MAP

Mpango Mkakati wa Miaka mitano 2025- 2030 wa Halmashauri ya Walei Kanisa Katoliki Tanzania. Mpango Mkakati wa Miaka mitano 2025- 2030 wa Halmashauri ya Walei Kanisa Katoliki Tanzania.  (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Mpango Mkakati wa Miaka Mitano: 2025-2030 Halmashauri Walei Tanzania

Mpango Mkakati wa Miaka mitano 2025- 20230 wa Halmashauri ya Walei Kanisa Katoliki Tanzania una lengo la kuimarisha nafasi ya waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa; kulea na kuwezesha vyama, mashirika, na jumuiya za Walei; na kukuza ustawi wa kiroho, kijamii na kiuchumi wa jumuiya ya waamini nchini kote. Mpango huu umejipambanua kwa kuakisi dira pana ya Kanisa Katoliki Tanzania, na unalenga kukabiliana na changamoto za ndani na za kimataifa.

HALMASHAURI YA WALEI - KANISA KATOLIKI TANZANIA, Dar es Salaam.

Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida, ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, tarehe 21 Juni 2025 alizindua Mpango Mkakati wa Miaka Mitano 2025-2030 wa Halmashauri Walei, Tanzania. Alitumia fursa hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai, imani pamoja na utume wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa na hasa zaidi katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa Mpango Mkakati, kielelezo cha utashi wake chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Askofu Mapunda ameomba baraka kutoka kwa Mwenyezi mungu kwa ajili ya Mpango huo Mkakati ili usaidie katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu, ili uwe kweli ni chemchemi ya wokovu na uzima wa milele. Ufuatao ni muhtasari wa Mpango Mkakati wa Miaka mitano 2025- 2030 wa Halmashauri ya Walei Kanisa Katoliki Tanzania kwa lengo la kuimarisha nafasi ya Walei katika Kanisa; kulea na kuwezesha vyama, mashirika, na jumuiya za Walei; na kukuza ustawi wa kiroho, kijamii na kiuchumi wa jumuiya ya waamini nchini kote. Mpango huu umejipambanua kwa kuakisi dira pana ya Kanisa Katoliki Tanzania, na unalenga kukabiliana na changamoto za ndani na za kimataifa, sambamba na kutumia fursa zilizopo kwa ajili ya kukuza umisionari wa Kanisa kwa namna ya ushirikiano, utume wa pamoja, na ushuhuda hai wa imani tendaji.

Uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Miaka minne 2025-2030
Uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Miaka minne 2025-2030   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Utangulizi Halmashauri ya Walei Tanzania (HWT) ni chombo cha Kitume kinachowaunganisha Waamini Walei katika wito na utume wao wa kuyatakatifuza malimwengu (AA 5, 6) katika ngazi zote kuanzia Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo (JNNK) hadi Taifa. Aidha, Vyama, Mashirika na Jumuiya za Kitume (VMJ) kulingana na Katiba ya Halmashauri ya Walei Tanzania toleo la 2019 hufanya kazi chini wa mwavuli wa Halmashauri ya Walei katika ngazi husika (HWT, 2019). Bila kuingilia karama za Chama, Shirika, wala Jumuiya ya Kitume, Halmashauri ya Walei katika ngazi husika, hutoa ushirikiano kwa kutoa ushauri, kuvitia moyo, kuviimarisha na kuvielekeza pale inapobidi. Katika ngazi ya taifa, Halmashauri ya Walei Tanzania ilianzishwa rasmi tarehe 24 Juni 1969 chini ya mwamvuli wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kupitia Idara ya Utume wa Walei chini Kurugenzi ya Kichungaji. Halmashauri hii iliundwa kwa madhumuni ya kuwakilisha Walei katika ngazi ya kitaifa na kuwawezesha kutekeleza kikamilifu utume wa Kristo wa upatanisho, ushirika, na uendelezaji wa uongozi bora ndani ya Kanisa. Lengo kuu la kuanzishwa kwake lilikuwa ni kuwapatia Walei muundo rasmi utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika utume wa Kanisa, kwa mujibu wa maono ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican (Vatican II). Halmashauri ya Walei Taifa inaendeshwa kwa mujibu wa Katiba yake, ambayo iliidhinishwa na TEC mwezi Desemba 2019. Katiba hii inaeleza dira na dhima ya Halmashauri, pamoja na kuweka msingi wa uratibu wa shughuli za Walei katika juhudi za pamoja za uinjilishaji (kupeleka Habari Njema kwa kila kiumbe) na kutakatifuza malimwengu.

