MAP

Injili ya Dominika ya 21 Mwaka C,Yesu  Kristo ni Mlango mwambamba. Injili ya Dominika ya 21 Mwaka C,Yesu Kristo ni Mlango mwambamba. 

Dominika ya 21 ya Mwaka C:“Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba”

Katika kujitahidi kupunguza unene na uzito wetu kwa kuuishi ukweli wa Injili hatupo peke yetu, tunaye Kristo aliye Bwana,Mungu na Mwalimu tunaye Mama Maria Msaada wetu Wakristo na Makimbilio yetu wakosefu.Tunao watakatifu walio waombezi wetu,tusali tukiomba maombezi yao kusudi kama wao walivyotosha kwenye mlango ule mwembamba na sisi tuje tutoshe hapo na kuingia kwenye furaha za uzima wa milele mbinguni saa yetu itakapofika,alleluia.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa radio vatican leo Dominika ya 21, “Jaribu kuingia kupitia mlango mwembamba…” (Lk 13:24) na kuonya kwamba vitongoji vya Ufalme vimejaa watu waliochoka na waliowahi kuamini.Si kila anayeniita ‘BWANA, BWANA…’ ataingia” – inahimiza unafiki wa imani iliyonyooka.“Watakuja kutoka magharibi, mashariki, kaskazini, kusini” inaonesha kuwa wokovu si mali au sehemu, bali ni huruma iliyopewa kwa Mataifa yote. Unapomtafakari Mwinjili Mathayo utaona mara nyingi Kristo anatumia lugha kali dhidi ya wadhambi, mara kadhaa amegusia moto wa gehenna, kuwatenga watu kana kwamba ni kondoo na mbuzi na kuwaadhibu hao “mbuzi” na mara 6 ametaja “kulia na kusaga meno”, H-uyo ni Yesu wa Mathayo…

Mwinjili Luka kwa upande wake, daima anamwonesha Yesu mpole, mwenye huruma, rafiki ya watoza ushuru na wadhambi, Jirani ya akina mama, Mfariji wa wagonjwa na Mchungaji anayewatafuta kondoo waliopotea… ni leo tu tunashuhudia maneno makali ya Yesu kama katika Mathayo yanayotusisimua na kupapaa damu mishipani… jaribu kufunga macho ufikiri unaona kamlango kembambaa, watu wanagombania kuingia hawawezi, wanafaulu wachache tu, halafu muda fulani mwenye nyumba anafunga  mlango, halafu kunakuwa na kelele nyingi, umuone akilini mwako mwenye nyumba anavyojibu kwa kejeli na bila kujali ‘siwajui, ondokeni kwangu…’ halafu ona kilio na kusaga meno kunakofuata!!

Yesu anatushauri kupita mlango mwembamba
Yesu anatushauri kupita mlango mwembamba

Jamani, huyu Yesu vipi? amesahau kuwa na huruma? upole wake umekwenda wapi? iwaje abamize mlango mbele ya watu waliomfahamu na waliomwalika mara nyingi kwenye shughuli zao? ni nini anachotaka kutufundisha kwa maneno haya ya kupita mlango mwembamba na tabia hii ya kuwafungia watu milango? Sehemu hii ya Injili haioneshi kabisa kama ni Habari Njema, ni vitisho tu nawe unaweza kata tamaa kabisa. Lakini si hivyo... Kristo anao ujumbe mzuri kwa kila mmoja wetu… Mtu mmoja alimuuliza “watakaoingia mbinguni ni wachache?” ni swali juu ya mwisho wa nyakati. Kristo anabadili swali hilo na kuliweka katika uhalisia wa sasa, hazungumzii mambo ya mwisho wa nyakati ila namna ya kuingia mbinguni kwa njia ya maisha ya leo, yaani namna ya kuwa mfuasi kamili na katika hilo sharti ni ku “jitahidi kadiri ya uwezo wako kupitia mlango ulio mwembamba, sababu wengi watataka kuingia wasiweze.” Ili ufaulu namna ni moja tu, kupunguza unene, basi! Kumbe tatizo sio maneno makali ya Yesu, tatizo sio kulia na kusaga meno, tatizo ni UNENE.

