukufu wa Mungu; kwa kujikita katika moyo wa huduma na kusimama imara katika imani. Hii ni imani yenye matumaini: Kuishi kwa kungoja kwa moyo wa utumishi” Somo I: Hekima 18:6-9 Wana wa Israeli walihifadhi usiku wa Pasaka kwa matumaini, wakimngojea Mungu awaokoe kama alivyoahidi. Walimwamini Mungu aliye mwaminifu kwa ahadi zake. Somo II: Waebrania 11:1-2, 8-1 Imani ni "kuamini pasipo kuona." Abrahamu ni mfano: alitii, alihama, aliishi kama mgeni, alimtolea Mungu mwanawe kwa imani. Hii ni imani inayochangia tumaini na uvumilivu wa safari ya wokovu. Injili: Luka 12:32-48 Yesu asema: "Msiogope, enyi kundi dogo; kwa maana Baba yenu amependa kuwapa Ufalme." Anafundisha kuhusu uaminifu katika kungoja kurudi kwa Bwana, na anatufundisha wajibu wa kuwa watumishi waaminifu. Mwanadamu anapaswa kuona udogo na udhaifu alionao akizingatia kuwa dunia na yaliyomo ikiwamo maisha yake ni mali ya Mungu na kwamba atayatolea hesabu, katika mazingira hayo mwito uwe “kufunga viuno na kuwasha taa” kadiri ya agizo la Kristo leo. Katika ulimwengu unaokumbwa na vita, ukosefu wa haki, kukata tamaa, na hofu kuhusu kesho, masomo haya yanatupatia dira mpya Tumaini linajengwa juu ya imani thabiti, si hali ya nje. Watu wa Mungu ni wanaosubiri kwa bidii na utulivu, si kwa hofu. Uaminifu wa kila siku unahesabiwa mbele za Mungu.
Juma lililopita yaani dominika ya 18 ya Mwaka C tulitafakari hatari ya kuweka nafsi zetu: roho, akili, utashi na mwili katika mali, kumwacha Mungu na kutojali watu. Leo Kristo anatufundisha kuwa kusudi tusipate hatari hiyo ya kufariki ghafla na kuwa tayari kwa ufalme wa mbinguni tunapaswa kukesha. Maandalizi hayo yanatudai uaminifu sababu ‘Bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyoijua...’, Mkesha wetu uweje? tufanye nini tunapokesha? Namna ya kukesha, namna ya kufunga viuno na namna ya kuwasha taa tunaipewa na somo la piliII (Ebr 11:1-2,8-19) imani thabiti. Somo la pili linatufundisha kuwa Abrahamu hakuishi tu kwa imani, bali alitembea na imani – alihama, alitarajia mtoto akiwa mzee, alijitolea hata kumtoa mwanawe. Imani yake ilikuwa ya matendo na ya kungoja kwa moyo wa utiifu. Je, mimi huendelea kungoja kwa utii hata nisipoona matokeo mara moja? Imani, ni hakika ya mambo yatarajiwayo, bayana ya yasiyoonekana.. Imani ni jibu la mwanadamu kwa ufunuo wa Mungu, tena ni njia pekee inayotuongoza katika upendo na muungano na Mungu. Imani ni kinasaba (DNA) kinachotuingiza ukoo wa kimbingu na warithi pamoja na Kristo.. Tukiisha kuipokea imani yatupasa kuilinda, kuitunza na kuikuza. Somo hilo limetupata Babu Ibrahim na Sara mkewe kama mfano wa imani na jinsi walivyobarikiwa kwa imani hiyo. Ibrahim ni mfano namba moja wa imani katika Agano la Kale na Mama Bikira Maria katika Agano Jipya.. wote hawakuelewa waliyoambiwa lakini kwa imani walitii na sasa ni watu muhimu katika historia ya wokovu.