Utume wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa
Utume wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1969, Halmashauri ya Walei Taifa imekuwa ikiendesha shughuli zake bila kuwa na Mpango Mkakati rasmi. Kwa zaidi ya miaka 50, uendeshaji wake umejikita zaidi katika uzoefu wa kihistoria, mazoea ya muda mrefu, na mtazamo wa “kuendelea kufanya kazi kwa mazoea,” pasipo mwelekeo madhubuti wa kimkakati. Kukosekana kwa muundo huu wa kina kumesababisha changamoto kadhaa katika kutekeleza ipasavyo majukumu yaliyowekwa katika Katiba ya Halmashauri ya Walei. Hali hii imesababisha nyakati fulani kuwepo kwa hali ya kutoridhika miongoni mwa waamini walei, jambo lililoibua hoja ya kuwa na mwongozo ulio wazi na utaratibu wenye mwelekeo wa kimkakati katika kutekeleza utume wake. Kwa kutambua pengo hilo, Mkutano Mkuu wa Mwaka uliofanyika katika Kituo cha Mafunzo ya Walei cha TEC cha Mwenyeheri Isidore Bakanja tarehe 26 Juni 2021, ulipitisha kwa kauli moja uamuzi wa kuandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Halmashauri ya Walei. Mpango huu unalenga kuweka mfumo wa wazi wa utekelezaji wa shughuli za Halmashauri, ili kuhakikisha kuwa juhudi zake zinaendana na utume wake wa msingi pamoja na wajibu wake wa kikatiba. Kwa mantiki hiyo, Halmashauri ya Walei Taifa inawasilisha Mpango Mkakati wake wa Miaka Mitano (2025–2030) kwa lengo la kuimarisha nafasi ya Walei katika Kanisa; kulea na kuwezesha vyama, mashirika, na jumuiya za Walei; na kukuza ustawi wa kiroho, kijamii na kiuchumi wa jumuiya ya waamini nchini kote. Mpango huu umejipambanua kwa kuakisi dira pana ya Kanisa Katoliki Tanzania, na unalenga kukabiliana na changamoto za ndani na za kimataifa, sambamba na kutumia fursa zilizopo kwa ajili ya kukuza umisionari wa Kanisa kwa namna ya ushirikiano, utume wa pamoja, na ushuhuda hai wa imani.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania

Kwa kujikita kwa mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, na Maandiko mengine ya Kanisa, na ya kiulimwengu yenye umuhimu katika uendeshaji wa shughuli za utume wa walei, Halmashauri ya Walei Tanzania imezindua rasmi Mpango Mkakati wake wa Miaka Mitano (2025/26–2029/30) tarehe 21 Juni 2025 katika hafla iliyoambatana na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Halmashauri ya Walei Tanzania. Uzinduzi huu umefanywa na Baba Askofu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Tanzania, Mhashamu Edward Mapunda, Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida, aliyeambatana na Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Kichungaji-TEC, Padre Clement Kihiyo. Hafla hiyo ilijumuisha wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa Mwaka unaojumuisha Wakurugenzi wa Utume wa Walei wa Majimbo, Kamati Tendaji za Majimbo 36 na Wenyeviti wa Vyama, Mashirika na Jumuiya za Kitume (VMJ) ngazi ya Taifa waliokuwepo. Kwa ufupi Mpango Mkakati huu, uandaaji wake ulikuwa shirikishi na uliandaliwa kutokana na mwanga wa mafundisho ya makala mbalimbali kama Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano na hususan Hati ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican juu ya Utume wa Walei (Apostolicam Auctuositatem); Barua ya Kitume ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo II juu ya Wito na Utume wa Walei (Christifideles Laici); Barua ya Kitume ya Baba Mtakatifu ya Yohane Paulo II kuhusu Kanisa Barani Afrika (Ecclesia in Africa); pamoja na makala mengine yanayohusu Kanisa la Kisinodi, Furaha ya Injili, Laudato si; na dira ya Baraza la Maaskofu Afrika na Madagascar (SECAM), Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Mashariki mwa Afrika (AMECEA) na malengo ya muda mrefu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) bila kusahau nyaraka na miongozo inayohusu ukuaji na uimarishwaji wa Jumuiya Ndogondogo za Kikristo nchini Tanzania na AMECEA kwa ujumla. Yafuatayo ni maudhui mafupi ya Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Halmashauri ya Walei Tanzania.

