Haiti,Ask.Mkuu Max Leroy Mesidor:Tunamshukuru Papa kwa kuingilia kati Haiti
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Haiti, wamemshukuru Baba Mtakatifu, Papa Leone XIV, kwa kuingilia kati juu ya Haiti wakati wa sala ya Malaika wa Bwana, tarehe 10 Agosti 2025. Baba Mtakatifu Leo mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana alisema “kwamba “hali ya watu wa Haiti inazidi kuwa mbaya. Kuna ripoti za mara kwa mara za mauaji, vurugu za kila aina, biashara haramu ya binadamu, uhamisho wa kulazimishwa na utekaji nyara.” Ninatoa wito wa dhati kwa wale wote waliohusika na kuachiliwa huru mara moja kwa mateka, na ninaomba uungwaji mkono madhubuti wa jumuiya ya kimataifa ili kuunda hali ya kijamii na kitaasisi ambayo itawawezesha Wahaiti kuishi kwa amani.”
Kwa njia hiyo kwa kupitia Askofu Mkuu Max Leroy Mesidor, wa Jimbo Kuu Katoliki la Port-au-Prince nchini Haiti alisema: “Tunamshukuru Baba Mtakatifu kwa kilio hicho kwa ajili ya watu wa Haiti, kwa wito wake kwa Jumuiya ya Kimataifa ili waweze kushugulika kwa kiasi kukubwa na kwa dhati juu ya hali halisi ya Haiti.” Wito huo unafafanua msisitizo wa Baba Mtakatifu kwa watu katika matatizo kwa waathirika wa ukosefu wa haki, wa vita, na wa vurugu. Papa Leo XIV, anakuwa mwangwi wa sauti ya Kanisa la Haiti, ambaye haichi kuomba kuisha kwa vurugu na kuwa na dhamiri kwa wale ambao wanapanda maombolezo ya familia na ya watu wote ambao wanawasaidia kwa namna moja au nyingine. Hakika, Kanisa la Haiti linabainisha kuwa "uhalifu haujui tena mipaka yoyote katika nchi yao. Utekaji nyara wa watu nane, akiwemo mtoto kutoka kituo cha watoto yatima cha Mtakatifu Helena huko Kenscoff, unashuhudia hili. Kitendo hicho cha kinyama ni mojawapo ya dalili nyingi za kushindwa kwa Serikali na kwa jamii inayopoteza maisha na utu wake."
Matumaini ya Kanisa la Haiti
“Ni matumaini kwamba kilio hiki kutoka kwa Papa kitasikilizwa na mamlaka ya Haiti na jumuiya ya kimataifa. Hata hivyo wamefanya mikutano mingi juu ya hali halisi katika nchi, lakini matokeo yanahitajika sana. Kikosi cha usalama cha kimataifa kimekuwa na matokeo kidogo sana. Kina upungufu mkubwa wa wafanyakazi na rasilimali za vifaa. Kilio hiki kutoka kwa Baba Mtakatifu lazima kisikike kwanza kabisa katika mioyo ya Wahaiti, kwa sababu ni juu yetu kwanza kabisa kuandaa nchi kwa kutekeleza mpango wa pamoja, kukuza mazungumzo kwa njia isiyo ya vurugu na ya haki. Ili kuwe na mazungumzo, ili kuwe na mkutano wa kitaifa, bunduki lazima zinyamaze. Ni lazima tuachane na vurugu.”
Kuungana kwa sala ili Mungu awasaidie watu wa Haiti
“Tunamshukuru Papa Leo kwa moyo wote. Tunaungana naye maombi yetu ili Mungu awasaidie watu wa Haiti wajikomboe kutoka kwa minyororo yote inayozuia maendeleo yao. Hasa vurugu za makundi yenye silaha, ukosefu wa mwamko wa kizalendo, na mapambano madogo ya kutaka madaraka na pesa. Jubilei hii ya matumaini iimarishe imani ya watu wa Mungu nchini Haiti. Jubilee na ilete wakati wa neema na baraka kwa ajili yetu, Wahaiti. Kwa maana matumaini katika Mungu hayakatishi tamaa.”