Makatekista Imarisheni Ulinzi na Usalama wa Watoto Dhidi ya Nyanyaso Mbalimbali
Na Angela Kibwana, Morogoro na Sarah Pelaji, -Vatican.
Mama Kanisa anawakumbuka kwa heshima na taadhima waamini walei waliojisadaka usiku na mchana kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu kwa njia ya mafundisho ya Katekesi. Hawa ni watu waliokuwa na imani thabiti na mashuhuda wa utakatifu wa maisha, baadhi yao wakaanzisha Makanisa na wengine kuitupa mkono dunia kwa njia ya ushuhuda wa kifodini. Hata katika ulimwengu mamboleo kuna Makatekista mashuhuri ambao ni viongozi wa Jumuiya zao na wanasaidia pia kurithisha na ukuzaji wa imani. Kuna jeshi kubwa la wenyeheri, watakatifu na mashuhuda ambao ni Makatekista waliolisongesha mbele Kanisa na kwa hakika wanahitaji kutambuliwa, kwa sababu wao ni utajiri mkubwa na amana ya Katekesi pamoja na historia nzima ya tasaufi ya Kikristo. Tangu baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Mama Kanisa ameendelea kupyaisha shukrani zake kutokana na kuwahusisha watu wengi zaidi katika mchakato wa uinjilishaji, wengi wao wakiwa ni waamini walei. Hawa wamejitahidi kutumia karama na mapaji yao, kiasi kwamba, wanaweza kuitwa kuwa ni “Plantatio Ecclesiae” yaani “shamba la Kanisa” pamoja na ustawi wa Kanisa. Kanisa linawashukuru na kulipongeza Jeshi la Makatekista ambalo limekuwa mstari wa mbele kutangaza, kushuhudia na kurithisha imani ya Kanisa kwa njia ya kazi zao kubwa. Katika nyakati hizi, ambapo wakleri ni wachache sana wa kuhubiri Habari Njema ya Wokovu kwa watu wengi hivi pamoja na kuendelea na shughuli za kichungaji, wajibu na dhamana ya Makatekista ni kubwa zaidi. Rej. AG 17.
Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA, wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo amewaasa Makatekista kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto dhidi ya vitendo vya unyanyasaji ili watoto waishi katika mazingira salama wakiwepo katika maeneo ya Kanisa na kwenye jamii. Askofu Musomba amesema hayo wakati wa Kongamano la Makatekista Kanda ya Mashariki ya Jimbo ya Kuu Katoliki la Dar es Salaam linaloundwa na majimbo 7 yaani: Morogoro, Dar es Salaam, Zanzibar, Bagamoyo, Tanga, Ifakara, na Mahenge na limeadhimishwa katika Jimbo Katoliki Morogoro. Aidha Askofu Musomba amesema kuwa katika nyakati za sasa baadhi ya wazazi wamepoteza mwelekeo wa malezi na makuzi kwa familia zao ambapo mara nyingi hawana tena habari na familia hivyo ni Makatekista pekee ndio wenye bahati ya kukutana na watoto kutoka maeneo mbalimbali ya parokia, hivyo wanapaswa kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto wakati wote wanaposhiriki mafundisho ya Kanisa.Hivyo wanapaswa kutambua kuwa wao si walimu wa dini tu, bali wazazi ambao wana wajibu wa kulea na kutunza watoto, hivyo wanapokuwa katika malezi na huduma ya kutoa elimu ya dini kwa watoto wawe na upendo na ukarimu kuwasaidia watoto wajisikie amani na salama katika Kanisa lao Katoliki badala ya kuwatesa au kuwa chanzo cha kuwanyanyasa kwa namna mbalimbali. “Tunayo nafasi kubwa ya kuwalinda watoto hawa ambao ni nguzo imara ya Kanisa ili wajisikie nyumbani ndani ya Kanisa lao Takatifu Katoliki, naomba mfahamu hilo katika utume wenu,” alisema Askofu Musomba. Hata hivyo aliwaomba Makatekista hao kutafakari kwa kina juu ya wito na utume wao kwa Kanisa, na safari yao ya Ukatekista kwa kumuweka Yesu mbele ambaye ni mwalimu ili awaongoze katika safari yao badala ya kujiingiza kwenye malimwengu kiholela bali wawe wa kwanza kutakatifuza malimwengu hayo.
Hata hivyo alisema kuwa Makatekista hao wanapaswa kufuata msingi wa Yesu ambaye ni Katekista wao Mkuu ndani ya Kanisa, hivyo amewaonya kutojiingiza kwenye mikumbo ambayo inapotosha na kufanya utume wao kutoonekana wa thamani ndani ya Kanisa. Makatekista hao ambao ni watangulizi wa Yesu kila wanapokwenda kama ilivyokuwa kwa Yohane Mbatizaji, hivyo wanapaswa kuwa makini katika utendaji wao ili watu wamuone Yesu kwa utumishi wao uliotukuka katika maneno na matendo yao. Pia wana wajibu wa kujiombea wao wenyewe ili waweze kujitakatifuza Kiroho. Katika ulimwengu ambao unakabiliwa na ongezekeko la madhehebu mbalimbali makatekista hao wanapaswa kusimamia ukweli juu ya mafundisho sahihi ya Kanisa ili kuimarisha imani za waamini kwa mafundisho sahihi ya Kanisa katoliki bila upotoshaji. Kongamano hilo limewakutanisha Makatekista kutoka kanda ya Dar es Salaam kushirikishana mambo mbalimbali ya kiimani Jimboni Morogoro, na kufanya hija kwa pamoja kama ndugu katika Kanisa moja Takatifu Katoliki la Mitume. Alisema kuwa ilikuwa ni hamu ya Maaskofu na Makatekista husika kuungana pamoja kama makatekista si kuungana tu kudai haki kama vyama vingine vya kudai haki, bali ni umoja katika Kristu katika imani, ushirika, ushiriki na umisionari kama kanisa la kisinodi linavyowadai kutembea pamoja kumwelekea Kristo.
Aidha umoja huo unaakisi wito wao kwa sababu kuwa katekista si ajira bali ni wito, kwa hiyo umoja huo unaakisi wito huo ndani ya kanisa na kuwakumbusha kutambua kwamba ukatekista haujaanza na wao, isipokuwa ulianza na Kristu mwenyewe, ambaye alitembea katika vijiji kuwasaidia wenye shida mbalimbali, kuwahurumia na kuwatembelea majumbani mwao na kuwalisha Neno la uzima na chakula cha kimwili ili washibe kimwili na kiroho. Askofu Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA, wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo alisema jambo pekee ambalo wanapaswa kufahamu makatekista hao ni kutambua kwamba licha ya changamoto wanazopitia kwenye utume wao lakini Mungu anadhihirisha kwamba ana mpango nao kwa sababu anawatumia kama vyombo vya kupeleka Injili kwa watu. Amewaomba Makatekista hao wasijidharau kulingana na kazi zao au hija yao ya maisha ya toba bali wawe na mwelekeo mzuri wa kufanya yanayompendeza Mungu kadiri ya mapenzi yake. Kongamano hilo la kwanza kufanyika kikanda limeanza Juni 23 hadi 25 mwaka huu likiongozwa na kauli mbiu isemayo ‘Wote wapatanishwe katika Kristo’ 2kor 5:20 ikiwa ni maandalizi ya kufanya kongamano la kitaifa hapo mwakani 2026.