UFAFANUZI: Kumbukumbu ya wokovu hutia moyo wa kungoja kwa imani, Katika Kitabu cha Hekima, tunakumbushwa jinsi Waisraeli walivyotunza usiku wa wokovu kwa matumaini. Hii inatufundisha kuwa tumaini halina maana ikiwa hatukumbuki uaminifu wa Mungu wa zamani. Je, mimi hukumbuka neema za Mungu maishani mwangu? Maisha yetu yahusishe kufunga viuno na kuwasha taa kwa kuishika na kuiishi imani, tufanye bidii kuipokea, kuijua, kuiishi, na kuwashirikisha wengine imani yetu inayotishiwa na changamoto kadha wa kadha. Mosi ni uwepo wa vikundi vya wabatizwa vilivyopoteza hamu na ladha ya imani, kuna ubaridi wa imani, kutopendelea mambo ya dini, mtazamo kwamba maoni binafsi ndio msingi na kipimo cha maadili na maamuzi ya maisha binafsi na kutukuza malimwengu. Pili, tatizo la ushirikina bado ni kubwa hata miongoni mwa wabatizwa, sababu ni nyingi ikiwapo tamaa ya mali.. pia umasikini unaosababishwa na kukosa elimu, afya njema, ulinzi na maisha bora. Tatu, ongezeko la wakana Mungu, hawa ni wasomi walioathiriwa na umagharibi na umashariki. Huenda kukosekana kwa malezi ya kina, ukaidi wa kutofuata mafundisho yanayojenga na usasa vimepelekea hali hii. Sote tutafakari na kuchukua uamuzi madhubuti wa kuishi imani yetu kikamilifu, huko ndiko kuweka hazina mbinguni, ndiko hasa kufunga viuno na kuwasha taa. Nne ni upinzani dhidi ya wakreli (anti-clergy) na uana-harakati wa walei, kudunisha nafasi ya wakreli na kusawazisha mafundisho na maamuzi ya magisterio kwa kivuli cha maendeleo na uelewa na hivi kuifanya imani kuwa jambo la kawaida tu linalofuata maoni na mapendekezo ya kila mtu.
Yesu anawaambia wanafunzi wake: "Msiogope… Baba yenu amependa kuwapa Ufalme." Kisha anasisitiza umuhimu wa kuwa tayari, wa kuishi kama watumishi waaminifu wanaongoja bwana wao arudi.Tumaini halimaanishi tu kukaa bila kufanya kitu – linamaanisha kufanya kazi kwa uaminifu huku tukingojea kwa tumaini. Katika Jubilei hii ya Matumaini, tunaalikwa kuwa, Watu wa kumbukumbu ya wokovu, Tujifunze kuona alama za uaminifu wa Mungu maishani mwetu.Mashahidi wa imani ya vitendo Si kuamini tu, bali kutembea kwa utii hata kwenye giza la maisha. Watumishi waaminifu kwa matumaini – Kila tendo, kila huduma, kila upendo mdogo unahesabika mbele za Mungu. Imani ambayo mwanzo wake ni Mungu mwenyewe inapaswa kuwa hai na endelevu ikipewa pumzi yake na matendo (Yak 2:14-18). Familia zisilegee, zichangamkie malezi ya imani na utu kadhalika mazingira ya kazini na katika jumuiya yashuhudie imani sababu imani siyo tendo la siri bali ni la ushuhuda wenye misingi yake katika upendo, haki, amani, maelewano na matendo ya huruma na ya utii. Imani inaonekana pia katika kuwatendea vizuri tuliokabidhiwa kuwalea na kuwapa posho kwa wakati wake. Kristo anasema heri akitukuta tunafanya hivyo, tusijisahau na kuanza kuwapiga, kula, kunywa na kulewa, tutakatwa vipande viwili! Nyumbani tunao wafanyakazi, tunawatendeaje? wanatumika kwa utumishi mwingi, posho kidogo tu tukidai wanakula na kulala bure, wanaweza kufanywa chochote hata na watoto wadogo kabisa wa wenye nyumba na kutendewa kama kondoo wa kuchinjwa na akina baba wenye tamaa, tukumbuke kilio cha wanyonge kama hawa husikika haraka mbele ya Kiti cha enzi.