Halmashauri Walei: Kuwaunganisha waamini wote
Halmashauri Walei: Kuwaunganisha waamini wote

2.     DIRA NA DHIMA (Vision and Mission Statements)

2.1. Dira: Kuwa kitovu cha ubora cha kuishauri ipasavyo Hierakia katika ngazi zote za Halmashauri kuanzia Jumuiya Ndogondogo, Parokia, Dekania, Jimbo hadi Taifa katika safari ya kulipeleka Kanisa mbinguni”

2.2. Dhima: “Kuwaunganisha Waamini Walei katika Wito na Utume wao wa kutakatifuza malimwengu kwa Injili ya Kristo katika ngazi zote kuanzia Jumuiya Ndogondogo za Kikristo hadi Taifa.”

Kwa mujibu wa mafundisho ya Kanisa, Halmashauri ya Walei Tanzania inalenga kuwawezesha walei kushiriki kikamilifu katika utume wa Uinjilishaji, usimamizi wa Kanisa, na mageuzi ya kijamii kwa matendo yanayoongozwa na imani. Dhima yake inalenga kuweka misingi imara ya kiutawala, kichungaji na kijamii kwa ajili ya maendeleo jumuishi ya jamii ya Kikristo, kwa kuzingatia maadili ya msingi ya Kikristo: huduma, haki, mshikamano na utu wa binadamu.

3.     Malengo Mahsusi ya Kimkakati, Mikakati na Ufuatiliaji.

Kukuza roho ya kimisionari na kisinodi
Kukuza roho ya kimisionari na kisinodi   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

3.1. Malengo Mahsusi ya Kimkakati (Strategic Objectives)

1.     Kukuza Uinjilishaji Mpya na wa Kina, na Malezi ya Kichungaji kwa Makundi Yote: Kuboresha kimkakati malezi ya kiroho kwa watoto, vijana, watu wazima na wazee ndani na nje ya majimbo kwa kuzingatia mahitaji yao mahsusi, ili kuimarisha ushiriki wa walei katika utume wa Kanisa.

2.     Kuimarisha Miundo ya Uongozi na Uwezo wa Taasisi ya Halmashauri ya Walei Tanzania: Kuweka mifumo thabiti ya uongozi na utawala, kuratibu shughuli za utendaji kwa ufanisi, na kuimarisha rasilimali watu na fedha ili kutimiza kwa ufanisi dhamira ya Halmashauri.

3.     Kudumisha Umoja na Ushirikiano kati ya Mapadre, Watawa na Walei:
Kukuza maelewano, heshima na mtazamo wa pamoja kati ya watendaji mbalimbali wa Kanisa kwa ajili ya ujenzi wa jumuiya ya waamini iliyo fungamana kwa dhati kulingana na matakwa ya Kanisa la Kisinodi na Kimisionari

4.     Kuendeleza Maendeleo Endelevu ya Jamii ya Kikristo na Vyama, Mashirika na Jumuiya za Kitume za Walei: Kuwezesha waamini (wanawake kwa wanaume na vijana) kielimu, ujasiriamali na mafunzo ya kiufundi kwa njia jumuishi inayojumuisha pia maskini na waamini walioko pembezoni mwa jamii ili jamii iishi kwa hadhi au heshima na udugu.

5.     Kukuza Utunzaji bora wa Mazingira nyumba ya wote na Usimamizi Endelevu wa Rasilimali: Kutekeleza wito wa ‘Laudato si’ ukizingatia Mwongozo wa Utekelezaji wa Laudato si wa AMECEA na TEC. Kwa kufanya hivi Halmashauri ya Walei Tanzania inalenga kutoa elimu ya mazingira (pamoja na masuala ya tabia nchi) na kuhamasisha matumizi endelevu ya rasilimali za aina yote katika ngazi zote za maisha ya Kanisa.

Halmashauri Walei: KLushirikisha waamini wa Vyama na Mashirika.
Halmashauri Walei: KLushirikisha waamini wa Vyama na Mashirika.

3.2. Mikakati ya Utekelezaji

1.          Uinjilishaji wa Kisasa na Malezi Endelevu ya Imani: Kutoa programu mahsusi au kamambe kwa kila kundi la waamini, kutumia mbinu mbalimbali ikiwa pamoja na kutumia teknolojia kwa uinjilishaji kidigitali.

2.          Kuimarisha Taasisi ya Halmashauri ya Walei: Kuwekeza katika mafunzo ya viongozi, ikiwa pamoja na vijana; kuimarisha mifumo ya uendeshaji, kuongeza vyanzo vya mapato, na kuanzisha mfumo madhubuti wa ufuatiliaji na tathmini ikiwa inasimamiwa na watu wenye weledi na mahiri kitaaluma.

3.          Umoja wa Kikanisa (yaani Kanisa la Kisinodi): Kuratibu mikutano ya mara kwa mara ya watendaji (hierakia, watawa na walei), mafunzo ya pamoja, miradi ya kikundi na maadhimisho ya pamoja ya Kanisa Katoliki.