Kama wewe ni mnene pole yako hutaweza kupenya, kamlango ni kadogo mno! Utajaribu mbinu zote, moja kwa moja, hakuna! tumbo kubwa mno. Upandeupande hakuna! kwa kutanguliza kichwa, haisaidii… linalohitajika ni moja tu, kuwa mwembamba! Maneno ya Kristo yana nia njema nasi, anatukumbusha kufanya “dayati” na kupunguza kilo, mfano za kiburi, na badala yake kuvaa unyenyekevu. Wengi tunataka ukubwa, umaarufu, heshima, hatuna majitoleo, hatutaki mabadiliko, tuna mitazamo yetu tu, huo ndio unene tunaotakiwa kuuondoa kusudi tutoshe pale mlangoni...

UFAFANUZI: Papa Leo XIV katika muhadhara wa Mkesha wa Sherehe ya Pentekoste alisisitiza “Roho Mtakatifu hufungua mipaka ya mioyo, kuondoa uzito wa kibinafsi, na kutupeleka katika upendo unaoleta undugu... Kipeo cha Kanisa kimekuwa amani pale ambapo hakuna ukuta au mgonjwa wa hofu ndani yake.” Mwenye nyumba anapofunga mlango yanazaliwa makundi mawili: la kwanza wapo nje na la pili wamo ndani. Wale wa nje hali zao mbaya, wajeuri na wanasumbua kwa kelele nyingi “tulikula na kunywa mbele yako...’ ‘tulitoa hata pepo kwa jina lako” (Mt 7:22), Mwenyewe hafungui wala nini, anawaita “wafanyaji wa udhalimu”. Hawa sio wapagani, wanamfahamu sababu wamesema walikula naye, ni wakristo hawa. Kumbe wapendwa haitoshi tu kubatizwa na kuandikwa kwenye rejista za sakramenti ofisini, tunatakiwa kufanya “dayati” na kujipatia wembamba wa kufaa.

Mlango mwembamba na mpana , "fanya uchaguzi"
Mlango mwembamba na mpana , "fanya uchaguzi"

Kundi la II wapo ndani. Kristo amewataja Ibrahim, Isaka, Yakobo, manabii na watu kutoka mashariki na magharibi, kaskazini na kusini. Hawa walitosha kwenye kale kamlango, waliuishi ukweli, walishika imani, walitenda mema, hawakusengenya, walimtakia kila mtu mema, walibariki, hawakulaani, walishika amri na kutimiza mapenzi ya Mungu hivi hawakuwa wanene wakatosha sentimita zile chache za mlango ule. Kupitia mlango mwembamba ni kuishi wito tulioitiwa na kutumia karama tulizojaliwa kwa manufaa ya wote. Je, Mkristo, wewe u mnene au u mwembamba? Unapojitathmini unajiona kutosha kwenye mlango wa ukubwa gani? itakuwa kichekesho kuniona nahitaji geti zima niweze kupita! Kuna vyanzo kama saba (7) hivi vya mahangaiko duniani vinavyopelekea kushindwa kupita kwenye mlango ule navyo ni ubaguzi, usasa, ukale na ujadi, kuchanganya imani, dhambi binafsi, sababu nje ya uwezo wetu, makanisa na vyama vya kidini visivyotulia.

Watu wa ndoa kwa mfano mnaufahamu mlango mwembamba wa kupitia? ni upendo tu, msamaha na shukrani... walau leo tu isipite bila kumwambia unampenda kuliko wote na nyakati zote, popote. Katika kujitahidi kupunguza unene na uzito wetu kwa kuuishi ukweli wa Injili hatupo peke yetu, tunaye Kristo aliye Bwana, Mungu na Mwalimu tunaye Mama Maria Msaada wetu Wakristo na Makimbilio yetu wakosefu. Tunao watakatifu walio waombezi wetu, tusali tukiomba maombezi yao kusudi kama wao walivyotosha kwenye mlango ule mwembamba na sisi tuje tutoshe hapo na kuingia kwenye furaha za uzima wa milele mbinguni saa yetu itakapofika, alleluia.

Domenika ya 21 ya mwaka C
23 Agosti 2025, 11:42