Papa Leo XIV amekuwa akisisitiza kuwa “Tumaini si faraja ya kihisia, bali ni msimamo wa kimisionari. Ni uwezo wa kuishi kwa furaha, uaminifu na wema hata bila uhakika wa mara moja.” Katika mwanga wa masomo ya leo, Anahimiza vijana, familia, na viongozi wa Kanisa kuacha hofu na kuishi kwa bidii ya kimisionari. Anaona tumaini kama huduma ya roho, si tu hali ya kusubiri; bali kuchukua hatua, kupenda, kutumikia huku tukimngojea Kristo. Tupo pia walimu, tumekabidhiwa wanafunzi tuwape posho kwa wakati wake yaani kuwashirikisha maarifa na maadili kusudi nao wakue na kufikia kipeo cha ubinadamu wao. Huenda tumejisahau na kulegea katika wajibu huo, tumesisitiza zaidi makuzi ya kiakili kwa wanafunzi wetu na kuacha kuwalea kiroho mintarafu imani na maadili. Tufunge viuno vyetu na tuwashe taa zetu kwa kuwalea katika ujumla wao: mwili, akili na roho.. vinginevyo atakapokuja Bwana katika saa tusiyoijua atatukata vipande viwili na kuweka fungu letu pamoja na wasioamini. Wengine ni viongozi, inafaa kuona upo ofisini kwa dhumuni gani, huduma au maslahi? Je, unawatazama wote katika usawa au kuna wengine unawaangalia kwa jicho moja na wengine kwa macho yote? Changamoto za watu zinajibiwa kwa wakati? Rushwa ina nafasi katika utendaji wako? Kuna muda umetenda kinyume na viapo vyako? Jiwekee hazina mbinguni, pale utakapokuwapo moyo wako. Tupo wanafunzi, tumepewa watumishi watupe posho kwa wakati. Watumishi hao ni walimu, walezi, mazingira ya shule, ratiba za darasani, michezo, kazi na bwenini, vitabu na notes tulizonazo. Je, tunasoma kwa juhudi na maarifa? tunasikiliza na kutenda? Huenda tunajisahau, kudharau au kuona muda bado. Maisha ya baadaye yanategemea msingi tunaouweka sasa, tukijifunza vema leo ndivyo tutakavyotenda baadaye kazini, tuzingatie lengo la uwepo wetu shuleni, ndiko kufunga viuno na kuwasha taa.
Watoto pia tunaalikwa kufunga viuno na kuwasha taa, tufanye mafundisho ili tubatizwe, tupate komunyo na kipaimara. Halafu, tuwahi shule na tuwasikilize walimu kwa utulivu bila kelele, tuwatii wazazi na tufanye wanayotuelekeza, tusiwanyime wenzetu bagia, tucheze pamoja, tusioneane.. Tusipofanya hivi Bwana atakuja saa tusiyoijua, atatukata vipande viwili na kutuwekea fungu letu na wasioamini. Sisi sote tufikiri sana kuhusu imani yetu, tusikilize sana kuhusu imani yetu, tutazame sana yahusuyo imani yetu na tuzungumze sana kuhusu imani yetu. Tujitajirishe kwa kujipa muda mbele ya Yesu wa Ekaristi na mbele ya Msalaba, tujizoeshe kulitaja Jina Takatifu la Yesu, na jina la Bikira Maria, na majina ya watakatifu, tupokee sakramenti, turudi kundini, tusali… angalieni, Bwana wetu atakuja siku tusiyodhani na saa tusiyoijua, atatukata vipande viwili na kutuwekea fungu letu pamoja na wasioamini. Yesu leo anatualika tusiishi kwa hofu, bali kwa matumaini ya kweli. Si matumaini ya kimazoea, bali ya, Kumbukumbu ya wokovu wetu, Imani ya kutembea hata tusipoona, Uaminifu wa kila siku kama watumishi waaminifu, Katika Jubilei hii ya Matumaini, Kanisa linaitwa kuwa “kundi dogo lisiloogopa”, bali linalosubiri kwa bidii, likitenda kwa upendo, likitazama ufalme wa milele.“Msiogope, enyi kundi dogo…” (Lk 12:32) “…heri huyo mtumishi ambaye bwana wake atakapokuja atamkuta akifanya hivyo.” (Lk 12:43). Amina.