4.          Maendeleo Endelevu ya Jamii: Kuwezesha vyama na jumuiya za walei kuanzisha miradi ya uzalishaji yenye tija na kutoa mafunzo ya kujitegemea kiuchumi ikiwa pamoja na ujasiriamali.

5.          Utunzaji wa Mazingira: Kutekeleza kiukamilifu miongozo ya utunzaji wa mazingira ikiwa pamoja na kuandaa vipindi vya elimu ya mazingira na kuhimiza maisha rafiki katika maeneo mbalimbali ngazi za majimbo na taifa.

Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili.
Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili.

3.3. Ufuatiliaji, Tathmini na Utekelezaji: Utekelezaji wa mpango mkakati huu utafanyika kwa mtindo wa ushirikishwaji kutoka ngazi ya chini hadi juu. Mfumo wa Matokeo Unaozingatia Ufuatiliaji na Tathmini (Results-Based Monitoring and Evaluation-RBM&E) utawekwa kwa ajili ya kupima maendeleo, kutambua mafanikio, changamoto na kutoa mapendekezo ya maboresho. Ripoti zitakuwa zinatolewa kila nusu mwaka katika ngazi ya jimbo na taifa, ili kudumisha uwazi, uwajibikaji, na kuboresha utekelezaji wa mpango.

4.     Bajeti na Mikakati ya Upatikanaji wa Fedha: Utekelezaji wa Mpango huu unakadiriwa kugharimu TZS Bilioni 2.5 kwa kipindi cha miaka mitano, sawa na wastani wa TZS Milioni 500 kwa mwaka. Fedha zitapatikana kupitia mchango wa majimbo, shughuli za ukusanyaji wa fedha kupitia maandiko ya kitaalam, misaada kutoka kwa wadau wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), wafadhili binafsi ndani na nje ya Kanisa, na endapo itahitajika, mikopo kutoka taasisi za kifedha.

5.     Misingi ya Mafanikio na Udhibiti wa Athari (Risks) Zinazoweza Kujitokeza. Mafanikio ya Mpango Mkakati huu yanategemea mshikamano kutoka majimbo yote, ushirikiano wa dhati na wadau, pamoja na upatikanaji wa rasilimali za kutosha. Athari au hatari kama vile kupungua kwa rasilimali fedha, ukosefu wa ushirikiano wa baadhi ya wadau au mabadiliko ya kijamii na kisiasa, zitakabiliwa kwa kutumia mikakati mbadala ya ufadhili na ushirikishwaji mpana wa wadau.

Dira kuwa kitovu cha ubora cha kushauri ipasavyo viongozi wa Kanisa
Dira kuwa kitovu cha ubora cha kushauri ipasavyo viongozi wa Kanisa

6.     Hitimisho: Mpango Mkakati huu ni dira ya mageuzi kwa Halmashauri ya Walei Tanzania kuwa taasisi imara, jumuishi na yenye mwelekeo wa utume, inayowajengea uwezo walei kushiriki kwa ukamilifu katika maisha ya Kanisa na jamii. Mpango Mkakati huu ni ahadi ya pamoja ya kuimarisha na kuendeleza utume wa uinjilishaji, maendeleo endelevu ya kijamii, na ustawi wa kiroho na kiuchumi wa waamini Wakristo kote nchini Tanzania. Kwa kujikita katika mshikamano, uwezeshaji, na usimamizi wa rasilimali kwa njia endelevu, Halmashauri inalenga kulijenga Kanisa hai lenye ushiriki wa dhati wa waamini; na wanaopenda kujitegemea na kujiendesha kwa dhana ya kuondokana na utegemezi. Ushiriki wa majimbo, viongozi wa walei, waamini na wadau wengine wa maendeleo utakuwa msingi wa mafanikio na matokeo ya muda mrefu ya mpango huu. Halmashauri ya Walei Tanzania inatambua kuwa dunia inayotuzunguka inabadilika kwa kasi, na mabadiliko hayo huambatana na changamoto mpya pamoja na fursa mpya. Tutaendelea kuwa na mtazamo wa kubadilika kadiri mazingira yanavyotutaka, tukijibu kwa haraka mahitaji yanayojitokeza na kurekebisha mikakati yetu inapobidi. Mafunzo yatakayopatikana kupitia mchakato wa ufuatiliaji na tathmini ya mara kwa mara yatatuhakikishia kuwa tunaendelea kuwa katika njia sahihi na kufanya maamuzi yaliyo makini katika kila hatua ya utekelezaji. Mwisho kabisa tunamalizia kwa nukuu ifuatayo: “Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?”  LK 14: 28.

Walei Tanzania Mpango

 

15 Julai 2025, 16:31