Papa Leo:Vita viishe na Watu wa Haiti waishi kwa amani!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Dominika tarehe 10 Agosti 2025 akiwa katika dirisha la Jumba la Kitume, kwa kuwageukia waamini na wahujaji waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, mjini Vatican, mara baada ya Tafakari alitoa miito kadhaa iliyotazama Ulimwengu mzima. Papa alianza kusema: “Ndugu wapendwa tuendelee kuomba ili vita vikomeshwe. Maadhimisho ya miaka 80 ya milipuko ya mabomu ya Hiroshima na Nagasaki yameamsha tena ulimwenguni kote kukataliwa kwa vita kama njia ya kusuluhisha mizozo. Wafanya maamuzi wakumbuke kila mara wajibu wao kwa matokeo ya uchaguzi wao kwa idadi ya watu. Wasipuuze mahitaji ya walio hatarini zaidi na hamu ya ulimwengu kwa amani.
Pongezi kwa Armenia na Azerbaijan
Kwa maana hiyo Papa Leo XIV aliongeza: "ninazipongeza Armenia na Azerbaijan, ambazo zimetia saini Azimio la Pamoja la Amani. Ninatumaini kuwa tukio hili linaweza kuchangia amani thabiti na ya kudumu katika Caucasus Kusini.” Hilo ni tukio hilo lililofanyika tarehe 8 Agosti 2025 kwa kutiwa saini, huko Washington Marekani, katika Ikulu ya nchi kwa tamko la pamoja kati ya Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinian na Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev.
Wito kwa ajili ya kusitisha vurugu huko Haiti
Kinyume chake, Papa aliongeza tena kwamba “hali ya watu wa Haiti inazidi kuwa mbaya. Kuna ripoti za mara kwa mara za mauaji, vurugu za kila aina, biashara haramu ya binadamu, uhamisho wa kulazimishwa, na utekaji nyara.” Ninatoa wito wa dhati kwa wale wote waliohusika na kuachiliwa huru mara moja kwa mateka, na ninaomba uungwaji mkono madhubuti wa jumuiya ya kimataifa ili kuunda hali ya kijamii na kitaasisi ambayo itawawezesha Wahaiti kuishi kwa amani.”
Salamu mbali mbali
Kwa kuhitimisha, Papa Leo alitoa salamu zake: “Nawasalimu ninyi nyote, waamini wa Roma na mahujaji kutoka nchi mbalimbali, hasa wale kutoka Woodstock, Georgia, Marekani, na wale wa Majimbo ya Down na Connor nchini Ireland. Ninawasalimu washiriki wa Operesheni Mato Grosso, kutoka miji mbalimbali ya Italia, na vikundi vya Parokia ya Stezzano, Medole, na Villastellone. Asanteni wote kwa uwepo wenu na maombi yenu. Dominika njema!