MAP

2025.08.02 Jubilei ya vijana: Mkesha wa sala huko Tor Vergata. 2025.08.02 Jubilei ya vijana: Mkesha wa sala huko Tor Vergata.  (@Vatican Media)

Dominika ya 20 Mwaka C:Thamani ya Msalaba kwa Mkristo!

“Kwa jina la Msalaba,juu ya Msalaba,kwa njia ya Msalaba na kwa sababu ya Msalaba,utajiri wa ukombozi tulioupoteza tumeurudishiwa”(Mtakatifu Andrea wa Crete).Huu ndio Msalaba katika maisha ya Kikristo,ambao hatuna budi kuupokea na kuubeba pamoja na Kristo kwa maana ujumbe ulio katika Msalaba ni hai,ukombozi,upatanisho na amani.Na ni kwa kuubeba Msalaba pamoja na Kristo tutastahilishwa kuungana naye katika maisha ya milele mbinguni.

Na Padre Paschal Ighondo –Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 20 ya mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe mkuu umejikita juu ya thamani ya mateso katika maisha ya kikristo, kwani ni kwa mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo, sisi tumekombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mauti na tumefanywa warithi wa uzima wa milele. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unasema hivi; “Ee Mungu, ngao yetu, uangalie, umtazame uso Kristo wako. Hakika siku moja katika nyua zako ni bora kuliko siku elfu” (Zab. 84:9-10). Na mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali; “Ee Mungu, umewawekea tayari wale wakupendao mema yasiyoonekana. Utie mioyoni mwetu hamu ya kukupenda, ili kwa kukupenda katika mambo yote na kuliko yote, tupate ahadi zako tunazotamani kupita yote”.

Mkesha wa Jibilei ya vijana
Mkesha wa Jibilei ya vijana   (ANSA)

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Yeremia (Yer 38:4-6, 8-10). Nalo ni simulizi la mateso aliyopata Nabii Yeremia kwa kutabiri kutekwa na kuangamizwa kwa mji wa Yerusalemu, kama watu wake hawataacha dhambi zao na kumrudia Mungu. Watu maarufu na wakuu wa Yuda waliofaidika na hali hii ya kumuasi Mungu, walichukizwa na utabiri huu, wakamwendea mfalme Sedekia, wakamshawishi ili Yeremia auawe. Mfalme Sedekia badala ya kutimiza wajibu wake, alimtoa Yeremia, akamkabidhi kwa adui zake, wakamchukua wakamtupwa katika shimo lenye matope, akateseka humo kwa njaa. Mungu alimwokoa kwa mkono wa Ebedmeleki, Toashi wa Ethiopia, mtu ambaye kwa wayahudi alidharauliwa. Na utabiri wa nabii Yeremia ulitimia kwa mji wa Yerusalemu kuangamizwa na watu wake kuchukuliwa mateka.

Mababa wa Kanisa wanalitazama kwa imani tukio hili kama mfano wa mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo. Na ujumbe kwetu sisi ni huu; tuwe wasikivu kwa maonyo yanayotolewa na viongozi wetu wa kiimani tunapokuwa tumekengeuka, wakituita tumrudie Mungu aliye kimbilio na kinga yetu. Tusipowasikiliza, matokeo yake ni kuangamia milele. Ni katika muktadha huu wimbo wa katikati unasema hivi; “Ee Bwana, unisaidie hima. Nalimngoja Bwana kwa saburi, akaniinamia, akakisikia kilio changu. Akanipandisha toka shimo la uharibifu, toka udongo wa utelezi; Akaisimamisha miguu yangu mwambani, Akaziimarisha hatua zangu. Akatia wimbo mpya kinywani mwangu, ndizo sifa zake Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa, nao watamtumaini Bwana. Nami ni maskini namhitaji, Bwana atanitunza. Ndiwe msaada wangu na wokovu wangu, Ee Mungu wangu, usikawie” (Zab. 39:13, 1-3, 17).

Mkesha wa sala kwa  vijana huko Tor Vergata
Mkesha wa sala kwa vijana huko Tor Vergata   (@Vatican Media)

Somo la pili ni la waraka kwa Waebrania (Ebr 12:1-4). Sehemu hii ya waraka huu kwa kuweka bayana taabu na mateso yaliyowapata waamini wakristo na jinsi walivyovumilia, wakifuata mfano wa Kristo Yesu aliyevumilia yote hata kufa msalabani, naye baada ya kufufuka kwake alipaa mbinguni na kuvikwa taji ya utukufu, nao pia walivikwa taji la utukufu mbinguni. Nasi tukivumilivu vivyo hivyo bila kuchoka, tukivipigana vita dhidi ya dhambi hata ikiwa ni kwa gharama ya damu yetu, tutastahilishwa kuurithi utukufu wa uzima wa milele, usioweza kufananishwa na gharama ya kitu chochote kile. Zaidi sana tunakumbushwa kuwa maisha yetu, ya kiroho au kimwili ni mapambano. Na mafanikio yoyote katika maisha yanahitaji juhudi na maarifa na kusali kwa bidii ili kupata maelekezo na miongozo kutoka kwa Mungu aliye asili ya mema yote.

Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk 12:49-53). Katika sehemu hii ya Injili tunasikia maneno magumu na ya kutisha aliyoyasema Kristo Yesu. Tunasoma hivi; “Mnadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Hata kidogo, si amani bali utengano. Na tangu sasa, jamaa ya watu watano, itagawanyika, watatu dhidi ya wawili, na wawili dhidi ya watatu” (Lk 12:51). Licha ya ugumu wake na kutisha kwake, ujumbe wake ni huu; Maisha ya kumfuata Kristo yanahitaji kufanya maamuzi magumu, ikiwa ni pamoja na kuachana na kutengana, na yote yaliyo kinyume na ujumbe wa Injili, ikiwemo ndugu, jamaa na marafiki. Hali hii na maamuzi haya yanaleta mateso yenye thamani ya ukombozi katika maisha ya mkristo. Nayo ni baraka, zawadi na shule ya utakatifu, nasi hatuna budu kuyavumilia na kuyabeba, ndio msalaba wetu. Hii ni kwa sababu mateso yakipokelewa kwa imani yanavyomuweka mwanadamu karibu zaidi na Mungu muumba wake.

Watakatifu wengi wanashuhudia ukweli huu. Mtakatifu Francis wa Assisi anasema; Msalaba au mateso ni daraja letu la kumwona Mungu kama tukiyatambua, tukayapokea kikristo kwa moyo wa Imani na kuyabeba pamoja na Kristo, na kuruhusu mapenzi ya Mungu yatendeke katika kuteseka kwetu. Mtakatifu Ignasi wa Antiokia anasema; “Mkristo anafananishwa zaidi na Kristo na kushiriki kikamilifu kazi yake ya ukombozi anapovumilia mateso ya maisha yake kwa imani. Mateso na kifo kwa vyenyewe havina uzuri wala faida yoyote. Lakini vikipokelewa kwa imani na mkristo, vinapata kuwa visakramenti, kwani vinakuwa alama ya mateso na kifo cha Yesu Kristo; na hivyo vinapata thamani tele mbele za Mungu”. Anasisitiza kusema; “nilipo karibu na upanga, ndipo nilipo karibu na Mungu, nilipo pamoja na wanyama wakali, ndipo nilipo pamoja na Mungu”. Akiwa safarini kwenda kuyakabili mateso aliwaambia waamini wake; “mniombee ili minyororo hii inisaidie kumpata Mungu”. Akasisitiza; “kama vile kito kisivyoweza kung’arishwa bila msuguano, vivyo hivyo hakuna mtu anayeweza kufanywa mkamilifu bila kutoa machozi na hapatakuwepo na utakatifu ambao hauna alama ya muhuri wa mateso ya Yesu”.

Wakati wa Mkesha
Wakati wa Mkesha   (@Vatican Media)

Mtakatifu Bakhita alipoambiwa anataka kuwa mtawa kwa sababu ya hofu ya kuendelea kuwa mtumwa alisema: “nikikutana na wale walioniuza pamoja na aliyeninunua na kunifanya mtumwa, nitapiga magoti kwa furaha na kuibusu miguu yao, kwani ni kwa mateso yao nimemtambua Kristo, ni kwa msaada wao nimekuwa mkristo.” Mtakatifu Vinsenti wa Paulo anasema; “inampendeza Mungu kumpatia mateso yule aliye imara katika upendo wake, hivyo kuchukua mateso na kunyamaa ni njia bora ya kujipatia fadhila na kumtukuza Mungu. Mateso ni mtihani wa Imani, ambayo kwayo twajifunza pia kutambua thamani ya wengine. Tena, ukiingizwa mwenyewe katika udhaifu wa majaribio, utawafahamu wengine vizuri zaidi”.

Mtakatifu Katarina wa Siena anasema: “hakuna mapendo yasiyo na mateso. Msalaba japo ni ishara ya mateso, vivyo hivyo ni ishara ya matumaini na mapendo kwetu. Linalobaki ni kuuangalia, kuutafakari, kuushangaa, kuusikiliza, kuuheshimu, kuutukuza na kuuabudu kwa matumaini na mapendo ya kina kwa kuwa ndio wokovu wetu, ni nguvu ya Mungu (1Kor 1:18). Msalaba unatufunulia na kutufundisha juu ya Hekima kuu ya Mungu. Msalaba unatufundisha siri ya Mungu. Msalaba unatufunulia na unatufundisha juu ya upeo wa upendo wa Mungu kwetu. Msalaba una nguvu ya kuwafanya watu waone ubaya wa dhambi na hivyo kuwafanya wakiri, watubu, waungame, kufanya malipizi na kuacha dhambi. Mtakatifu Andrea wa Crete anasema: “Kwa jina la msalaba, juu ya msalaba, kwa njia ya msalaba na kwa sababu ya msalaba, utajiri wa ukombozi tulioupoteza tumeurudishiwa”.

Wakati wa Mkesha
Wakati wa Mkesha   (@Vatican Media)

Huu ndio Msalaba katika maisha ya Kikristo, ambao hatuna budi kuupokea na kuubeba pamoja na Kristo kwa maana ujumbe ulio katika msalaba ni ujumbe wa uhai, ukombozi, upatanisho na amani. Na ni kwa kuubeba msalaba pamoja na Kristo tutastahilishwa kuungana naye katika maisha ya milele mbinguni. Ni katika muktadha huu kila mkristo anapaswa kuuona Msalaba kama ishara ya mapendo, neema, sala, msamaha na matumaini. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali; “Ee Bwana, uzipokee dhabihu zetu zinazotufanya tushirikiane nawe katika muungano mtukufu, ili tunapokutolea yale uliyotupa, tustahili kukupokea wewe mwenyewe”.  Na katika sala baada ya komunyo anasali; “Ee Bwana, sisi tuliounganika na Kristo kwa sakramenti hii, tunakuomba kwa unyenyekevu rehema yako, tufanane naye hapa duniani, tustahili kushirikiana naye kule mbinguni”.

Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari ya Padre Pascal: Dominika ya XX ya Mwaka C
16 Agosti 2025, 09:44