Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe,ibada kwa B.Maria:"Aliye na Maria kama mama,ana Kristo kama Kaka"
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe, Padre Mfansiskani Mkonventuali (OFMConv,) alizaliwa kunako Januari 1894 nchini Poland na kifo chake tarehe 14 Agosti 1941. Alikuwa ni Padre, mmisionari na mfiadini wa Poland. Alijitolea kufa badala ya mwanamume mwenye familia aitwaye Franciszek Gajowniczek katika kambi ya kifo ya Wajerumani huko Auschwitz, iliyoko Poland iliyokuwa inakaliwa na Wajerumani wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu.
Kwa njia hiyo hili lilikuwa ni tendo kuu la ushujaa la Kolbe lilitokea wakati wa Vita hivyo ambapo alikuwa akiwakaribisha wakimbizi wengi wa Kiyahudi, huku akionesha dhamira yake ya kulinda wanaokandamizwa na kukuza hadhi ya binadamu. Baadaye alikamatwa na kupelekwa Auschwitz. Huko, mnamo Agosti 1941, mfungwa mmoja alitoroka, jambo lililofanya wasimamizi wa kambi wachague wanaume kumi ambao wangekufa kwa njaa. Kwa kuwa mmoja wa wanaume waliochaguliwa, Franciszek Gajowniczek, alikuwa na familia, Kolbe alijitolea kuchukua nafasi yake. Tendo hili la kustaajabisha la upendo wa kujitoa sadaka liliangazia dhamira isiyoyumba ya Kolbe ya kuiga kutokuwa na ubinafsi kwa Kristo. Kwa majuma mawili, Kolbe na wafungwa wengine waliohukumiwa waliteseka bila chakula au maji. Katika kipindi chote cha jaribu hilo roho ya Kolbe iliendelea kuwa sawa. Hadi leo, maisha yake na mauaji yake yanaendelea kuwatia moyo Wakatoliki wengine wengi wasiohesabika! Katika ulimwengu ambao mara nyingi una sifa ya ubinafsi, historia yake ni ukumbusho wenye kugusa moyo kwamba ukuu wa kweli unatokana na matendo ya upendo na kujisadaka bila ubinafsi.
Kutangazwa kuwa Mtakatifu 1982
Padre Kolbe alikuwa akijishughulisha sana na kukuza ibada ya Bikira Maria Msafi wa Moyo, na alianzisha na kusimamia monasteri ya Niepokalanów karibu na mji wa Warsaw, huku akiendesha kituo cha radio cha amateur (SP3RN), na kuanzisha au kuendesha mashirika mengine na machapisho mengine kadhaa. Kunako tarehe 10 Oktoba 1982, Papa Mtakatifu Yohane Paulo II alimtangaza Padre Kolbe kuwa Mtakatifu na kumtangaza kuwa shahidi wa upendo. Kanisa Katoliki kwa hakika linaheshimu kama mtakatifu wa waendeshaji radio ya wasio na ujuzi, watumiaji madawa ya kulevya, wafungwa wa kisiasa, familia, waandishi wa habari, na hata wafungwa. Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alimfafanua mtumishi wa upendo wa Maria kuwa kama “mlinzi wa karne yetu ngumu."
Siku kuu yake inaangukia katika tarehe 14 Agosti, ambayo kwa hakika ndiyo siku ya kuuawa kwake kishahidi. Kutokana na juhudi za Padre Maximiliani Maria Kolbe kuendeleza ibada kuu ya Bikia Maria, Mtakatifu, anajulikana kama "mtume wa kuwekwa wakfu kwa Bikira Maria.” Kwa hakika Mtakatifu Maximilian Kolbe, anajulikana kwa imani yake ya kina na moyo wa kujitolea. Baadhi ya mawazo yake muhimu zaidi yanahusu upendo, imani katika Mungu, na umuhimu wa kujitolea kwa Bikira Maria. Aliamini kwamba “upendo ndio nguvu pekee ya uumbaji na kwamba kujiamini kulisababisha kushindwa, wakati imani kwa Mungu na Bikira Maria ilikuwa njia ya wokovu.”
Kuna sentensi 7 kati ya nyingi za Mtakatifu Kolbe zinazojulikana sana:
"Usiogope kumpenda sana Bikira Maria Mwenyeheri. Huwezi kamwe kumpenda zaidi ya Yesu alivyompenda."
“Tukumbuke kwamba upendo unaishi na unamwilishwa na sadaka. Upendo unaishi na bila sadaka hakuna Upendo."
"Katika nyakati zetu, tunaona, hazikozi huzuni, na kuenea 'kutojali.' (...) Hangaiko letu la kwanza kabisa lazima liwe kumpa sifa kwa kadiri ya uwezo wetu, tukijua kwamba hatuwezi kumtukuza jinsi anavyostahili.”
"Yeyote aliye na Maria, kama mama yake ana Kristo kama kaka yake."
"Msalaba ni shule ya upendo."
"Kuwa Mkatoliki ina maana: Unapopiga magoti mbele ya altare, ufanye hivyo kwa njia ambayo wengine wanaweza kutambua kwamba unamjua ambaye unampigia magoti."
"Ikiwa Malaika wangeweza kuwaonea watu wivu, wangekuwa na wivu wa kitu kimoja tu: Komunio Takatifu.”